Takwimu zisaidie kusukuma maendeleo

Muktasari:

  • Takwimu zenye ubora zina sifa kadhaa ikiwemo kuwa mahsusi (specific), zinazopimika (measurable), zinazofikika (attainable), zenye uhalisia (realistic) na zenye muda maalum (time bound).

Kupanga ni kuchagua, bila takwimu zenye ubora hakuna namna unaweza kupanga. Maamuzi yasiyotokana na takwimu sahihi hayawi bora na yenye manufaa kwa anayeyafanya au anaotarajia wanufaike nayo.

Takwimu zenye ubora zina sifa kadhaa ikiwemo kuwa mahsusi (specific), zinazopimika (measurable), zinazofikika (attainable), zenye uhalisia (realistic) na zenye muda maalum (time bound).

Aidha takwimu zenye ubora zinatakiwa ziwe zimekusanywa na mtaalam au wataalam wenye sifa na vigezo vinavyotambulika kitaifa na kimataifa. Baada ya kukusanywa ni lazima zipitiwe ili kuondoa makosa ya kibinadamu, zichanganuliwe na zitafsiriwe katika lugha rahisi kueleweka na watu wote.

Bila takwimu zenye ubora huwezi kupanga mipango ya kimaendeleo yenye tija kwa taifa. Matumizi sahihi ya takwimu zenye ubora huondoa malalamiko katika jamii juu ya mgawanyo wa rasilimali ikiwemo fedha, watumishi na vifaa.

Kwa mfano, kwa kutumia takwimu Serikali inaweza kujenga hoja ya kwanini imeamua kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ikiwamo ujenzi wa barabara, ununuzi wa ndege na utengenezaji wa madawati badala ya kuzielekeza nguvu hizo kwenye huduma za afya, maji au kilimo.

Matumizi sahihi ya takwimu zenye ubora hupunguza maswali na kutoa majawabu yenye ushahidi wa kisayansi ambayo kila mwenye hoja kinzani anatakiwa kujipanga kabla hajaongea hadharani na kupendekeza tofauti na ilivyoamriwa.

Maandalizi ya kujadili na kupitisha mpango na bajeti ya Serikali ni lazima uzingatie na kuungwa mkono na takwimu zenye ubora za mwenendo wa uchumi kwa kuzingatia utendaji wa kila sekta kwa miaka iliyopita na kinachohitajika sasa.

Kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopo, takwimu zinatakiwa zielekeze sekta ipi itengewe kiasi gani cha fedha na mahitaji mengine na si kwa kuzingatia matakwa ya mtu au kikundi cha watu waliopewa dhamana ya kuwasilisha mapendekezo hayo.

Takwimu zenye ubora ni kioo kinachoonyesha uhalisia wa jambo bila kupendelea. Zinabainisha ukuaji, kudumaa na kurudi nyuma katika utekelezaji wa kila katika sekta, idara au taasisi ya umma.

Kujua ukubwa au udogo wa tatizo na nguvu zinazohitajika kuwekezwa ili kulitatua, ni lazima utumie tawimu zenye ubora. Kwa mfano kama kuna shule mbili zenye mahitaji sawa, huwezi kuwapanga walimu 10 kwenye shule moja na kuwapeleka wanne kwenye inayobaki.

Lakini, kama hakuna ama mwenye dhamana ameamua kutozitumia au hajui namna ya kuzitumia takwimu zilizopo, zenye ubora unaohitajika, hili linaweza kutokea na kuleta malalamiko kutoka kwa wananchi na walimu wenyewe kwaababu baadhi watakuwa wanafanya kazi kubwa kuliko wengine.

Kuwa na takwimu zenye ubora inawezekana. Inahitaji utashi wa kisiasa na kuwekeza kwenye rasilimali ikiwemo watu, fedha na vifaa ili zitumike kwa namna ambayo italeta manufaa kwa wananchi wa kila wilaya au mkoa nchini.

Aidha ni lazima pawepo na uelewa sawa kuanzia mifumo ya ukusanyaji wa takwimu hadi usambazaji kati ya watakwimu waliopo katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi na watumiaji hasa watunga sera au wanaopanga mikakati ya idara.

Baada ya Chama cha Watakwimu (Stata) kushindwa kuwaunganisha wanachama wake ni vyema kikaanzishwa chombo ambacho kitakuwa kinasimamia taaluma na weledi wa watakwimu nchini kama ilivyo Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) au Bodi ya Wafamasia.

Sasa hivi watakwimu wamegawanyika katika makundi makuu matatu, kuna watakwimu wa NBS, wa Serikali za Mitaa (Tamisemi) na sekta binafsi. Hawa wote wanahitaji chombo cha kuwaunganisha ili wawe na misingi ya pamoja juu ya takwimu.

Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 inazitambua zaidi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), taasisi na idara za Serikali, taasisi binafsi au mtu binafsi ili mradi zikidhi vigezo vilivyowekwa.

Mipango bila kutumia takwimu zenye ubora ni kupoteza rasilimali ikiwemo muda, fedha au nguvu kazi. Tuwekeze kwenye takwimu na tafiti kwa ajili ya mipango itakayokuwa na tija wakati wote kwa wananchi wanaozitumia.

Hili likifanywa kwa umakini unaohitajika siyo tu litachochea maendeleo ya nchi, bali litapunguza malalamiko ya wananchi, migogoro ya jamii, halmashauru au mamlaka zilizopo, na manung’uniko ya watumishi wa umma waliopo kwenye ofisi tofauti.

Ni wakati sahihi kwa mamlaka za umma kuanza kutunza takwimu za masuala yote muhimu ili zitumike kufanikisha mipango mingi inayoandaliwa kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Zikiwapo takwimu bora katika kila ofisi ya umma, itakuwa rahisi kuhudumia wananchi wenye mahitaji tofauti ndani ya muda mfupi hivyo kuharakisha maendeleo yao.

Umuhimu wa takwimu upo kwenye kila sekta ya uchumi. Wafanyabiashara, wakulima, wafugaji hata wavuvi pia. Kw akutumia takwimu zilizoandaliwa kwa kuzingatia kanuni zote hurahisisha kusimamia mgawanyo wa ruzuku inayotolewa na serikali, ugawaji w amisaada kwa waliokumbwa na majanga au kufanikisha mpango wowote unaotekelezwa.

Takwimu hizi zinahitajika sasa hivi na si suala la kungoja kesho kwani maendeleo ya siku zijazo yatachangiwa na maandalizi mema ya sasa.

Anapatikana kwa namba 0685214949/0744782880 au [email protected].