SAIKOLOJIA : Tambua maneno yasiofaa katika malezi ya watoto unapowaasa

Muktasari:

  • Siku nyigine nilipata bahati ya kusikiliza somo la mwalimu mmoja aliyekuwa akiwafundisha watoto. Yule mwalimu akaanza kuwauliza wanafunzi wake maswali. Mwanafunzi wa kwanza akatoa jibu lisilo sahihi. Mwalimu akasema “Nilijua kuwa huyu mpumbavu asingeweza kupata jibu sahihi. Kutarajia kupata jibu sahihi kutoka kwake ni kama kukamua jiwe kwa kutengemea litatoa maji. Kisha mwalimu akamuuliza mwanafunzi mwingine ambaye alitoa jibu sahihi.

Siku moja nilimtembelea jamaa yangu fulani nyumbani kwake. Niliwakuta watoto wao wawili wanakula. Mmoja alikuwa akimweleza mwenzake jambo fulani. Mara mama akamfokea yule aliyekuwa akiongea kwa kusema “Wewe mjinga funga kopo lako na endelea kula.” Licha ya maneno ya mama kuwa yanakera lakini pia mtoto angeweza vipi kufunga mdomo na kuendelea kula.

Siku nyigine nilipata bahati ya kusikiliza somo la mwalimu mmoja aliyekuwa akiwafundisha watoto. Yule mwalimu akaanza kuwauliza wanafunzi wake maswali. Mwanafunzi wa kwanza akatoa jibu lisilo sahihi. Mwalimu akasema “Nilijua kuwa huyu mpumbavu asingeweza kupata jibu sahihi. Kutarajia kupata jibu sahihi kutoka kwake ni kama kukamua jiwe kwa kutengemea litatoa maji. Kisha mwalimu akamuuliza mwanafunzi mwingine ambaye alitoa jibu sahihi. Hata hivyo, mwalimu yule akacheka sana na kusema “Leo mvua itanyesha. Huyu mpumbavu amepata jibu sahihi!”

Hii ni baadhi ya mifano ya maneno yasiyofaa ambayo wazazi na walimu wanaweza kutumia kwa watoto. Ingawa watoto huvumilia lakini maneno haya huwa na athari katika maisha yao yote. Watoto hujifunza namna ya kuongea au kujieleza kutoka nyumbani na shuleni na hatimaye kutoka katika jamii. Watoto wanaolelewa katika mazingira ya kutukanwa na kusahihishwa makosa yao kwa kukashifiwa hukua na kuwa watu wazima wenye tabia hizo hizo. Tabia za aina hii huweza kuwafanya wapate matatizo kazini, katika ndoa na hata katika jamii kwa ujumla.

Wataalam wa saikolojia huweza kutambua aina ya lugha inayotumika nyumbani kwa kuchunguza jinsi watoto wanavyowasiliana na kuongea na wenzao. Kutokana na madhara ambayo watoto hupata kutokana na jinsi wazazi na walimu wanavyoongea nao, wataalamu wamebaini baadhi ya kauli ambazo hazifai kutumiwa kwa watoto. Zifuatazo ni baadhi ya kauli hizo.

Usingefanya hivi

Baadhi ya wazazi huwavunja moyo watoto wanapofanya jambo fulani vizuri. Wao huwapongeza huku wakiweka neno “lakini”, Kwa mfumo binti wa miaka 8 alisafisha chumba chake vizuri na kutandika kitanda. Mama yake akamwambia “Umefanya vizuri lakini hapo kitandani usingeweka mto mmoja juu ya mwingine” Maneno haya yanamfanya mtoto awaze kama hivi; “Nilidhani nimefanya vizuri, lakini mama alivyosema kumbe sikufanya shughuli hii vizuri.”

Hata hivyo, mzazi napofikiria umri wa mtoto na kazi aliyoifanya je anastahili kukosolewa kwa kosa dogo kama kuweka mtu mmoja juu ya mwingine. Na hata kama angelifanya kosa sio, vyema kumsahihisha wakati ule ule alipofanya kazi nzuri. Ni vyema tungezungumzia wakati mwingine kile ambacho hakukifanya vizuri kati yale mengine mazuri. Aidha, ni vyema kumuuliza maoni yake kuhusu jambo hilo ambalo unaona hakulifanya vizuri. Kwa mfumo kumuuliza “Unaonaje kama badala ya kuweka mtu wa pili juu mwingine ungeuweka kando ya mwingine?”

Usiseme hivyo

Kuna wazazi huwa wana tabia ya kuwambia watoto wao “ Usiseme hivyo” Kwa mfano mtoto mmoja alisema, “Mimi sifurahishwi na tabia ya kaka yangu.” Baba yake akamfokea na kumuonya asiseme hivyo kuhusu nduguye. Alimalizia kwa kugomba kwa sauti “Usirudie siku nyingine.”

Karipio hili halikuwa sahihi kwa mtoto. Linampatia mawazo kuwa hisia zake hazithaminiwi na zinaonekana hazina maana. Tunapowakanusha watoto hivi wanapata mawazo kuwa wao hawana haki ya kueleza hisia zao wala michomo ya mawazo wanayoipata. Kwa mfano katika tukio hili, baba angemuuliza mtoto kwa nini hafurahishwi na tabia ya nduguye.

Kwa kuwapatia fursa za kueleza hisia zao tunawaweka katika mazingira ya kutathimini sababu za hasira zao na tunapata nafasi ya kuweza kujadiliana nao kuhusu hisia zao. Faida ya kuwaonyesha tunawajali ni kutuwezesha sisi kuwapatia mafunzo kuhusu uhusiano mwema.

Umefanya vizuri sana kuliko nilivyofikiria

Kuna mzazi ambaye anamsifu mtoto wake kwa kila anachofanya, hadi wakati mwingi hata mtoto mwenyewe anakosa imani kama sifa zote anazopewa ni kweli. Ni dhahiri kuwa watoto hufurahia kusifiwa kila wanapofanya jambo zuri, lakini wazazi hawana budi kuhakikisha wanakuwa wakweli kwa sifa wanazitoa. Wazazi wanaweza kuwapamba kwa sifa kubwa kama vile “Wewe ni mtoto mwenye akili sana kuliko watoto wenzako” Lakini anapokuwa shuleni walimu na wanafunzi wenzake wanamshutumu kwa kutokuwa na akili na pengine hata akawa anafeli mitihani. Mwanafunzi huyo anapolinganisha sifa za wazazi na za shuleni huigiwa na mashaka kama wazazi wake ni wakweli na kama sifa wanazompa ni sahihi. Sifa hizi za uongo huwa na madhara kwa watoto kwani huweza kuwafanya wakabweteka na wasijibidishe kujiendeleza katika maisha wala kujisahihisha kwa kasoro wanazoweza kuwanazo. Aidha, wanapokua na kuwa watu wazima wakaona hawana sifa walizokuwa wakipewa na wazazi hufadhaika na kukata tamaa.

Huna maana yoyote

Wakati mmoja nilizungumza na mzee mmoja aliye na watoto na wajukuu wengi. Mzee huyo alinambia kuwa mara nyingi watoto huweza kupata hali inayolingana na matamko wanayotoa wazazi wao. Kwa mfano mzazi anayemwanbia mtoto wake hivi. “Kutokana na tabia zako hizi hautokuwa na maendeleo katika maisha bali utakuwa mzururaji.” Kama mzazi atayarudiarudia maneno haya, mtoto anapofeli mtihani shuleni hujiliwaza kwa mawazo kwa kusema “Hata hivyo, nisengeweza kufaulu maana baba na mama huwa wanasema mimi sitopata maendeleo yoyote katika maisha.

Wazazi wanapaswa kuepuka kutumia maneno ya kuwabashiria watoto wao matukio mabaya katika maisha. Wanapokasirika wasizitumie ghadhabu zao kwa kuwadhuru watoto wao kisaikolojia. Lishutumu kosa alilokosa na wala siyo mtoto mwenyewe.