Tanzania ni ya mamilioni ya watu wanaokuja, tuwatunzie nchi yao

Maelfu ya wananchi wakiwa kwenye sherehe ya kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika.Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Jamii yenye shukurani kuhusu uhuru wake, utaiona jinsi watu wake wanavyoishi kwa kuongozana badala ya kutawalana. Kwa Tanzania ambayo amani imekuwa moja ya tunu za nchi, jamii yenye kuheshimu tunu hiyo ingeonekana ikiishi kwa tahadhari kubwa. Tofauti zinapoibuka zinazungumzwa kisha mazingira ya amani yanaboreshwa.

Ipo minong’ono kuhusu maandamano. Inavuma kutoka mitandao ya kijamii. Yapo matamko makali kutoka kwa viongozi wa nchi, wanasema “wanaopanga kuandamana waandamane wakione”. Hii ni dalili kwamba Taifa huru ambalo Desemba 9, mwaka huu litaadhimisha miaka 57 ya uhuru, watu wake hawaonyeshi kuwa na shukurani ya kuwa jamii huru inayojiongoza.

Jamii yenye shukurani kuhusu uhuru wake, utaiona jinsi watu wake wanavyoishi kwa kuongozana badala ya kutawalana. Kwa Tanzania ambayo amani imekuwa moja ya tunu za nchi, jamii yenye kuheshimu tunu hiyo ingeonekana ikiishi kwa tahadhari kubwa. Tofauti zinapoibuka zinazungumzwa kisha mazingira ya amani yanaboreshwa.

Tunaweza kutokuwa na hofu juu ya harakati za maandamano mitandaoni. Hata hivyo, hofu haiwezi kukosekana kwa kuwa siasa zimegeuka uadui. Ikiwa viongozi hawafungui dirisha la mazungumzo na wapinzani wao, hivyo kufanya waishi kama maadui, unaachaje kuingiwa woga?

Kwa hali ilivyo, ni rahisi kupatia kama utasema viongozi wengi wa vyama vya upinzani, wanafurahia kile kinachonadiwa mitandaoni. Vilevile utakuwa umekosea kama utasema kwamba wapinzani wanalaani kuwapo harakati za maandamano.

Dhana hii inajengwa katika msingi kwamba hali ya mshikamano kama nchi si nzuri. Hilo lipo dhahiri kwa kila mwenye kufikiri sawasawa.

Tanzania ya leo haitakiwi kuwa ya kudai ukombozi. Kwamba liwepo kundi la kuhamasisha uhuru wao. Miaka 56 nchi ipo huru upande wa Tanganyika (Tanzania Bara) na miaka 54, Zanzibar. Tanzania ni dola ya vyama vingi vya siasa. Kwa nini wapinzani wanalalamika kuwa mazingira yao ya kisiasa yanakandamizwa?

Tanzania haipaswi kufanana na Ujerumani ya wakati wa utawala wa Nazi (mwaka 1933-1945) ya viongozi na wanaharakati kila upande kusema lake; Tanzania ya sasa Serikali inasema “Hapa Kazi Tu”, wapinzani wanadai demokrasia. Unapaswa kuwa na kauli moja.

Matamko kila siku

Wakati Viongozi wa serikali wakitoa kauli nzito kulaani maandamano, viongozi wa dini wametokeza na kushauri cha kufanyika. Wanaharakati wanasema yao. Waandishi wa habari wanaripoti na kuchambua kadiri wanavyojaliwa. Magazeti yanawekwa tahariri. Suluhu ni moja tu; Kusikilizana.

Lakini viongozi wa nchi na wapinzani wao hawataki kusikilizana. Hawaoni umuhimu wala ulazima wa kuketi na kujadiliana.

Si kwamba hawaoni jinsi ambavyo nchi ilivyo na mgawanyiko usio na sababu. Wamepewa kila mlango wa ufahamu. Macho kazi yake ni kuona tu. Mara nyingi macho huona hatari baada ya vitendo kutendeka. Hata hivyo, masikio wanayo, hivyo wanaweza kusikiliza. Wamejaliwa midomo, kwa hiyo ni utashi wao kuzungumza. Ubongo upo, ni jukumu lao kuutumia kutafakari kwa sura wanayoitaka wao.

Masikio yapo kusikiliza kinachosemwa na wengine. Ubongo unawezesha kutafakari kile ambacho masikio yamekisikia. Kama ndivyo, kwa nini hakuna maelewano?

Haya ndiyo maajabu ya Tanzania ya sasa, ufahamu upo wa kutosha, kwa hiyo ukweli unajulikana miongoni mwa wanaobishana. Kutokuelewana kunamaanisha utashi wao wa kutoukubali ukweli.

Sauti ya Mungu

Ikiwa sauti mbalimbali zenye kushauri hazijasikilizwa. Viongozi wa dini kutoka misikitini na kanisani walishatoa rai yao kuhusu kusikilizana na kuelewana lakini hali bado ngumu. Pengine watu wanataka wasikie sauti ya Mungu ikiwaonya. Bahati mbaya Mungu hajawahi kutoa sauti ikasikika kwa waja. Sauti ya Mungu huonekana kuliko kusikika.

Kipindi cha kudai uhuru wa India, shujaa wa wakati wote wa India, Mahatma Gandhi, aliendesha harakati kwa kaulimbiu ya “Jicho kwa jicho litaiacha dunia nzima ikiwa kipofu”. Tafsiri ni kuwa kila mmoja akiwa anaona, basi dunia itageuka kipofu, yaani lazima wawepo wenye kujifanya hawaoni.

Ni kaulimbiu iliyosheheni ushauri wa kuwapo maridhiano. Kwamba uhuru upatikane bila machafuko. Neno jicho kwa jicho ni sawa tu na jino kwa jino. Kila mmoja akijiona anaweza kung’ata, mwisho dunia itageuka kibogoyo, maana meno yote yataisha kwa kung’atana.

Hayo ndiyo mafundisho pia katika vitabu vitakatifu. Kinyume chake ndiyo sauti ya Mungu huonekana badala ya kusikika.

Sauti ya Mungu ilionekana Rwanda mwaka 1994, ikiwa ni matokeo ya kustawi kwa chuki ya muda mrefu ya ukabila. Watutsi walikuwa wakilalamikia kutotendewa haki na Serikali iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Rais wa muda mrefu zaidi wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana, kwamba ilijenga mfumo wa ukiritimba kwa Wahutu kumiliki kila upendeleo.

Nyakati Watutsi wakilalamika si Habyarimana wala Serikali yake walioelewa kitu, waliziba masikio na walizuia ubongo wao kufikiri.

Kikundi cha waasi cha Rwanda Patriotic Front (RPF), kilipoanza chokochoko baada ya viongozi wake, Paul Kagame na mshirika wake, marehemu Fred Rwigyema kuanza harakati kwenye mpaka Uganda na Rwanda, si Habyarimana, Serikali yake wala upande wa RPF walioona umuhimu wa mazungumzo.

Mwaka 1994 baada ya kutokea mauaji ya kimbari, takriban watu milioni 1.2 walipopoteza maisha, ikiwa ni mfululizo wa matukio ya mauaji baada ya wapiganaji wa RPF kuangusha ndege iliyokuwa imembeba Habyarimana na aliyekuwa Rais wa Burundi, Cyprien Ntaryamira, hayo yalikuwa ni matokeo ya jamii kutotumia ipasavyo milango ya ufahamu.

Watu wakilalamika wasikilizwe. Vilevile ukitaka na wewe usikilizwe, anza kuwasikiliza wenzako. Kagame na RPF walikuwa mbogo baada ya Watutsi kutosikilizwa na utawala wa Kihutu tangu yalipofanyika mapinduzi ya mwaka 1959. Hata hivyo ni Kagame huyohuyo aliposhauriwa na Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete azungumze na waasi wa Rwanda, alikuwa mkali kuliko pilipili kichaa.

Ni sawa na kusema Kagame alishasahau madhara ya kutozungumza kama yalivyojionyesha mwaka 1994. Inawezekana anasahau kwa sababu machafuko yaliyotokea yalimnufaisha yeye binafsi hadi kuwa mtawala wa nchi. Matokeo yake, lipo vuguvugu la Wahutu wanaodai watarejea madarakani Rwanda kama ilivyotokea katika mapinduzi ya mwaka 1959.

Mfano wa Kenya, Tanzania

Kama Kagame alivyomjia juu Kikwete alipomshauri kuzungumza na waasi, ndivyo Angola ilivyovuna mauaji ya watu wengi pamoja na kutengeneza jamii kubwa ya walemavu wa viungo kwa sababu ya kutosikilizana kati ya Serikali na wapinzani. Mazungumzo ni tiba, hilo linafahamika vizuri kabisa. Ubishi na ukaidi vimesababisha hasara kubwa kwenye nchi nyingi.

Hivi karibuni vinara wa kisiasa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye ni Rais wa nchi hiyo na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga walikutana kwa mazungumzo na kutoa tamko la kuondoa mgogoro uliokuwepo tangu Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 8 na kurudiwa Oktoba 26, mwaka jana.

Awali Uhuru alishinda lakini matokeo yalibatilishwa na mahakama. Na uchaguzi ulipopangwa kufanyika Oktoba 26, mwaka jana, Raila na muungano wa vyama vilivyomsimamisha, National Super Alliance (Nasa) walisusia.

Uhuru safari hii pia alishinda kwa idadi kubwa ya kura, licha ya kwamba idadi kubwa zaidi ya wapigakura haikujitokeza kupiga kura. Uhuru aliapishwa kuwa Rais wa Kenya Novemba 28, mwaka jana kwa muhula wa pili mpaka mwaka 2022. Raila kwa upande wale alijiapisha kuwa Rais wa Kenya Desemba 12, mwaka jana.

Hali hiyo jinsi ilivyokuwa, jumlisha na historia ya Kenya hasa kutokana na machafuko baada ya Uchaguzi Mkuu Kenya mwaka 2007, vilevile mgawanyiko wa kikabila, uhasimu unaofahamika wa makabila ya Wajaluo, Wakikuyu na Wakalenjin unapata sintofahamu isiyo na mfano.

Nguvu ya kisiasa ya Raila (Mjaluo), Uhuru (Mkikuyu), wakati Makamu wa Rais, William Ruto ambaye ni Mkakenjin kwa pamoja vinaibua wasiwasi mkubwa.

Hata hivyo, Uhuru na Raila walipokutana walitangaza kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kujenga Kenya iliyo moja. Uamuzi wao umepongezwa na wengi, maana umeiponya nchi. Angalau sasa wananchi wanaishi kwa amani bila wasiwasi wa misuguano ya kisiasa. Hilo lililotokea Kenya limeonwa na viongozi wa kisiasa nchini, ila hawajaonyesha kama wanalo la kujifunza ili kuweka mbele mazungumzo.

Viongozi wa siasa nchini ni wasomi, wanaielewa dunia na historia yake. Wanatambua kuwa kila palipofanyika mazungumzo na amani ilistawi. Wanaelewa kwamba palipokosa kusikilizana, matokeo yalikuwa mabaya.

Wanafahamu heshima ya viongozi waliopenda ushirikiano na mahasimu wao wa kisiasa kama Rais wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, mwanademokrasia Pedro Pires wa Cape Verde na wengine.

Mifano ya wanasiasa wenye heshima kutokana na kupenda masikilizano ipo, vilevile yaliyowakuta watu waliokuwa na kiburi na jeuri. Wana kila mlango wa ufahamu. Tatizo hawataki tu kusikilizana. Huo ndiyo mshangao wa Tanzania ya sasa. Hata hivyo, wakumbuke kuwa Tanzania ni zaidi ya watu milioni 52 waliopo sasa. Tanzania ni ya watu zaidi ya milioni 200 watakaoishi baada yetu. Tusikilizane ili tuwatunzie nchi yao.