Tanzania yetu ni umoja wetu,tuujenge pamoja

Muktasari:

Mkoloni alitawala nchi, miili yetu na fikra zetu. Jukumu hili la kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo lilikuwa ni la kila Mtanzania mwenye upeo wa kuona mbali. Mwalimu Julius Nyerere, kwa kutumia chama cha siasa kilichoshiriki kuleta uhuru, alijitahidi kujenga umoja na kupandikiza uzalendo.

Baada ya kupata uhuru wetu, kazi kubwa ilikuwa ni kuimarisha umoja wa kitaifa na kupandikiza moyo wa kizalendo kwa Watanzania wote. Maana mkoloni alikuwa amefanya kazi ya kuwafanya Watanzania kujichukia, kuchukia mila zao, miungu wao na hata lugha zao.

Mkoloni alitawala nchi, miili yetu na fikra zetu. Jukumu hili la kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo lilikuwa ni la kila Mtanzania mwenye upeo wa kuona mbali. Mwalimu Julius Nyerere, kwa kutumia chama cha siasa kilichoshiriki kuleta uhuru, alijitahidi kujenga umoja na kupandikiza uzalendo.

Tanu na baadaye CCM, kwa wakati ule ilikuwa na picha tofauti, kutojiunga na chama kulionekana kama usaliti. Sababu kubwa ikiwa kwamba wakati wa mkoloni, kuna vyama vilivyounga mkono wakoloni. Kuna vyama vilivyotaka wakoloni waendelee kutawala. Lakini pia kulikuwa na vyama ambavyo, havikulenga kujenga umoja wa kitaifa, vilitaka Tanzania ibaki ni ya watu weusi tu, vilitaka kuifuta historia, kitu ambacho ni kigumu kufanyika.

Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea iliyoanzishwa na Mwalimu Nyerere chini ya Azimio la Arusha, lengo lake kubwa ilikuwa ni kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo. Mwalimu alitaka kutufikisha katika hatua ya kuutanguliza utaifa kabla ya kitu chochote kile. Alitaifisha shule na hospitali za mashirika ya dini ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki sawa.

Vijiji vya ujamaa, Jeshi la Kujenga Taifa na Azimio la Musoma vililenga kumtengeneza Mtanzania mwenye mshikamano na uzalendo. Wakati ule tulikuwa na chama kimoja cha siasa. Ingawa si watu wote waliojiunga na chama cha siasa, ingawa wengi walikuwa na imani juu ya nia ya chama hicho.

Na kusema kweli chama hicho kiliangalia maslahi ya kila Mtanzania – ni tofauti kabisa na sasa hivi tunaposikia misemo ya CCM ina wenyewe. Na kweli kimatendo ni kwamba CCM ina wenyewe.

Na kwa fikra potovu, fikra ambazo ni lazima zifanyiwe kazi kubwa, ni kwamba baadhi ya hawa wana CCM wanafikiri wao ndio Watanzania peke yao na wana haki zaidi ya wengine.

Mwalimu alitengeneza falsafa ya chama kimoja. Aliielezea watu wakaielewa. Watanzania walio wengi walipenda sana mfumo wa chama kimoja, maana waliona umuhimu wake. Lakini hasa waliona umuhimu wa chama cha Mwalimu, ambacho kilikuwa na lengo na kuunda umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo.

Upepo wa kuanzisha vyama vingi vya siasa ulioikumbwa dunia nzima, ulipoingia Tanzania, asilimia 80 ya Watanzania walipenda nchi yetu kuendelea na mfumo wa chama kimoja. Asilimia 20 tu ndio walikubali mfumo wa vyama vingi, lakini Mwalimu akasema hao wachache wasikilizwe.

Bahati mbaya tulikubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi kabla ya kuimarisha umoja wa kitaifa na uzalendo wa kweli. Vitu hivi viwili ni vigumu kuvijenga katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Au niseme kwa maneno mengine, kwamba mfumo wa vyama vingi vya kisiasa unafaa kwa nchi ambayo imefanikiwa kujenga umoja wa kitaifa na uzalendo wa kweli, si chini ya miaka 100.

Nchi changa kama yetu ni vigumu kuendesha siasa ya vyama vingi bila kuleta mtengano na wakati mwingine vita au mapambano ya dola na vyama ambavyo havikushika madaraka.

Baada ya kuwa na mfumo wa vyama vingi kwa kipindi cha miaka 26 sasa, tunaweza kuona wazi kwamba vyama hivi havijengi umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo.

CCM imeendelea kuwa na nguvu na kuendelea kuimarisha “UCCM” badala ya “Utanzania”. Mikakati ya chama hiki kikongwe, kukomboa majimbo yaliyo kwenye mikono ya vyama vya upinzani si ya kuimarisha umoja wa kitaifa. Kinachofanyika ni kupandikiza mapenzi ya chama hadi watu wakakipenda zaidi ya taifa lao.

Hili ni zuri upande mmoja na upande mwingine ni baya. Ni zuri watu kukipenda chama chao, lakini ni baya pale wanachama wanapofikia hatua ya kufikiri kwamba wao ndio wana haki zaidi katika taifa kuliko watu wengine.

Wakati wa mkoloni, kigezo cha kupima uzalendo wa mtu ilikuwa ni uanachama wa chama cha siasa, na hasa chama kilichokuwa kikilenga kuleta ukombozi, kama Tanu, chama ambacho baadaye kiligeuka na kuwa CCM, baada ya kuungana ASP cha Zanzibar.

Mtazamo huu ambao ulikuwa na maana wakati ule umeendelea leo hii. Watu wengi na hasa wale wanachama wa CCM, bado wanafikiri kigezo cha uzalendo ni kujiunga na CCM. Na wana mawazo kwamba yule aliye nje ya CCM ni msaliti.

Tatizo hili limejitokeza kwa vile wimbi la kuanzisha vyama vingi lilikuja kabla ya wakati wake. Lilikuja bila maandalizi. Kwa upande mmoja ni vizuri na kwa upande mwingine ni vibaya. Ni vizuri kwa sababu chama kimoja, kinawafanya watu kuwa vipofu na kushindwa kuona ukweli wa mambo katika jamii.

Vyama vingi vya siasa vinasaidia kufichua dosari na kukifanya chama kinachotawala kisijisahau. Lakini, kwa upande mwingine ni vibaya maana, kinachotokea kuanzisha vyama vingi bila msingi imara, matokeo yake ni kuendeleza chama kimoja, kama ilivyo sasa hivi kwa CCM.

Kama tungelikuwa tumefikia ukomavu wa kisiasa, kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, CCM ingevunjwa kwanza, na vyama vyote vikaanza upya.

Tungeanzisha vyama ambavyo nia na lengo kubwa lingekuwa ni kujenga taifa letu kwa kuleta mshikamano na kuimarisha uzalendo. Vyama vingekuja na sera mbalimbali za kutimiza lengo hilo.

Kwa vile CCM inatokana na vyama vilivyoshiriki kumfukuza mkoloni na ni chama kilichoendelea kutawala hadi tunaingia mfumo wa vyama vingi, kinapata upendeleo wa kihistoria.

CCM, ambayo ilitokana na Tanu, lengo lake la msingi lilikuwa ni kupambana na mkoloni na kuleta uhuru. Kazi hii ilifanyika vizuri. Baada ya hapo iliendelea kufanya kazi ya kuimarisha uhuru. Kwa maoni yangu mimi, kazi hii ingeendelea zaidi ya miaka 50, kabla ya kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa. Maana, tungeanza na mfumo wa vyama vingi tukiwa na agenda tofauti na ile ya ukoloni.

Mwelekeo wa CCM, wa ‘kuchinjachija’ na ‘kuwatupa’ wapinzani, kukomboa majimbo yote, kuwakomboa watu walioikimbia CCM na kuwarudisha kundini, si mwelekeo wa kujenga umoja wa kitaifa na kuimarisha uzalendo. Ni mwelekeo wa kukijenga chama kimoja, ni ishara mbaya kwa siku za usoni.

Tumeshuhudia wabunge na madiwani wakivikimbia vyama vyao vya siasa na kujiunga na CCM, na kwa kufanya hivyo wanatuingiza kwenye gharama kubwa ya kufanya uchaguzi. Lakini kama hilo halitoshi sasa tumeshuhudia mtoto wa chuo kupoteza maisha kwenye harakati hizi za kurudia uchaguzi.

Ni nani aliwaambia askari wetu kutumia risasi za moto katika kutawanya maandamano ya kisiasa. Duniani kote maandamano yanatawanywa kutumia risasi za mpira na maji ya kuwasha. Kwetu hapa Kinondoni, risasi za moto zimetumika. Kwa nini, tunataka kufahamu. Si ule uchunguzi unaofanyika bila kutoa majibu.

Tuelezwe ni kwa nini binti huyu amepoteza maisha yake? Kwa nini kutumia risasi za moto kwa watu ambao hawana silaha ni jambo ambalo halikubaliki ni la kulaani kwa nguvu zote.

Kama tunalenga kujenga umoja wetu, ni lazima sote tupaaze sauti zetu na kulaani tukio hili. Ni lazima mhusika afikishwe kwenye vyombo vya sheria. Tukikaa kimya na kuogopa kusema, tutajenga utamaduni mbaya wa kutumia bunduki kujenga umoja wetu.

Hatuwezi kujenga umoja kwa kukubali kupoteza maisha ya Watanzania. Damu ya binti huyu, ambaye hakuwa hata na ushabiki wa kisiasa, alikuwa kwenye masomo yake, iwe juu ya wale wote walioelekeza risasi za moto kutumika kwenye maandamano ya kisiasa.

Nyakati hizi tulizomo, ni vigumu chama cha siasa kujenga umoja wa kitaifa. Tunahitaji chombo cha kujenga umoja wa kitaifa. Tunahitaji chombo cha kuwakusanya Watanzania wote bila kuangalia mapenzi na imani yao kwenye vyama.

Bila kuwa na lengo moja kama taifa, mfano kama lengo letu la zamani la kumfukuza mkoloni, ni vigumu kuyafikia maendeleo ya kweli. Ni lazima tuwe na chombo cha kutuunganisha, kiasi kwamba Chadema, ikiingia madarakani ifanye kazi na Watanzania wote, bila kuangalia imani zao za vyama.

Ikitawala TLP, ifanye kazi na Watanzania wote bila kuangalia imani zao za vyama. Na ikitawala CCM ifanye vilevile. Chombo hiki ni lazima kiende sambamba na juhudi za kuandika Katiba mpya ya taifa letu.

Rais John Magufuli ni muhimu atambue hili. Pamoja na jitihada zake za kutaka kuijenga upya Tanzania, hawezi kufanikiwa kiasi kizima akifungamana na chama chake cha siasa na kuvimaliza vyama vingine.

Upinzani ni muhimu sana kwenye siasa, bila upinzani mambo mengi yatalala na hakutakuwa na mkosoaji. Ni muhimu Rais atambue kwamba tunahitaji chombo cha kutuunganisha kama taifa, ambacho kinakubalika kwa Watanzania wote.

Mwelekeo wake ulikuwa mzuri, lakini dalili hizi za kuikumbatia CCM, na kukubali mfumo huu wa wawakilishi wa wananchi kubadilishabadilisha vyama, na kuendelea kulikingia mkono jambo hili kutaweka doa kwenye uongozi wake.

Pia, matumizi ya silaha za moto yamekuwa mengi. Watanzania hatukuzoea utamaduni huu. Tumeshuhudia watu wakitishiwa kwa silaha za moto mchana kweupe, watu wakishambuliwa na silaha za moto – wengine wakipotea kama mwandishi wa gazeti hili na wale waliotangulia. Huu ni utamaduni mpya na mbaya ambao hauwezi kujenga umoja wa taifa letu.

Tunahitaji chombo cha kututoa usingizini na kutufundisha kwama chama, si kitu cha kwanza katika taifa, utaifa ndicho kitu cha kwanza na vingine vinafuata. Leo hii chama ndicho kitu cha kwanza na mengine yanafuata. Huku ni kupotoka.

Daima tukumbuke kwamba Tanzania yetu ni umoja wetu na ni wajibu wetu kuujenga umoja wetu.

Padri Privatus Karugendo.

+255 754 633122