MAONI YA MHARIRI: Tukiweka nadhiri, Taifa Stars itakwenda Afcon 2019

Muktasari:

Timu zake zote zilivurunda isipokuwa timu ya wanawake ya Kilimanjaro Queens ambayo ilitwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati katika soka ya wanawake.

Miongoni mwa miaka ambayo Tanzania ilifanya vibaya katika mashindano mbalimbali ni 2016.

Timu zake zote zilivurunda isipokuwa timu ya wanawake ya Kilimanjaro Queens ambayo ilitwaa ubingwa wa Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati katika soka ya wanawake.

Tunaweza kusema angalau wametufuta machozi japokuwa ni mengi na hayafutiki kirahisi.

Watanzania wanataka kuona timu zao zinafika mbali, katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, kwa kuwa kiu yao ni ya muda mrefu kwenye medani ya michezo katika ngazi hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Shirikisho la Soka Afrika, CAF, lilitangaza ratiba ya fainali za Afrika, Afcon kwa mwaka 2019.

Wakati wenzetu wakichuana Gabon, sisi tunaanza kuwasubiri wenzetu hao na kuungana nao baadaye kwa kuitafuta safari ya Cameroon 2019.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Tanzania imepangwa Kundi L ikiwa na timu za Uganda, Lesotho na Visiwa vya Cape Verde.

Ukiangalia haraka haraka, Tanzania inaweza kuwa na nafasi katika kundi hilo ama la, na nafasi inaweza kuwepo ikiwa mkakati utawekwa kwamba lazima fainali za 2019, Tanzania iende Cameroon.

Hatuwezi kwenda Cameroon kama hakutakuwa na maandalizi ya maana, hakutakuwa na mikakati na kama hakuna mshikamano wa pamoja kusema hii ni dhamira ya Tanzania kwamba iwe jua, iwe mvua lazima bendera ya Tanzania ipeperuke Cameroon.

Ratiba imeshatolewa, sasa isichukuliwe kimzahamzaha maandalizi ya timu.

Kufanya vizuri kwa timu inatakiwa maandalizi mazuri na zaidi ni kuipa timu mechi nyingi za majaribio bila kujali Taifa Stars inacheza na nani, kinachoangaliwa ni kiwango cha uchezaji kama kinakidhi kwa wachezaji wetu.

Hata kama Taifa Stars haitakuwa na wachezaji wengi kutoka nje, timu ikipata maandalizi mazuri, mechi nyingi za kujipima nguvu, itafika mbali tu.

Kinachoigharimu Taifa Stars ni kucheza kwa kutojiamini kwa kuwa wachezaji wamezoea mechi za kisiwani za ligi bila kutoka au kukutana na timu mbalimbali za kimataifa kupata ladha tofauti.

Mfano, Taifa Stars ya mwaka 2006/8 pamoja na kuwa haikuwa na mafanikio ya kutwaa ubingwa, ilikaribia kucheza Afcon 2008 kwa kupoteza dakika za mwisho, ilicheza mechi nyingi za kirafiki na ilikata tiketi ya Chan 2009 na kama si uzembe wa wachezaji, timu ingeingia fainali.

Sasa, kuna vitu vingi kwa maandalizi ya timu zaidi ya kuijengea kujiamini kwa kucheza mechi nyingi za kirafiki za kujipima nguvu.

Kwa utaratibu ulioanzishwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa, BMT, kufuatilia kwa karibu vyama vya michezo, tuna imani wataingia ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuona namna gani maandalizi yanafanyika na kadiri muda unavyokwenda kujua yamefikia wapi, na Tanzania inacheza na nani.

Kama alivyosema Naibu Waziri, Anastazia Wambura kwamba 2017 ni mwaka wa ushindi, hiyo pekee ni chachu hadi kwa Taifa Stars kuona inafika mbali hata kucheza fainali za Cameroon 2019.

Wachezaji wa Taifa Stars wanaifahamu vizuri soka ya Visiwa vya Cape Verde, Uganda na labda Lesotho yaweza kuwa ni timu nyepesi, lakini inawezekana soka yao ikawa imebadilika.

Cha msingi ni maandalizi ya mapema, kujipanga na kuweka nia na nadhiri kuwa lazima Taifa Stars iende Cameroon kwa fainali za Afcon 2019.