UCHAMBUZI: Tukubaliane na mfumo wa risiti, upo hadi Ulaya

Muktasari:

Lakini ukweli ni kwamba Wafanyabiashara wa Tanzania watakaofanikiwa kufuata sheria na taratibu wanaweza kwenda kufungua biashara zao hata Ulaya.

Wafanyabiashara wengi sasa wanalalamika agizo la kila bidhaa inayouzwa iwe na risiti yake. Wengi wanalalamikia hata kutumia mashine za kielektroniki (EFD) kwa madai kwamba zinawapunja.

Lakini ukweli ni kwamba Wafanyabiashara wa Tanzania watakaofanikiwa kufuata sheria na taratibu wanaweza kwenda kufungua biashara zao hata Ulaya.

Tatizo la wengi ni kwamba walizoea biashara za kienyeji kwani ipo fursa ya kuzungumza na maofisa wa kodi na kuendelea na biashara bila kulipa kodi kwa mwaka mzima.

Ni lazima wakumbuke kwamba nchi tajiri duniani zinazidi kusonga mbele kiuchumi kutokana na mfumo sahihi wa ukusanyaji wa kodi.

Lakini kwa upande wa Tanzania suala la kulipa kodi linakuwa na utata kila mwaka kutokana na kukosa mfumo mzuri unaowafanya wananchi hususan wafanyabiashara wapende kulipa kodi. Miaka mingi suala la kodi kwa wafanyabiashara lilijulikana kama siyo la lazima bali la hiari, lakini mara kadhaa kodi iliwagusa moja kwa moja wananchi wengi wa kawaida na mali zao ndogondogo.

Kwa ujumla mfumo wa kodi nchini unabadilika kila mwaka kulingana na mtazamo wa wataalamu na hata kiongozi wa juu anavyotaka.

Kwa mfano Watanzania wa miaka ya 80 hadi 90 waliwahi kushuhudia kodi ya kichwa ambayo kila Mtanzania aliyekuwa zaidi ya miaka 18 alikuwa akilipa kila mwaka.

Kodi hiyo ilifutwa baada ya kuonekana ni kero kwa watu wengi kwani baadhi walikuwa wakizihama nyumba zao na kuishi kwenye mapori kwa kuogopa kukamatwa.

Hali kadhalika ipo miaka ambayo kodi iliwekwa kwenye vyombo vyote vya usafiri zikiwamo baiskeli ambazo nazo zilikuwa zikilipiwa kodi kila mwaka. Kodi ya baisikeli ilifutwa enzi za Serikali ya awamu ya tatu kwa maelezo kwamba ina kero kubwa kwa wananchi wa hali ya chini.

Katika kipindi kirefu Serikali imekuwa na uhakika wa kupata kodi kutoka kwa wafanyakazi ambao wanakatwa moja kwa moja kwenye mishahara yao.

Lakini wafanyabiashara mara zote walikuwa wakiguswa kwa masuala ya leseni na kodi ya mapato ambayo nayo utaratibu wake kwa miaka mingi ni majadiliano.

Mwaka huu chini ya Serikali ya awamu ya tano kodi umekuwa tofauti kwa wafanyabiashara wote nchini. Hivi sasa wanaonekana kuguswa sana na kodi kwa sababu ya kutakiwa kutoa risiti kwa kila bidhaa wanazouza. Serikali ya Rais John Magufuli inasisitiza kila mfanyabiashara lazima atoe risiti anapouza bidhaa. Kwa kipindi kifupi wimbo wa risiti umenoga mijini ingawa bado wafanyabiashara wanajiuliza.

Wapo wafanyabiashara wenye maduka makubwa yenye mzunguko kubwa wa mamilioni ya fedha kila siku, lakini hawaamini na wala hawaoni sababu za kutoa risiti.

Kwa mfano, katika Jiji la Mbeya bado watu wengi wananunua bidhaa madukani na kusafirisha mizigo hadi vijijini bila risiti. Wafanyabiashara wengi wanaona fahari wasipotoa risiti kwa mnunuzi.

Lakini ukweli ni kwamba Serikali ya sasa imedhamiria kila mfanyabiashara anapouza bidhaa lazima atoe risiti.

Hivyo ni jambo la lazima kwa wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo na wakubwa kutambua kwamba suala la kulipa kodi au kutoa risiti ni la lazima katika nchi yoyote duniani.

Hakuna nchi ambayo inaruhusu wafanyabiashara kutolipa kodi. Wakati wote wafanyabiashara wa Kitanzania wakumbuke kwamba wakifanikiwa kukua kimtaji kipindi cha Serikali ya awamu hii wanaweza kwenda kufungua biashara katika nchi yoyote ikiwamo Rwanda na hata Ulaya.

Mchambuzi ni mwandishi wa gazeti hili mkoani Mbeya (0767 338897)