MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tunalisubiri kongamano la wadau wa Kiswahili

Tuesday November 21 2017

 

By Erasto Duwe

        Mikakati mingi ikiwa inaendelea kufanywa na Serikali na asasi zake kwa lengo la kukiendeleza Kiswahili.

Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), kimeandaa Kongamano kubwa la lugha ya Kiswahili litakalofanyika Novemba 23 hadi 24 katika Chuo Kikuu cha Dodoma.

Kongamano hilo litawakutanisha wadau mbalimbali wa Kiswahili kutoka Afrika Mashariki na kwingineko.

CHAKAMA ni chama cha Kiswahili kilichoundwa mwaka 2002 kikihusisha nchi za Afrika ya Mashariki, na makao yake makuu yako jijini Arusha, Tanzania.

Lengo kubwa la CHAKAMA pamoja na malengo mengine ni kuratibu, kukuza na kuendeleza utafiti, ufundishaji na utumiaji wa Kiswahili katika Afrika Mashariki katika nyanja zake zote.

Shughuli kubwa zitakazofanywa katika siku hizo za kongamano ni uwasilishaji wa makala anuwai za kitaaluma zihusuzo lugha ya Kiswahili na majadiliano yatakayotawala mada husika.

Wawasilishaji watatoka miongoni mwa Wanachakama walioandaa makala hizo. Mada kuu katika Kongamano hilo ni “Kiswahili na Maendeleo ya Afrika Mashariki.”

Mada hii kuu ina mada ndogondogo ambazo zimefanyiwa tafiti na kuandikiwa makala zitakazowasilishwa katika kongamano hilo.

Miongoni mwa mada hizo ndogondogo ni pamoja na Kiswahili na Utandawazi, Kiswahili na Elimu, Hali ya Kiswahili katika mataifa ya Afrika Mashariki, na Kiswahili na Maendeleo ya Uchumi.

Nyingine ni Kiswahili na Siasa, Kiswahili na Uchapishaji, Kiswahili na Utafiti, Kiswahili na Usalama, na kadhalika.

Makala takriban 105 zitakazowasilishwa katika kongamano hilo na kufanyiwa majadiliano, zinahusiana na maeneo mbalimbali yaliyotajwa katika mada hizo ndogondogo.

Miongoni mwa mada hizo, zipo zile zinazohusu masuala motomoto ya kisasa yanayoibuka mathalani kuhusu maendeleo ya lugha na changamoto anuwai zinazokikabili Kiswahili.

Aidha, mada hizo zinahusiana na matumizi ya Kiswahili katika nyanja mbalimbali kama mada hizo ndogondogo zinavyojipambanua.

Kiswahili kwa wakati huu, kimepewa hamasa kubwa kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali ndani na nje ya Afrika.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kwa vitendo katika matukio ya kitaifa na kimataifa.

Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika moja ya vikao vya Bunge alionyesha bayana nia ya Serikali ya kukiendeleza Kiswahili kimataifa.

Alieleza kuwa, Serikali itawatuma wakalimani watakaofanya ukalimani wa hotuba za viongozi mbalimbali watakaoiwakilisha Tanzania katika mikutano ya kimataifa sehemu mbalimbali nje ya nchi.

Aidha, Bunge la Afrika Mashariki nalo tayari limekifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika vikao vyake.

Halikadhalika, idadi ya vyuo vikuu vinavyofundisha Kiswahili huko ughaibuni, inazidi kuongezeka siku hadi siku na raghba ya wageni kujifunza Kiswahili imeongezeka maradufu.

Mwenyekiti wa CHAKAMA Afrika Mashariki, Dk Mussa Hans, anatoa wito kwa wanachama, wadau na wapenzi wote wa Kiswahili kushiriki kwa wingi katika kongamano hilo ili kuweza kujadili na kuzidi kukiimarishia Kiswahili misingi yake kama taaluma lakini vilevile kama lugha ya mawasiliano na utandawazi.     

Advertisement