Tusijenge wala tusivunje ukuta, tulinde amani yetu

Muktasari:

  • Serikali imekuwa na mvutano na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa muda sasa tangu chama hicho kilipotangaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kupinga kile ilichokitaja kuwa ukandamizwaji wa demokrasia nchini.
  • Mikutano na maandamano hayo yatakayofanyika Septemba Mosi yamepewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
  • Jeshi la Polisi lilitangaza kupiga marufu mikutano na maandamano hayo na tayari viongozi kadhaa wa chama hicho wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za uchochezi.
  • Licha ya viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini kutaka Serikali ikutane na viongozi wa Chadema ili suluhu ipatikane, hakuna maridhiano yaliyofikiwa mpaka sasa.

Maadalizi ya kujenga Umoja  wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) na kuuvunja yanaendelea, huku kila upande ukiwa na imani ya kutumia nguvu zake zote.

Chadema, wakiwaandaa wanachama wao na watu wengine ambao ni wapenzi wa ukuta ili kuandamana bila silaha za moto lakini wakiwa na silaha yenye nguvu  kuliko zote ‘wananchi’ na Serikali ikiandaa askari na silaha za moto.

Tunawajibika kuwakumbusha ndugu zetu hawa kwamba wakifanyacho ni batili na historia itawahukumu. Ole wao hata tone moja la damu limwangike. Hakuna kujenga ukuta, wala kuvunja ukuta, maana Tanzania ni yetu sote!

Ni lazima tuliseme hili bila woga na bila kubembeleza urafiki au upendeleo wa aina yoyote ile. Ni wajibu wetu kulilinda na kulijenga taifa letu. Tukishindwa kulijenga kwa jasho letu, basi tulijenge kwa damu yetu; si kumwaga damu, bali ni damu kufanya kazi bila kuchoka na kujenga uhai wa taifa letu.

Hili jambo kwamba Tanzania ni yetu sote, ni lazima lieleweke kwa kila raia wa nchi hii. Hakuna aliye bora zaidi hapa. Wapinzani ni Watanzania na wana haki zote kama wananchi.

Hata kama hawajafanikiwa kutwaa dola, lakini ni Watanzania. Wana CCM, si Watanzania bora zaidi ya wengine. Sote ni Watanzania na sote tuna haki sawa mbele ya sheria na mbele ya haki zote za taifa letu.

Viongozi wa dini wana nafasi ya pekee kulieleza hili, maana kwa namna moja ama nyingine, wanatuhimiza kwamba sote ni watoto wa Mungu. Kwamba Mungu hana ubaguzi, anawaumba binadamu wote wakiwa sawa.

Na kwa vile sisi tuliamua kuwekeana mipaka na kutangaza nchi kinyume na matakwa ya muumba, ukweli unabaki pale kwa wale wote wanaojikuta kwenye kipande kimoja kinachojulikana kwamba ni nchi, basi raia wa nchi hiyo ni binadamu walio sawa mbele za Mungu na jamii inayowazunguka.

Viongozi wetu wa dini wakikaa kimya, wakiwaogopa viongozi wa Chadema, CCM na Serikali wakaacha Ukuta ukajengwa na kuvunjwa damu itakayomwagika hapa ni laana ambayo hawawezi kuikwepa. Hii itakuwa dhambi ambayo itawatafuna wao na vizazi vyao.

Viongozi wetu wa dini wana wajibu wa kutetea utamaduni wa kuifuata Katiba na kuilinda, pia viongozi wetu hao ni wajibu wao kuhakikisha demorasia inafuatwa na watu wote wanaishi kama watoto wa Mungu.

Tumekubali wenyewe na kuliweka ndani ya Katiba yetu kwamba nchi yetu inafuata siasa za vyama vyingi na kwamba ni nchi ya demokrasia. Maana yake iko wazi, kwamba mfumo wa siasa za vyama vingi una sheria zake na ni muhimu kuzingatiwa.

Demokrasia nayo ina utaratibu wake; kuruhusu uhuru wa kujieleza na kuvumilia maoni tofauti. Ni bahati mbaya kwamba Mungu katuumba na tofauti  ya maoni, tunafanana kwa mengine na kutofautiana kwa mengine, hivyo bila kuvumiliana na kuchukuliana ni vigumu kuishi kwenye dunia hii.

Haya mambo ambayo   ndugu zetu wa Chadema, CCM  na Serikali iliyo madarakani wanayandaa si mahitaji ya Watanzania. Huu si wakati wa jeshi letu la polisi kupambana na raia! Na wala kazi ya polisi si kupambana na rai, bali  ni kumlinda na mali zake.

Jeshi la polisi linaloendeshwa kwa kodi ya raia, maana wapinzani na wale wa chama tawala, wote wanatoa kodi, likageuka kuwapiga raia. Na wala Watanzania hawahitaji Ukuta kati yao na Serikiali yao iliyochaguliwa kwa mujibu wa Katiba.

Kumbukumbu,  zetu, zinaturudisha nyuma wakati Mwalimu, akilielezea Jeshi la Tanzania, kwamba ni Jeshi la Wananchi. Tofauti na majeshi mengine ambayo yanakuwa na jukumu la kuwalinda watawala, ndugu zao, mali zao na maslahi yao, Jeshi la Tanzania ni la kulinda usalama wa wananchi na nchi yao.

Kama hakuna tishio la amani ya nchi yetu. Tishio la kuhatarisha usalama wa taifa kutoka nje, kama vile tulivyovamiwa na nduli  Idi Amin wa Uganda, jeshi linabaki kambini, labda kama lina mazoezi ya kwenda kupamba na adui nje ya nchi.

Watanzania bado wana mahitaji mengi kama Taifa, kuwaingiza kwenye utamaduni wa kupigana kwa kukataa kukubaliana ni dhambi ya mauti. Watanzania wanahitaji maji, umeme, chakula, dawa, barabara, elimu na afya bora; kilio chao ni utawala bora na viongozi wao kuwajibika.

Wanataka waone maisha yanakuwa nafuu; bei ya sukari inatelemka, nauli inakuwa nafuu na vyakula vinapatikana kwa bei nzuri. Miaka 50 baada ya Uhuru Tanzania haina kitu chochote cha uhakika: Hatuna umeme, maji, chakula na elimu ya uhakika na kule vijijini hakuna nyumba, malazi na vyoo vya uhakika. Tumeshuhudia mara nyingi mashirika ya misaada kutoka nje ya nchi yakijenga vyoo vijijini.

Kasoro ya Serikali

Chadema ni chama cha upinzani. Ni wazi lengo lake ni kushika dola siku moja. Hivyo daima kitajitahidi kuangalia kasoro ambazo zinachelewesha maendeleo na kuwaeleza wananchi. Kasoro kubwa ya Serikali ya CCM ni kushindwa kulinda rasilimali za  taifa letu.

Imewaachia watu wakachota fedha za umma bila kuchukua hatua zozote zile na ugonjwa sugu wa kulindana.  Maandamano  ya Chadema na mikutano yao ni kulenga kuwaelewesha wananchi yale ambayo CCM imeshindwa kuyatekeleza.

Hivyo, itakuwa siyo busara CCM nayo kujibu hoja hizo kwa maandamano na mikutano. Au Serikali kutumia askari polisi wanaotunzwa na kodi za wananchi kuzima hoja za Chadema. Tulitegemea CCM ambacho ni chama kikongwe, kina wazee wenye busara na hekima kingejibu hoja za Chadema kwa matendo.

Kama Chadema wanasema Katiba imevunjwa, tunataka majibu kwa matendo kwamba Katiba haivunjwi. Na hili lionyeshwe kwa uhalisia hata na watu wanaojiandaa kwa maandamano na kujenga Ukuta, waone na kukubali.

Huu siyo wakati wa kujenga ukuta wala wa kuuvunja. Huu ni wakati wa kupamba na nafsi zetu ili kushinda ushabiki wa kisiasa unaoelekea kulitafuna taifa letu.

Chadema wakishirikiana na wale wanaowaunga mkono, wanajenga Ukuta kwa kusukumwa na ushabiki wa kisiasa. CCM, Serikali na Rais wetu, John Magufuli wanasukumwa na ushabiki wa kisiasa.

Bila kuwa juu ya ushabiki wa kisiasa ni vigumu kuleta mabadiliko na kusonga mbele. Tusijenge ukuta, wala tusivunje ukuta, bali tulijenge taifa letu.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, anapatikana kwa baruapepe: [email protected]  na [email protected] simu+255 754 6331 22.