Tusiwape mafisadi nafasi ya kupumua visiwani Zanzibar

Muktasari:

  • Taarifa moja ni ya kijana wa mjini Unguja, Rashid Abdulla Ali (31) aliyehukumiwa kifungo cha miezi mitatu kwa kuiba nazi 10.

Nilipokuwa ninafuatilia habari za matukio mbalimbali ya Zanzibar wiki iliyopita taarifa mbili zilinishangaza na kuniacha nikijiuliza maswali mengi bila ya kupata majawabu ya kuridhisha.

Taarifa moja ni ya kijana wa mjini Unguja, Rashid Abdulla Ali (31) aliyehukumiwa kifungo cha miezi mitatu kwa kuiba nazi 10.

Taarifa ya pili ni ya watumishi 28 wa Serikali kufukuzwa kazi kwa kuiba fedha za umma kwa kutumia hadaa, huku wengine wakikubaliwa kurejesha mamilioni ya shilingi walizojipatia kwa udanganyifu.

Kilichonishangaza ni kuona aliyeiba nazi amewajibishwa sawasawa kwa uhalifu alioutenda wa kumuibia mkulima nazi 10, lakini wafanyakazi hewa wale waliopokea mishahara wasiyostahiki wamefukuzwa kazi na wengine kuruhusiwa kurejesha fedha walizochota kutoka Hazina ya Zanzibar.

Sina lengo a kumtetea au kuonyesha imani kwa huyu mwizi njaa wa nazi kwa sababu wizi ni wizi tu, hata uwe wa kisheti au andazi.

Lakini, napata taabu kuelewa kwa nini hawa walioiba mamilioni ya shilingi wanapewa nafasi ya kurejesha fedha walizochota serikalini kwa njia zisio halali.

Kwa mtazamo wangu kama anayeiba fedha serikalini anapata afueni ya kuonewa huruma kwa uhalifu alioufanya, basi na huyu mwizi njaa wa nazi naye angepewa afueni ya kutakiwa amlipe mkulima fedha za nazi alizoiba au amrejeshee nazi zake 10.

Hizi habari za wafanyakazi hewa zimekuwa zikisikika visiwani mara kwa mara katika miaka michache iliyopita kila baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)au panapofanyika zoezi la kuhakiki watumishi wa Serikali.

Nimezungumzia mara nyingi hatari ya jamii kujenga matabaka na utamaduni wa baadhi yetu kuoneana huruma au kulindana kwa maovu na uhalifu tunaoutenda, kama wa kuiba fedha za umma.

Kwa kweli hawa watu wanaojifanya wajanja, bila ya shaka kwa kushirikiana na wengine, kujilipa mishahara na posho wasizostahiki au kufanya mbinu za kujipatia chochote katika manunuzi ya vifaa au utoaji wa zabuni kwa miradi mbalimbali hawastahiki kuonewa huruma.

Hawa si wezi bali ni mijizi iliyokubuhu na ndio wanaosababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kukwama kutokana na uroho wao wa kujitajirisha harakaharaka.

Mara nyingi panapofichuliwa kashfa hizi za ufisadi utaona ni watu wachache sana, haifikii hata robo ya hao wanaotuhumiwa wala wanaowajibishwa kisheria

Sijui kuna tatizo gani hapa, hata watu wanaofanya wizi huu wanavyoweza kuukwepa mkono mrefu wa sheria na ndio maana wizi wa aina hii unakuwa ukirejea kila baada ya muda mfupi kwa sababu wanaofanya hivyo huwa wanaamini watakwepa kwenda jela.

Safari hii tumeambiwa wafanyakazi 23 wamerejesha Sh82 milioni kati ya Sh141 milioni zilizopotea kwa njia mbalimbali za hadaa.

Wakati huohuo wapo ambao hawajapatikana na kwamba Jeshi la Polisi linafuatilia suala hili.

Hapa inafaa tukumbushane kwamba baadhi ya wizara na taasisi za Serikali zinaonekana kukubuhu kwa mwenendo huu mchafu wa wizi wa mchana.

Wizara ya Elimu

Kwa mfano, mwaka jana tulielezwa kugunduliwa wafanyakazi 422 wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali waliochukua likizo bila ya malipo, lakini waliendelea kupata mishahara bila kuwapo kazini.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri, aliyethibitisha kuwepo kadhia hiyo alieleza kwamba suala hili lilikuwa linafuatiliwa lakini mpaka leo hatujapata taarifa rasmi limefikia wapi.

Kulinyamazia suala hili au kulimaliza kwa njia za kimyakimya hakutoi sura nzuri ya utawala bora na kwa njia moja au nyengine inakuwa sawa na kuwaachia watumishi wengine wa Serikali wenye tabia kama hiyo kuendelea kwa imani kuwa hawataguswa na mtu. Vilevile naona ni vizuri nikumbushe kwamba miaka sita iliyopita kati ya wafanyakazi hewa karibu 4,000 waliogundulika katika uhakiki wa watumishi wa Serikali Visiwani, 1,400 walikuwa katika Wizara ya Elimu.

Kwa lugha nyepesi inaonekana wizi wa fedha za umma umekubuhu kupita kiasi katika wizara hii.

Wafanyakazi wengine hewa waligunduliwa katika idara mbalimbali za Serikali na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Tokea ilipotolewa ripoti ile ya uhakiki wa watumishi wa Serikali hakuna taarifa za uwazi zilizoelezea ni wafanyakazi wangapi waliohusika na wizi huu waliwajibishwa kisheria au kiasi gani cha fedha kilichokuwa kimechotwa kilirejeshwa Hazina.

Wakati umefika kwa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuamua kwamba muhali sasa basi na wizi na mafisadi washughulikiwe ipasavyo kama wanaoiba nazi na maandazi, bila ya kujali vyeo vyao serikalini au wazee wao ni nani. Huu mtindo wa kulindana kwa maelezo ya huyu mwenzetu au tunakumbuka mchango wake mwema au hisani ya wazee wake inatuponza na kurejesha nyuma maendeleo ya Zanzibar.

Kubana matumizi

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amesikika mara kwa mara katika siku za hivi karibuni akisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na hali ngumu ya maisha ni kubana matumizi.

Lakini, hata ukibana matumizi kwa kiasi gani kama bado kuna ufisadi au ubadhirifu wa fedha za umma ni sawa ni kujipunguzia mzigo wa kilo moja na kujitwisha mwingine uliokuwa umepakiwa katika lori.

Si vizuri na haitoi sifa ya haki kuona siku zote wanaoshtakiwa mahakamani na kufungwa jela ni wale wanaoitwa wizi njaa walioiba sinia ya maandazi, mkungu wa ndizi au nazi mbili tatu lakini wanaoiba mamilioni ya shilingi serikalini wanaachwa.

Ni vyema kwa ufisadi unaogunduliwa na CAG wa Zanzibar ukafuatiliwa mwanzo hadi mwisho na kila aliyeiba fedha za umma kuwajibishwa kisheria.

Vinginevyo tutakuwa siku zote tunapiga hatua moja mbele na kurudi nyuma kilomita mbili.

Watu wema hupaswa kulindana kwa mambo mema na mazuri na sio mabaya lakini, kila anayezifanyia ubadhirifu fedha za umma ni adui wa watu wa Zanzibar kwa vile hizo fedha wanazozikwapua na kuzitia mifukoni mwao zingesaidia kuwapatia mamia ya watu maji safi na salama, dawa katika hospitali zetu na madawati mamia ya watoto wetu wanaokaa kwenye sakafu shule na kuathiri afya zao.

Tusifike pahala tukaanza kudhani kuwa kuiba fedha za umma au mtumishi kuzichezea atakavyo ni haki ya kila mtumishi wa Serikali.

Tuwaandame na tuwasakame watu ambao wanataka kututia kwenye umaskini kwa kuwa si watu wanaofaa kuonewa imani, huruma wala muhali kwani hawa ni wauaji wasiokuwa na haya wala huruma.