Tuziache takwimu ziongee kwa maendeleo endelevu

Muktasari:

Takwimu zenye ubora na zilizotafsirika vyema zinatosha kutoa dira ya tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Kupiga hatua moja mbele, zinahitajika takwimu zinazojitosheleza ili wahusika wafanye maamuzi sahihi yatakayoisaidia jamii.

Takwimu ni hisabati ambazo ukikosea kanuni, njia utapata jawabu lisilosahihi. Maendeleo endelevu yanategemea matumizi ya takwimu sahihi. Ili kuwa na maendeleo endelevu ni lazima kutumia takwimu kupanga mipango ya maendeleo.

Takwimu zenye ubora na zilizotafsirika vyema zinatosha kutoa dira ya tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Kupiga hatua moja mbele, zinahitajika takwimu zinazojitosheleza ili wahusika wafanye maamuzi sahihi yatakayoisaidia jamii.

Moja ya sifa alizonazo Rais John Magufuli kabla na baada ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuongea kwa takwimu. Kumbukumbu zinaonyesha, kwenye wizara zote alikopitia alifanya hivyo.

Kuongea kwake takwimu kulimbeba na kumjengea sifa ya uwajibikaji. Ni ukweli usiopingika kuwa mtu yeyote anayeongea takwimu kuelezea sekta yake anajua alipo na anakotaka kuelekea. Ni rahisi kujitathmini na kuweka njia ya kufika unakotaka kwenda.

Ni gharama kuwa na takwimu bora. Inahitajika uwekezaji wa kutosha kwenye kukusanya, kuhifadhi, kuchambua, kuhakiki na kusambaza kwa wadau. Wahenga walisema; kama elimu ni ghali basi jaribu ujinga. Hakuna namna isipokuwa kuwekeza kwenye mfumo wa takwimu. Ili kujua kama kikundi, chama, au nchi inasonga mbele au kurudi nyuma ni lazima takwimu zitumike.

Hakuna mtu asiyetumia takwimu, mfano familia yenye watu wanne ikiwa inatumia kilogramu mbili za mchele, endapo watu wenye hadhi ile ile wataongezeka na kufikia sita maana yake ni kuwa mchele utahitajika kilogramu tatu na si mbili tena. Haya ni matumizi ya takwimu kwa maendeleo ya familia.

Endapo kila familia itakua na utamaduni wa kutunza na kutumia takwimu, hali hiyo itaenea kwa jamii nzima hivyo kuhamasisha mamlaka ziolizopo kuanza kutunza taarifa za kila jambo linalowagusa wananchi.

Ili Serikali ijue inahitaji kuandaa chanjo kiasi gani kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni lazima iwe na idadi ya watoto wote nchini wenye chini ya miaka mitano. Huwezi kujua halmashauri ya wilaya au mkoa inahitaji madawati kiasi gani bila kufahamu idadi ya wanafunzi.

Serikali ina mambo mengi yanayohitaji kufahamika kabla uamuzi wake haujafikiwa. Bunge haliwezi kupitisha bajeti kama hakuna taarifa sahihi za masuala mbalimbali ya uchumi, kijamii hata kisiasa.

Kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa jambo kunahusisha matumizi ya takwimu. Ili uweze kuelezea mafanikio, mfano mwaka 2015 mkulima alipata magunia tatu za mahindi kwenye shamba la eka moja ila baada ya kujifunza kanuni bora za kilimo mwaka 2016 akapata magunia saba kwenye shamba hilo. Haya ni mafanikio yaliyobainishwa kwa kutumia takwimu.

Moja ya faida kubwa za kutumia takwimu ni kupunguza maswali na kurahishisha uwelewa. Kwa kutumia mfano huo wa mkulima, bila kutumia takwimu anaweza kusema mwaka 2015 alilima hakuvuna sana, mwaka 2016 akalima tena na kupata mazao mengi.

Kwa msikilizaji au msomaji atabaki na maswali mengi, mwaka 2015 alivuna kiasi gani? Alilima kwenye eneo lenye ukubwa gani? Maswali ya aina hiyo yatajirudia tena kwa mwaka 2016. Kwa kutumia takwimu kama nilivyoonesha hapo awali, maswali yote yatafutika na kutoa picha pana ya hali ilivyokuwa mwaka 2015 na 2016 pia.

Si wakulima pekee, madereva barabbarani pamoja na mamlaka za usimamizi zinaweza kuonyesha vyanzo vya ajali mbalimbali kwa muda fulani kuhamasisha watu kubadili tabia.

Takwimu pia hutoa picha ya eneo ambalo halijafanya vizuri, mfano mwaka 2015 wanakijiji wa walijenga shule tatu za msingi kati 10 zinazohitajika. Mwaka 2016 wakajenga moja kati ya saba zinazohitajika.

Kwa takwimu utabaini kuwa wanakijiji hawakufanya vizuri kwenye ujenzi wa shule kwani walitekeleza ujenzi kwa asilimia mwaka 2015 na 14.29 mwaka 2016. Badala ya kupanda wameshuka.

Familia inayotumia takwimu inaweza kutambua kiasi gani cha mchele, unga wa mahindi, maharage, nyanya, vitunguu, mafuta na mengineyo kwa siku, wiki, mwezi au mwaka hivyo kupanga mipango bora ya matumizi ya fedha kwa muda husika.

Hali kadhalika kwa Taifa, linapotambua mgawanyo wa wananchi kwa umri, jinsi, makazi na shughuli za uzalishaji linaweza kupanga mipango bora ya maendeleo kwa wananchi wake. Bila kupanga kwa kutumia takwimu ni sawa na kutembea ukiwa umefumba macho.

Hata mgawanyo wa rasilimali mfano ruzuku ya wakulima au Sh50 milioni kila kijiji takwimu za wanufaikaji zinahitajika ili kupata uwiano sahihi.

Kwa maendeleo endelevu ni lazima taasisi zote zitumia takwimu katika shughuli za kawaida na maendeleo. Tuwekeze kwenye takwimu kwa maendeleo endelevu ya familia na Taifa kwa ujumla.

Hili si suala la kuahirisha, linapaswa kutekelezwa sasa kwa ajili ya kesho yetu. Mataifa yote yaliyoendelea yamefanya vyema kwa sababu huweza kujitathmini kwa kutumia taarifa zilizochujwa kwa matumizi mahsusi. Hizi ni takwimu ambazo Tanzania inazihitaji pia.

Mwandishi ni mtakwimu na Ofisa Mipango.