UCHAMBUZI: Kitakachomchelewesha JPM ni kubishana na wapinzani

Muktasari:

  • Ni bora Rais Magufuli aruhusu kukosolewa ili ajue njia ya kwenda

Kumekuwapo  maoni tofauti kuhusu utendaji wa vyama vya siasa katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano wa Rais John Magufuli.

Maoni hayo yanatokana na kauli za Rais  kukataza siasa hadi mwaka 2020, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiandaa operesheni yake waliyoiita Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

Tunajua  kauli ya Rais ya ‘Hapa Kazi Tu’ na amekuwa akiisisitiza mara kwa mara katika mikutano yake, huku akisisitiza kuwa hataki mtu amcheleweshe.

Wakati Chadema kikijipanga kufanya mikutano na maandamano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi mwaka huu, Rais Magufuli naye amesisitiza kuwa hataki kujaribiwa.

Baadhi ya watu wameishauri Chadema na vyama vingine vya upinzani kutofanya operesheni maana huu ni wakati wa kazi. Nimemsikia Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustine Mrema akiponda operesheni hizo za Chadema na kutaka watu wazipuuze.

Kibaya zaidi, hoja sasa imehamishwa kutoka kwenye haki ya vyama vya siasa kufanya shughuli zao na kuwa vinamchelewesha Rais Magufuli kutekeleza ahadi zake za uchaguzi. Huo ni uonevu kwa vyama vya upinzani.

Vyama vya siasa viko kwa mujibu wa sheria, kitendo cha kuvikandamiza kwa namna yoyote ile ni kupingana na sheria za nchi.

Nchi yetu inaendeshwa kwa Katiba na Sheria. Hata kama mfumo wa vyama vingi ulioridhiwa mwaka 1992 uliridhiwa kwa shingo upande, bado Katiba na sheria zimeeleza kabisa kuhusu wajibu na haki za vyama vya siasa.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 3 inasema;

(1) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

(2) Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo.

Sheria ya Vyama vya Siasa (sura ya  258) na kanuni (zilizotungwa chini ya fungu la 22(h) na Kanuni za Maadili za vyama vya siasa mwaka 2007 zimetafsiri chama cha siasa kuwa ni: “Chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kwa mujibu wa Sheria”

Sehemu ya pili ya kanuni hiyo inahusu chama cha siasa kuwa ni; 

4-(1) (a) kutoa elimu ya uraia na elimu ya uchaguzi kwa wananchi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi;

(b) Kutoa maoni ya kisiasa kadri itakavyoona inafaa ili kutekeleza sera zake, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar;

(c) Kujadili na kushindanisha Sera zake na zile za chama cha siasa kingine kwa lengo la kutaka kukubalika na wananchi;

(d) Kuwa na uhuru wa kutafuta wanachama na kama ni wakati wa kampeni basi kuwe na uhuru wa kutafuta kuungwa mkono na wapiga kura; na (e) Kila chama cha siasa kitakuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.

Sasa kwa sheria hizi, Chadema au chama kingine cha upinzani kina kosa gani kufanya mikutano au maandamano? Sheria hizi zimekufa? Bunge gani lilikaa na kufuta au kurekebisha sheria hizi?

Inasikitisha kuona Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anashindwa kutetea sheria hizi?

Jaji Mutungi ambaye ndiye mlezi wa vyama vya siasa nchini anashindwa kuvitetea kwa mujibu wa sheria. Badala yake anawakemea wanaotaka kufanya mikutano na maandamano.

Jaji Mutungi aliyebobea katika sheria, anashindwaje kumshauri Rais Magufuli kuhusu sheria hizi?

Halafu utasikia Msajili anataka kufuta vyama vya siasa vinavyoshindwa kujiendesha.

Vitajiendeshaje kama haviruhusiwi kutafuta wanachama kupitia mikutano? Vitakutanaje na wanachama wao ili kupanga mikakati yao bila mikutano? Vitashindanishaje sera zao kama sheria inavyoeleza bila kufanya mikutano?

Vitatoaje elimu ya uraia kama inavyoeleza sheria bila mikutano?

Sina lengo la kukitetea chama chochote, kwa sababu hata siku CCM ikishindwa uchaguzi, itazitumia sheria hizi hizi kutaka kufanya siasa.

Chama kushinda uchaguzi haina maana sasa kimekuwa juu ya sheria kukataza vyama vingine kufanya siasa.

Kazi ya vyama vya upinzani ni kuipinga Serikali iliyoko madarakani. Siyo kazi ya Chadema, CUF, NCCR Mageuzi au chama kingine cha upinzani kuiunga mkono CCM kwenye utendaji wa kila siku.

Vyama vya upinzani vikifikia hapo ndiyo vimekufa. Kinachofanywa na Mrema wa TLP ni usaliti kwa upinzani.

Kuna mambo ya msingi ambayo vyama vyote na wananchi wote wanatakiwa kuyaunga mkono bila kujali itikadi za siasa. Mambo haya ni pamoja na kulinda amani, umoja wa kitaifa, kufanya kazi kwa bidii. Hizo ndizo tunu za Taifa.

Ni bora Rais Magufuli aruhusu kukosolewa ili kupitia ukosoaji huo ajue njia ya kwenda. Kwa mfano, Rais amekiri mara kadhaa kuwa CCM aliyoirithi ilikuwa imeoza kwa ufisadi, jambo ambalo lilipigiwa kelele na wapinzani kwa muda mrefu.

Leo CCM imeichukua ajenda ya ufisadi ya wapinzani na kuifanya kuwa ajenda yake huku Rais Magufuli akiunda Mahakama ya Mafisadi.

Hiyo ndiyo kazi ya upinzani. Ni kukosoa na kupinga chama kilichoko madarakani ili ikiwezekana nacho kije kushika madaraka. Upinzani ni ushindani wa vyama vya siasa usiokwisha.

Siyo kazi yao kuipigia makofi CCM, siyo kazi yao kumsifu Mwenyekiti wa CCM wala kada yoyote. Hapo watakuwa wamesaliti upinzani.

Hata CCM wanayo misimamo yao wanayoisimamia kwa dhati, kwa nini wapinzani wasisimamie? Kwa hiyo huu ni mchezo tu unaosimamiwa na sheria, mtu hatakiwi kuziruka.

Rais Magufuli angeendelea tu kutekeleza ahadi zake, maana uwezo anao, sababu anayo na vitendea kazi vyote anavyo.

Kitakachomchelewesha kutekeleza ahadi zake ni kupigizana kelele na wapinzani ambao wana haki kisheria kumpinga.