UCHAMBUZI: Uwekezaji unahitajika kuondoa tofauti na maskini

Muktasari:

Hali hii ni miongoni mwa ukosefu mkubwa wa haki ulimwenguni. Hatima ya watoto wanaotoka katika familia maskini si lazima iishie hivi. Vifo vingi vinaweza kuepukwa kwa hatua zilizothibitika, zenye matokeo makubwa, na kwa kiasi, gharama nafuu.

Takwimu zinaonyesha kuwa watoto wanaokua katika umaskini, wana uwezekano wa kufariki kabla ya kufikisha miakmia tano mara mbili zaidi, wakilinganishwa na walio katika mazingira bora zaidi yao.

Hali hii ni miongoni mwa ukosefu mkubwa wa haki ulimwenguni. Hatima ya watoto wanaotoka katika familia maskini si lazima iishie hivi. Vifo vingi vinaweza kuepukwa kwa hatua zilizothibitika, zenye matokeo makubwa, na kwa kiasi, gharama nafuu.

Mama anapokuwa akijifungua nchini Tanzania, kuna uwezekano wa asilimia 36 kwamba hatahudumiwa na mkunga mwenye mafunzo. Uwezekano huo huongezeka hadi asilimia 58 endapo mama huyo anatoka katika familia maskini.

Kukosekana kwa mhudumu wakati wa kujifungua kunamuweka mtoto hatarini. Miongoni mwa sababu kubwa zinazohusishwa na vifo vya mama na mtoto ni pamoja huduma zisizojitosheleza kama vile uangalizi wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, pamoja na ukosefu wa chanjo.

Licha ya hatua kubwa katika miaka 10 iliyopita, watoto 67 katika kila uzazi hai 1,000 nchini Tanzania wanafariki dunia chini ya miaka mitano baada ya kuzaliwa. Upatikanaji wa huduma muhimu kwa mama na watoto maskini umeendelea kuwa changamoto.

Ripoti mpya ya Unicef; Kupunguza Tofauti: Nguvu ya Kuwekeza kwa Watoto Maskini, inaonyesha usawa utapunguza gharama na kuokoa maisha. Takwimu zilizochambuliwa kutoka nchi 51 ikiwamo Tanzania, zinaonyesha uwekezaji wa kuimarisha hatua muhimu za ukuaji wa watoto maskini unahitajika zaidi kuliko kwa wasio maskini.

Idadi ya vifo vinavyoepukwa kwa kila Dola milioni moja za Marekani zilizotumiwa, iko juu mara 1.8 zaidi miongoni mwa maskini kuliko wasio maskini.

Utafiti ulichunguza matunzo wakati wa ujauzito, uwapo wa mkunga wakati wa kujifungua, unyonyeshaji maziwa ya mama, chanjo kamili, matumizi ya vyandarua vyenye dawa na kutoa matibabu kwa mtoto mwenye ugonjwa wa kuhara, homa au kichomi na kuunganisha utoaji wa huduma hizo na vifo vya watoto.

Utafiti umebaini kuwa, katika nchi zilizoshiriki, tija kwenye afya na lishe imeimarika zaidi miongoni mwa makundi ya watu maskini katika miaka ya hivi karibuni.

Imeonekana vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua karibu mara tatu, haraka zaidi katika jamii maskini kati ya mwaka 2003 na 2016 ikiwa ni matokeo ya kuongezeka kwa uchukuaji hatua zenye ufanisi wa juu.

Kingine kilichobainika ni kuwa, kupanua uchukuaji hatua zenye kuleta matokeo ya juu dhidi ya umaskini kuna faida katika thamani ya fedha.

Matokeo hayo yana maana kubwa kwa Serikali katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambayo yanasisitiza kupunguzwa kwa utofauti wa kipato pamoja na kuzuia vifo vya vya uzazi vinavyozuilika ifikapo mwaka 2030.

Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo hivi. Utafiti wa Demografia na Afya Tanzania unaonyesha kuwa idadi ya watoto wanaofariki chini ya miaka mitano imeshuka kutoka 147 kwa uzazi hai 1,000 mwaka 1999 hadi 67 mwaka 2015-16.

Utafiti pia unaonyesha tofauti kubwa. Nyanda ya Kusini Magharibi ilikuwa na vifo 95 wakati wastani wa vijijini ulikuwa vifo 86. Ni katika maeneo haya ambako watoto hawa na familia zao hawapati huduma bora za afya kwa usawa, jambo tunalolikazia.

Tanzania inakaribia kuingia katika uchumi wa kipato cha kati huku sehemu kubwa ya nguvu kazi ya baadaye yaani watoto wa leo, inaendelea kuathiriwa na vikwazo lukuki vinavyowarudisha nyuma.

Katika miaka 10 mpaka 15 ijayo, kundi kubwa la vijana litakuwa ndilo lenye wazalishaji uchumi. Kuwabaini watoto walio katika mazingira magumu, kufanya uwekezaji unaohitajika ili nao pia wapate mwanzo mzuri wa maisha ni pendekezo muhimu.

Watoto hawa wanaweza kukua wakiwa wenye afya njema, ujuzi, na kuwa nguvukazi imara inayohitajika kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Nimekutana na watoto walio katika mazingira magumu huko Nyanda za Juu Kusini, mikoa ya Magharibi na Zanzibar, nina matumaini tutaongeza kasi ya kuwafikia watoto hawa. Mtoto aliyezaliwa katika familia maskini si lazima aanze maisha huku hatima yake ikiwa hatarini.

Kupunguza tofauti, ni utafiti unaoziasa Serikali kuwekeza ili kuwafikia wasiofikika, hasa watoto na wanawake kutoka kaya maskini.

Kamwe rasilimali hazitoshi kushughulikia mahitaji yote kwa wakati mmoja lakini Serikali inapaswa ‘kutomwacha yeyote nyuma.’

Maniza Zaman ni Mwakilishi wa Unicef nchini.