UNWTO yazindua mwaka wa utalii endelevu na maendeleo

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa UNTWO, Dk Taleb Rifai alisema zipo sababu nyingi za kuutambua mwaka 2017 kuwa mwaka wa utalii endelevu na maendeleo kutokana na mchango wa tamaduni tofauti ambazo zimeimarisha amani na kufanikisha watu kutembelea maeneo tofauti bila tatizo lolote.

Dar es Salaam. Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) limezindua mwaka 2017 kuwa wa utalii endelevu na maendeleo na kutilia mkazo maeneo matatu ya kipaumbele.

Katibu Mkuu wa UNTWO, Dk Taleb Rifai alisema zipo sababu nyingi za kuutambua mwaka 2017 kuwa mwaka wa utalii endelevu na maendeleo kutokana na mchango wa tamaduni tofauti ambazo zimeimarisha amani na kufanikisha watu kutembelea maeneo tofauti bila tatizo lolote.

“Kulikuwa na watalii zaidi ya bilioni 1.2 waliotembelea mataifa tofauti mwaka jana huku watu bilioni sita wakifanya utalii wa ndani duniani kote. Sambamba na kukua kwa sekta hii, tunalo jukumu la kuifanya iwe endelevu, yenye usawa na jumuishi,” alisema Dk Rifai.

Maeneo yaliyosisitizwa kutokana na fursa zake ni utalii wa kiutamaduni, kilimo na mazingira na nchi wanachama kutakiwa kuyapa kipaumbele ili kuongeza tija kwa wananchi na Pato la Taifa.

Mpango huo umezinduliwa jijini Madrid na Mfalme Felipe VI wa Hispania kwenye mkutano uliohudhuriwa na zaidi ya mawaziri 40 na maofisa waandamizi 57 wa utalii kutoka nchi mbalimbali duniani ulibainisha namna sekta hiyo inavyoweza kuzinufaisha jamii za mataifa wanachama hasa wananchi.

“Kuichagua Hispania kuzindua mpangio huu ni ishara ya kutambua jitihada zilizopo za kuimarisha utalii wa utamaduni, kilimo na mazingira,” alisema mfalme huyo.

Kabla ya kuzinduliwa, mpango wa utalii endelevu ulitangazwa Desemba 2015 na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Mataifa (UN) ukiwa sehemu ya Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayotekelezwa tangu mwaka 2015 mpaka 2030.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Generali Gaudence Milanzi alisema ingawa Tanzania haikuwakilishwa kwenye mkutano huo, inayo maadhimio ambayo itayatekeleza.

Alisema juhudi zinazofanywa na Serikali zinalenga kuhakikisha utalii unafanywa kwenye kanda zote pamoja na kuongeza vivutio. “Licha ya utalii wa wanyama tunataka kuimarisha ule wa utamaduni na lugha hasa Kiswahili,” alisema generali Milanzi.

Alibainisha kwamba maonyesho yaliyofanyika wilayani Nyasa na uwapo wa Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam ni mwanzo kuelekea utangazaji wa utalii wa utamaduni wa makabila mbalimbali nchini huku fursa zilizopo kwenye fukwe zikiendelea kufanyiwa kazi pia.

“Ndege zinazoendelea kununuliwa na Serikali zinalenga kufika maeneo yote ambayo yalikuwa hayafikiki. Licha ya Kanda ya Kaskazini, tunaka kote kwenye vivutio wageni wafike na kufurahia utalii wa Tanzania,” alisema.