Uamuzi mgumu wawakabili wakimbizi wa Kiafrika Israeli

Saturday January 20 2018

Wakimbizi walioko nchini Israel wakionyesha

Wakimbizi walioko nchini Israel wakionyesha bango lenye msomamo wao wa kupinga kutimuliwa katika nchi hiyo kwenda sehemu nyingine. Picha ya Mtandao 

By Othman Miraji

Karibu wahamiaji 40,000 wa Kiafrika walioko Israeli wako katika hatari ya kufukuzwa nchini humo au kufungwa jela. Siku kumi zilizopita Baraza la Mawaziri la nchi hiyo liliamua kwamba wale waliojipenyeza kuingia Israeli kwa njia isiyokuwa ya halali watatakiwa kuchagua ama ‘wanaweza kushirikiana na Serikali ili warejee makwao kwa hiari, la sivyo sheria ifuate mkondo wake’ kwa maana wafungwe jela kwa muda usiojulikana.

Tangu Februari Mosi, wahamiaji hao itabidi waarifiwe kwamba wanaweza kuondoka nchini ndani ya siku 60, ama la kuna hatari ya wao kutupwa magerezani. Inasemekana kwamba kati ya nchi ambazo huenda zikawapokea wakimbizi hao watakaofukuzwa ni Rwanda na Uganda.

Jumuiya za kupigania haki za binadamu zinailaumu Israeli kwamba imewaweka wakimbizi hao katika hali ya kutojua hatima yao.

“Israeli kwa makusudi inawazuia Waafrika kuwasilisha maombi yao ya kutaka kupewa hifadhi ya ukimbizi na inawafukuza kutoka katika nchi hiyo kwa kisingizio kwamba hawajawasilisha serikalini maombi yao,”alisema Dror Sadot, msemaji wa Jumuiya ya Kuwatetea Wahamiaji iliyoko Tel Aviv nchini humo, kuhusu uamuzi huo wa Baraza la Mawaziri la Israeli.

Pia, Jumuiya yenye kuwatetea watu wanaotishiwa kuangamizwa yenye makao yake mjini Göttingen, Ujerumani, imeulaumu mpango huo wa Serikali ya Israeli kuwa ni wa kuwadharau binadamu na unakwenda kinyume na sheria za kimataifa. Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi (UNHCR) limesema lina wasiwasi mkubwa juu ya mpango huo na hasa juu ya usalama wa watu watakaofukuzwa.

Serikali ya Israeli itakuwa tayari hadi Machi mwaka huu kumpa kila “Mhamiaji Haramu” dola za Kimarekani 3,500 na tiketi ya ndege ili arejee kwao au kwenda katika nchi nyingine ya tatu itakayompokea.

Kwa mujibu wa duru za Serikali ni kwamba fedha hizo zitapungua kila pale mtu atakapochelewa kuichukua ofa hiyo. Na pindi mtu atakataa kuichukua basi atatiwa jela.

Karibu wakimbizi wote wa Kiafrika wanaofaulu kupenya na kuingia Israeli wanatumia njia za nchi kavu, kupitia eneo la Sinai la Misri. Wengi wao wanakumbana na mateso ya kikatili njiani kutoka kwa mabedui wa Sinai.

Hulazimishwa kuwapigia simu jamaa zao waombe watumiwe maelfu ya dola ili walipie ukombozi wao kutoka kwa watu waliowashikilia.

Wale wasiokuwa na familia nyumbani za kuwatumia fedha basi huwa hatarini, mara nyingine huuawa na viungo vyao vya mwili kuibiwa. Wanapokuwa nchini Israeli, wakimbizi hao hawaruhusiwi kufanya kazi, na wanapofanya kazi bila ya kupata kibali, mara nyingi polisi hufumba macho. Lengo la wengi wa wakimbizi ni kubakia Israeli.

Wakimbizi 900 wa Kiafrika, wanaume, wanawake na watoto, wameichukua ofa hiyo ya kibiashara iliyotolewa na Serikali ya Israeli. Lakini, kuna hatari mbele. Wako Wasudani walioikubali, lakini walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Khartoum walikamatwa na polisi. Walihojiwa na kuulizwa kwa nini walienda Israeli? Pia, walipigwa.

Tangu mwaka 2005 wakimbizi wa Kiafrika wamekuwa wakiingia Israeli, mwanzoni katika makundi ya wachache, lakini baadaye walifikia hadi alfu moja kila mwezi. Wengi walitokea Eritrea (30, 549) na pia Sudan (8,232).

Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji ya Israeli pia kuna watalii 91,000 katika nchi hiyo wasiokuwa na vibali vya kukaa nchini (Viza). Israeli ina wakazi milioni 8.5 japokuwa ni nchi ndogo, lakini inamudu kubeba mzigo wa wakimbizi hao, na hata zaidi ya hao. Katika miaka ya mwanzo polisi waliwaweka na kuwalinda wakimbizi katika aina ya makundi.

Hiyo ina maana kwamba hawajatambuliwa rasmi kama wakimbizi, lakini walikuwa hawana haja ya kuogopa kufukuzwa kutoka nchi hiyo. Ilimaanisha pia kwamba hakuna yeyote kati ya wageni hao aliyeomba rasmi hifadhi ya ukimbizi.

Israeli ilijenga uzio katika mpaka wake na eneo la Sinai la Misri kujilinda na mmiminiko wa wakimbizi na baadaye iliwapa adhabu watu waliodiriki kujipenyeza mpakani. Tangu mwanzo wa mwaka 2012 watu hao wametajwa rasmi kwamba ni wahamiaji haramu.

Ni sasa ambapo yanamiminika maombi ya watu kutaka kukubaliwa kutambuliwa rasmi kama wakimbizi, lakini bila ya mafanikio makubwa. Ni maombi machache sana yaliyokubaliwa.

Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Israeli huko Jerusalem ni kwamba Serikali ya nchi hiyo inaweza kuwafukuza wakimbizi kutoka nchi hiyo, lakini ikiwa kuna nchi nyingine itakayokuwa tayari kuwachukua. Novemba mwaka jana Waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda, Louise Mishikiwabo, alitangaza kwamba nchi yake iko tayari kuwachukua watu 10,000 wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi. Shuruti iliyotolewa ni kwamba waende kwa hiari yao.

Uamuzi wa karibuni wa Baraza la Mawaziri la Israeli unaashiria kwamba Rwanda huenda imefikia makubaliano na Israeli juu ya jambo hilo.

Kwa mujibu wa ripoti za Serikali ya Israeli ni kwamba kuna wakimbizi 1,420 ambao tayari wamezuiliwa makambini na tangu kujengwa uzuio katika mpaka na Misri ambako wakimbizi 60,000 wameingia Israeli wakitokea Afrika.

Waziri Mkuu Netanyahu alisema wameshawafukuza wakimbizi 20,000, na sasa kuna kazi ya kuwafukuza waliobaki. Alisema siasa ya nchi yake kuhusu kutoa hifadhi ya ukimbizi inatokana na mfumo tete wa kijamii katika nchi hiyo. Waisraeli wengi katika mitaa ya kimaskini ya Tel Aviv wanahisi si tena salama kutokana na kuweko idadi kubwa ya wahamiaji wa Kiafrika.

Kutokana na tafsiri rasmi, Israeli ni dola ya Kiyahudi, lakini kuna Waislamu wengi katika nchi hiyo kama jamii ya wachache. Na kutokana na mpango wa kuwafukuza wahamiaji haramu, Israeli itaifunga Kambi ya Holot ilioko katika Jangwa la Negev na ambayo imesababisha mabishano makubwa. Awali, Bunge la Israeli, Knesset, huko Jerusalem liliipa uwezo Idara ya Uhamiaji kuwakamata watu wanaovuka mpaka kinyume na sheria na kuwashikilia kwa miaka mitatu katika Jela ya Saharonin iliyowekwa hasa kuwapokea wakimbizi haramu.

Katika jela hiyo ya Saharonin mtu huwa mfungwa asiyekuwa na haki badala ya kuwa mkimbizi anayelindwa na mikataba ya kimataifa. Wafungwa 10 huwekwa katika chumba kimoja na mji ulioko karibu na hapo ni masafa ya saa moja kwa basi. Huko ni baridi sana wakati wa msimu wa baridi na katika kiangazi joto ni kali mno. Kila mtu hupewa Euro 15 kila wiki ambazo hazitoshi hata kwa nauli ya basi kwenda Tel Aviv. Waziri wa utamaduni wa Israeli, Miri Regev, aliwahi kusema kwamba wakimbizi wa kutokea Afrika ni jipu la saratani katika mwili wa taifa la Kiyahudi.

Pia, Serikali ya Israeli haiweki siri juu ya nia yake ya kumfukuza kutoka nchi hiyo hadi mkimbizi wa mwisho. Cha kusikitisha ni kwamba wakati dola ya Israeli iko tayari kumpokea Myahudi yeyote wa kutoka popote duniani na kumpa papo hapo uraia wa nchi hiyo, lakini, haiko tayari kumstahamilia kumpa hifadhi ya ukimbizi Mwafrika aliyekimbia vita na mateso kutoka kwao. Hapo ndipo inapopatikana shida kwa Israeli kujikwamua na madai ya watu wanaosema kwamba dola hiyo ni ya kibaguzi.

Advertisement