Uchaguzi baada ya miaka saba, hoja hii haina tija

Muktasari:

  • Kwa hiyo, unaposikia Juma Nkamia, mbunge wa Chemba anapendekeza kuongeza muda wa kipindi cha utawala kuwa miaka saba kati ya uchaguzi na mwingine, yafaa tuangalie muktadha wake.

Mara nyingi mabadiliko ya sheria hupendekezwa ili kushughulikia changamoto fulani iliyotokea kutokana na sheria au utaratibu uliokuwapo awali.

Kwa hiyo, unaposikia Juma Nkamia, mbunge wa Chemba anapendekeza kuongeza muda wa kipindi cha utawala kuwa miaka saba kati ya uchaguzi na mwingine, yafaa tuangalie muktadha wake.

Muktadha wenyewe ni hali ya kisiasa ya Tanzania, ambapo inaaminika na wapenzi wa CCM na wafuasi kindakindaki wa Rais John Magufuli kuwa kiongozi aliyepatikana safari hii ni bora, hajapata kutokea.

Wanadai ni Rais wa kihistoria na amekuwa akichukua jitihada nyingi za kuikomboa nchi na kada ya wanyonge.

Kwa sababu hiyo, wapenzi hawa wa Rais wanaounga mkono sera za Serikali wanaamini, kuwa rais huyu ni wa kipekee na hivyo, yafaa apewe muda zaidi ili aendelee kuinyoosha nchi na wananchi, hususan wale wanaojulikana kama ‘wapiga dili’.

Kiongozi mkuu wa shule hii ya fikra ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye mara nyingi alishatangaza anavyomkubali Rais Magufuli.

Katika moja ya kauli zake alisema, ingekuwa mapenzi yake, basi angetamani Rais Magufuli atawale milele, kauli ambayo ilionekana kuungwa mkono na wapenzi wengi wa siasa za ‘umagufuli’ na kuwaudhi wengine, hasa wapinzani.

Nikisema siasa za umagufuli, narejea mtazamo mpya wa kiuongozi ambao unajitofautisha na wa awamu zilizopita katika nyanja nyingi, kama msisitizo katika ulinzi wa rasilimali za nchi, vita ya ufisadi na udhibiti mkubwa katika uhuru wa kisiasa na kujieleza.

Baada ya kauli ya Mwinyi ya kutangaza mahaba yake kwa uongozi wa Rais Magufuli, kisha ikafuata kampeni ya ‘Magufuli Baki’, ambayo walioanzisha baadaye waliamua kuichengesha kwa kudai lengo ni kumuomba abaki katika msimamo wake wa kutetea maskini, wanyonge na kupigania rasilimali za taifa.

Ni kwa sababu kumekuwa na fikra hizo, ndiyo maana tunapokutana na muswada wa Nkamia, wengi tunaelewa kuwa hizi ni jitihada za kutekeleza fikra zile za Mwinyi na vuguvugu la harakati za Magufuli baki.

Nionavyo, huenda walio nyuma ya kampeni hizi waliona kuwa kuondoa kabisa ukomo wa kutawala, yaani vipindi viwili vya miaka mitano, kungekutana na upinzani mkali na hata mrejesho mbaya kutoka jumuiya za kimataifa.

Hivyo imeonekana hii ni njia nzuri zaidi ya kumuongezea Rais Magufuli muda wa utawala, walau kwa kuanzia. Wadadisi wengi wa kisiasa pia wanaamini hivyo.

Sababu zilizotolewa na Nkamia si hizi, yaani, kumpa muda zaidi wa kutawala Rais Magufuli. Sababu rasmi ni kwamba kufanya uchaguzi mara kwa mara ni ghali, lakini pia Nkamia amependa tuige Rwanda akiamini kwamba ni nchi yenye mafanikio lakini ikiwa na mfumo huo.

Hata hivyo, Nkamia anasahau kwamba tayari Rwanda imeshapitisha mabadiliko ya Katiba yatakayoanza kutumika 2024, kuondoa kipindi cha miaka saba kurudi mitano.

Demokrasia ni ghali

Kwa hoja yake ya gharama, bila shaka Nkamia amesahau kuwa demokrasia ni ghali na itabaki kuwa ghali. Tunatakiwa tusiangalie upande wa gharama tu, bali pia faida kubwa ipatikanayo kutokana na demokrasia.

Demokrasia ndiyo mzizi wa amani na haki katika nchi zenye watu wa matabaka tofauti kama yetu. Nasema hivyo kwa sababu katika mfumo huu, kila mtu ana fursa ya kugombea nafasi ya uongozi na pia ya kuchagua kiongozi.

Zipo nchi ambazo zimevurugika kwa sababu tu ya kukosa demokrasia, pia zipo nyingine ambazo hazina demokrasia lakini zina kinachoitwa amani, basi mara nyingi amani iliyopo ni feki. Ni amani ya kulazimisha ambayo msingi wake ni nguvu za dola.

Kwa hiyo, demokrasia yaweza kuwa ghali, lakini inalipa. Na kama hatupendi kuigharamia, basi labda muswada wa Nkamia ungependeza tuondoe kabisa uchaguzi, tuje na mfumo mwingine.

Pia, sina hakika kama tunaweza kuitaja Rwanda kama nchi yenye mafanikio, labda tukijua mafanikio yanayozungumzwa ni katika nyanja zipi. Lakini hata ingekuwa imefanikiwa kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa, sina hakika kama kuwa na kipindi cha utawala wa miaka saba ni moja ya sababu.

Nkamia ametaka tuige mfano wa Rwanda lakini hajazingatia ukweli kwamba yanayofanyika leo Rwanda ni matokeo ya historia yake. Huenda Rwanda ingepitia historia ya kawaida, bila uzoefu wa mauaji ya kimbali na mapinduzi ya kijeshi, hali ingekuwa tofauti.

Ni ajabu kwamba katika nchi zote ambazo Nkamia alitamani tuziige, amechagua Rwanda. Vyovyote iwavyo, ukweli ni kwamba miaka mitano ndiyo kiwango cha muda cha kukaa madarakani kinachofuatwa na nchi nyingi, labda kama nilivyotangulia kutaja kwamba kuna ajenda nyingine ya kuitafuta miaka saba.

Kuongezea muda ni woga

Ujanjaujanja wa kutaka kuongeza kipindi cha utawala kwa sababu unaamini ni kiongozi bora sana ni matokeo ya woga. Kufanya hivyo ni kufanya makosa ya kujiaminisha kuwa katika Taifa la watu zaidi ya milioni 50, hakuna ambaye anaweza kuongoza kama aliyepo au hata zaidi. Kwa utafiti gani tulioufanya unaotufanya tuamini hivyo?

Kwani huyu aliyepo, ametokea wapi? Nani alijua kuwa angefanya anayoyafanya sasa? Basi kama alitokea Magufuli, bila kutarajiwa, kwa nini tusiamini kuwa wapo wengi ambao wanaweza wakapokea kijiti kutoka kwake na kufanya bora zaidi.

Kubadili Katiba kwa sababu ya mtu, ni jambo lenye ukakasi mwingi na binafsi natafsiri kuwa ni kuidhalilisha Katiba na kufifisha dhana ya utawala wa sheria. Makali ya utawala wa sheria yanaonekana katika maeneo haya, ambapo mnatokea kumpenda mno mtu lakini sheria inasema hamuwezi kuwa naye tena.

Ni vema Watanzania tujifunze kuwa njia pekee ya kupata viongozi bora si kung’ang’ania huyu mmoja ambaye baadhi wanadhani ndiye bora na kumlazimisha abaki nanyi milele.

Jambo wanalotakiwa kuelewa watu wa namna hiyo ni kuwa kwa kanuni za maumbile kutawala milele hakuwezekani, kwani watu hufa na kuzeeka. Njia bora ni kuandaa viongozi wapya.

Kuna namna mbili ya kuandaa viongozi. Kwanza, kwa mkakati mpana wa kitaifa kupitia mifumo yetu ya elimu na mafunzo, ambayo yatajenga uwezo na uzalendo. Namna ya pili, ni jitihada za kiongozi aliyepo za kuwalea wasaidizi wake na kuwasogeza katika majukwaa ambayo vipawa vyao vitaonekana.

Na sijui kwa nini mbinu hizi za kiujanja ujanja zinaanza sasa hata baada ya mkuu mwenyewe, Rais John Magufuli kutangaza kuwa hana hamu ya kutawala zaidi ya muda wake, na kimsingi angefurahi kama angepumzika baada ya kipindi kimoja!