Ufaulu wenye shaka shule za Serikali

Muktasari:

Wanasema ufaulu huo wa ‘miujiza’ umekuja huku kukiwa hakuna juhudi thabiti za kukuza taaluma katika shule nyingi za Serikali ambazo pamoja na mambo mengine, zinakabiliwa na changamoto tete ya uhaba wa walimu.

Baadhi ya wadau wa elimu nchini wamestushwa na matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibu na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yakitaja shule tano za Serikali kuwa katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.

Wanasema ufaulu huo wa ‘miujiza’ umekuja huku kukiwa hakuna juhudi thabiti za kukuza taaluma katika shule nyingi za Serikali ambazo pamoja na mambo mengine, zinakabiliwa na changamoto tete ya uhaba wa walimu.

Wanatilia shaka matokeo hayo wakisema huenda matokeo yaliyotajwa hayaakisi ukweli wa taaluma katika shule hizo.

Akitangaza matokeo hayo hivi karibuni, Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Charles Msonde, alizitaja shule tano za kongwe za Serikali katika orodha ya shule 10 bora, ikiwamo moja Sekondari ya Wavulana ya Tabora ambayo uongozi wa shule na wanafunzi wanakiri ina uhaba mkubwa wa walimu hasa wa masomo ya sayansi.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema) ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Elimu Suzan Lyimo anasema ni jambo la ajabu kwa shule kuwa na matokeo mazuri wakati bado zina mahitaji ya muda mrefu anayosema hayajatekelezwa.

“Inawezekana ni muujiza au kuna sura ya siasa katika matokeo hayo. Mimi sioni sababu hasa ya shule za Serikali kupanda kiasi hicho, kwa sababu kama ni motisha kwa walimu bado hawajapata, vifaa vya kufundishia bado ni tatizo, yote hayajafanyika, lakini shule za Serikali zimepanda,” anasema na kuongeza:

“Bado mimi kama mwalimu kitaaluma ninafanya utafiti wangu. Lakini katika tafiti zangu za nyuma nilibaini kuwapo kwa mchezo wa kisiasa kwani miaka miwili kabla ya uchaguzi, matokeo huwa yanakuwa mazuri kwa shule za Serikali ili kuibeba Serikali.”

Aishukia Necta

Lyimo pia ametilia shaka utendaji wa Necta, akisema limekuwa likiendeshwa kwa usiri mkubwa.

“Baraza linaendeshwa kwa siri kubwa, wala huwezi kujua wanasahihishia mitihani wapi. lakini kama tungefuatilia usahihishaji na kujua jinsi wanavyofanya tungejua mengi. Inawezekana siasa zinatumika kuibeba Serikali,” anasema Lyimo na kuongeza:

“Naendelea na utafiti kujua, kwa nini wakati bado Serikali haijaboresha shule zake, lakini ghafla zinafanya vizuri, kwa nini Shule ya Sekondari ya Azania iliyokuwa ikifanya vizuri ianguke vile? Necta wanasahihishaje mitihani?”

Mdau wa elimu, Heri Bakari ana shaka na ufaulu akihoji kama wamefaulu au wamefaulishwa? Wasiwasi wake unatokana na taarifa aliyosoma kwenye gazeti moja la kila siku (siyo hili) kuwa shule kama Tabora Boys haikuwa na walimu wa sayansi, lakini nayo imo kwenye orodha ya shule bora.

“ Walimu ni nguzo kubwa katika ufaulu wa shule yoyote, nenda katika shule binafsi uone mchango wa walimu katika maendeleo ya taaluma. Sikatai kuwapo kwa wanafunzi wazuri, lakini napata wasiwasi mkubwa shule isiyo na walimu kuwa katika kumi bora. Ingekuwa ya 30, au 40, tusingesema kitu,” anaeleza.

Uhaba wa walimu Tabora Boys

Moja ya shule zilizofanya vizuri katika matokeo hayo ni Sekondari ya Wavulana ya Tabora, ambayo pamoja na mafanikio hayo imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu wa sayansi.

Hassan Bakari ni mmoja wa wahitimu wa shule hiyo ambaye pia mshindi wa kwanza kati ya wanafunzi 10 waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi.

Baada ya matokeo kutangazwa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa shule hiyo haina walimu wa sayansi kwa miaka mitatu sasa.

Kwake ufaulu huo ni juhudi binafsi alizotokanazo tangu alipokuwa Shule ya Sekondari ya Mirerani Benjamin Mkapa ya Arusha.

Ni juhudi binafsi

Wakati matokeo hayo mazuri kwa shule hizo zikiwapa sifa viongozi wa shule na hata Serikali kwa jumla, Mhadhiri wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Dk Luka Mkonongwa anasema, matokeo hayo ni matunda ya juhudi binafsi za wazazi na wanafunzi.

“Shule nyingi za Serikali hazina walimu wa kutosha, kwa hiyo wanafunzi wanatafuta masomo ya ziada. Hizo ni juhudi binafsi za wazazi, lakini shule ndiyo zinazopata sifa,’’ anasema.