Ufisadi ulimpaisha, kumng’oa Zuma

Muktasari:

Uwekezaji katika nafasi ya naibu rais, ulijengwa na ukweli kuwa, Mandela alishaweka wazi kwamba alitaka kujenga misingi ya utu, ushirikiano wa kijamii kama taifa, kisha angeacha watu wenye nguvu zaidi kiakili na kimwili waendeleze gurudumu.

Mwaka 1994 wakati wa Uchaguzi Mkuu ANC, ilikuwa ikifahamika kwamba Nelson Mandela angeendelea na urais wa chama ambao alianza kuushika mwaka 1991, alipompokea shujaa wa wakati wote wa Afrika Kusini, Oliver Tambo. Kutokana na ufahamu huo, mnyukano ulikuwa ni kwenye nafasi ya naibu rais, kwa sababu aliyekuwa akiishikilia, Walter Sisulu alikuwa ametangaza kukaa pembeni kwa sababu ya umri.

Uwekezaji katika nafasi ya naibu rais, ulijengwa na ukweli kuwa, Mandela alishaweka wazi kwamba alitaka kujenga misingi ya utu, ushirikiano wa kijamii kama taifa, kisha angeacha watu wenye nguvu zaidi kiakili na kimwili waendeleze gurudumu.

Hivyo, uchaguzi wa ANC 1994, ulilenga kushika madaraka ya nchi kwa makomredi – Thabo Mbeki, jacob Zuma, Cyril Ramaphosa, Chris Hani na wengine.

Ramaphosa akiwa kijana zaidi wakati huo, alikuwa akistawi vizuri. Hani alikuwa mjamaa mwenye ushawishi mkubwa na aliyefikiriwa kuwa naibu rais wa ANC chini ya Mandela, mbele ya Mbeki na Zuma.

Mwaka 1993 baada ya kuwa dhahiri kwamba Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa kidemokrasia Afrika Kusini ungefanyika mwaka 1994 na ANC kuwa na uhakika wa kushinda, ndipo mnyukano ulianza.

Zuma na Mbeki waliunda timu moja kuwashughulikia wale wote waliokuwa wakifikiriwa. Kishindo cha Mbeki na Zuma hakikuwaacha salama Ramaphosa, Hani, Essop Pahad na mdogo wake, Aziz Pahad na wengine wengi.

Aprili 10, 1993, Hani alipouawa kwa risasi na Mpoland aliyekuwa na uraia wa Afrika Kusini, Janusz Walus, ndani ya ANC kulikuwa na hali ya kunyoosheana vidole kwamba pengine mnyukano wa uongozi ndio ulikuwa sababu, hasa nafasi ya naibu rais wa chama.

Hii ni kwa sababu Afrika Kusini ni nchi ambayo Serikali yake inafuata mfumo wa Bunge – chama ambacho kinashinda wabunge wengi ndicho huunda Serikali, na kiongozi wa chama huthibitishwa kuwa Rais, kwa hiyo kiongozi msaidizi wa chama huteuliwa kuwa makamu wa Rais.

Hivyo, katika hali ya sasa, Mbeki hapaswi kushangilia baada ya Zuma kuanguka, badala yake anastahili kuongeza kilio, maana timu yake ya kuwania madaraka baada ya Mandela imeangushwa jumla. Alianguka yeye 2008 na sasa Zuma, Mshindi ni Ramaphosa ambaye alikuwa hasimu wao.

Hivyo, Ramaphosa ndiye anachekelea maana amewaangusha mahasimu wake wote baada ya miaka 25 ya mapambano.

Maelewano ya Zuma na Mbeki yalikuwa sababu ya Zuma kutochukua fomu ya kugombea unaibu rais wa ANC mwaka 1994, hivyo kumwacha Mbeki akipita bila kupingwa.

Safari hiyo ya mwaka 1994, ilikuwa matayarisho ya kuchukua hatamu ya uongozi kama marafiki kwenye uchaguzi wa chama mwaka 1997, pale Mandela alipojiweka pembeni.

Safari ya Zuma, Mbeki

Mbeki na Zuma walikuwa marafiki hasa kuanzia 1975 walipokutana Swaziland kimkakati, wakiwa vijana waaminifu wa Tambo. Wanajua siri kamili ya kushinda vita ya dhidi ya ubaguzi wa rangi. Wanazijua nyakati ngumu za kumtetea Mwafrika Kusini.

Kati ya mwaka 1987 mpaka 1990, Tambo aliwateua Mbeki na Zuma kuwa wahusika kwenye mazungumzo ya mwafaka kati ya ANC na Serikali ya Kikaburu Afrika Kusini. Desemba 1997, Mbeki alipochaguliwa kuwa Rais wa ANC, Zuma alikuwa naibu rais wa chama. Mwaka 1999 Mbeki alipokiongoza chama chake kushinda uchaguzi, alichaguliwa kuwa Rais, kisha Zuma akawa naibu wa rais.

Mwaka 2004, urafiki wao uliingia mdudu, baada ya Zuma kushambuliwa na kashfa mbili za jinai. Kesi ya kwanza ilikuwa ya ubakaji, ya pili ni ufisadi. Ni kashfa hizo ambazo zilimfanya Zuma aandamwe na vyombo vya habari na Bunge. Mwisho Mbeki aliamua kumpumzisha Zuma Juni 14, 2005.

Ushirika wa Zuma na Mbeki ulivurugwa na kashfa ya silaha za jeshi la Afrika Kusini, ikidaiwa kuwa baadhi ya vigogo walihongwa fedha nyingi kurahisisha biashara hiyo kufanyika 1999, chanzo chake ni baada ya Serikali ya Afrika Kusini kufanya maboresho ya silaha za kijeshi kwa kununua nyingine.

Vigogo wengine waliotajwa kwenye kashfa hiyo ni mfanyabiashara tajiri Afrika Kusini ambaye alikuwa pia mshauri wa kifedha wa Zuma, Schabir Shaik pamoja na mdogo wake, Chippy Shaik.

Mwanasiasa na mfanyabiashara aliyekuwa na nguvu kubwa Afrika Kusini, Fana Hlongwane, yeye uhusika wake ulitokana na kuwahi kuwa mshauri wa kifedha wa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, enzi za utawala wa Mandela, Joe Modise, aliyefariki dunia mwaka 2001.

Wakati kashfa hiyo inaibuka mwaka 2002 na kutikisa Bunge mwaka 2003, Modise alikuwa ameshafariki dunia, hivyo akapona kutajwa. Mwaka 2003, aliyekuwa Mnadhimu wa ANC bungeni, Tony Yengeni alikiri kupokea rushwa, hivyo kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela tangu mwaka 2004.

Sababu ya Zuma kuondolewa kazini ni baada ya Shaik ambaye alikuwa mshauri wake wa kifedha na mfanyabiashara maarufu, kukutwa na hatia ya kashfa hiyo, hivyo kuhukumiwa kifungo jela miaka 15. Katika hukumu ya Shaik, Jaji aliyeendesha kesi hiyo, Hilary Squires alitaja jina la Zuma mara 471.

Ni namna jina la Zuma lilivyotajwa mara nyingi kiasi hicho, ndiyo sababu iliyoviamsha vyombo vya habari na wanasiasa hasa vyama vya upinzani, kuhoji mno, hivyo Juni 14, 2015, Mbeki alilihutubia Bunge na kusema:

“Kwa masilahi ya mheshimiwa Naibu Rais na Serikali, mfumo wetu mchanga wa kidemokrasia na nchi yetu, litakuwa jambo bora kama tutamwondoa Jacob Zuma kwenye majukumu yake ya Naibu Rais wa Jamhuri na mjumbe wa baraza la mawaziri.”

Kama Naibu Rais, Zuma alikuwa pia mbunge, hivyo baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya Naibu Rais, alijiuzulu na ubunge. Zuma alifunguliwa mashtaka ya ufisadi kwa kuhusika kwake kumsaidia Shaik katika dili la silaha, lakini Zuma alishinda kesi na jaji alisema kuwa Mbeki kama Rais alihusika kushinikiza mashtaka hayo.

Mbeki alikuwa Rais wa ANC tangu mwaka 1997, Zuma akiwa naibu wake. Aliongoza chama kwa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja. Mwaka 2007, baada ya Mbeki kuwa Rais kwa miaka 10, na miaka miwili tangu Zuma alipoondolewa katika cheo cha Naibu Rais wa Afrika Kusini, uhasimu wao ukadhihirika kwenye Uchaguzi Mkuu wa ANC mwaka 2007.

Mwaka 2007, Mbeki na Zuma wote walichukua fomu za kuwania urais wa chama. Hivyo, kwa mara ya kwanza marafiki wenye historia kubwa na inayofanana ya ukombozi wa Afrika Kusini, waliingia kwenye uchaguzi ili kupimana ubavu, baada ya kuachiana nafasi kwa muda mrefu.

Kusimama kwa Mbeki na Zuma kugombea urais wa ANC, kilikuwa kishindo cha vigogo kwenye chama, kwani tangu kifo cha Hani, kisha kufanikiwa kumdidimiza Ramaphosa, Zuma na Mbeki ndiyo walionekana kuwa watu wazito zaidi kwenye chama.

Dalili za mpasuko zilikinyemelea chama. Ilionekana kwamba chama kingegawanywa pande mbili. Ushauri wa wengi ukawa ama Ramaphosa au Tokyo Sexwale mmoja achaguliwe ili kukiunganisha chama, maana wao hawakuwa na makundi.

Hata hivyo, nguvu ya Zuma na Mbeki haikuruhusu mgombea mwingine apenye katikati.

Uchaguzi ulipofanyika, Zuma alimshinda Mbeki, hivyo kuwasha taa mpya ya mabadiliko ya utawala kwenye nchi. Kilichotokea Afrika Kusini mpaka Mbeki kuwekwa pembeni kama Rais wa nchi, kinatazamwa kama mapinduzi ya kisayansi ambayo Zuma aliyafanya kumpumzisha Mbeki kwenye utawala.

Baada ya Zuma kumshinda Mbeki, hukumu ya mashtaka ya ufisadi yaliyokuwa yanamkabili Zuma ilisomwa. Hukumu hiyo ya Mahakama Kuu iliyosomwa na Jaji Christopher Nicholson, ilihitimisha safari ya Mbeki kama mtawala wa Afrika Kusini.

Septemba 12, 2008, Jaji Nicholson akisoma hukumu kesi ya Zuma na ufisadi, alisema kuwa Mbeki kama Rais wa nchi aliingilia Idara ya Mashtaka katika kesi hiyo, hivyo akahitimisha kwamba mashtaka dhidi ya Zuma hayakuwa na msingi wowote.

Baada ya hukumu hiyo, Zuma akiwa Rais wa ANC, alichochea kuitishwa kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya ANC haraka ambacho kilifikia uamuzi wa kumtaka Mbeki ajiuzulu urais kutokana na kashfa ya kuingilia mashtaka kama hukumu ilivyosomwa na Jaji Nicholson.

Septemba 20, 2008, ikiwa ni siku nane baada ya hukumu ya Jaji Nicholson na ikiwa imesalia miezi tisa ili amalize muhula wake wa pili kama Rais wa Afrika Kusini, Mbeki alitangaza kujiuzulu ili kutii wito wa ANC, kisha Kgalema Motlanthe alichaguliwa na chama kuwa Rais wa mpito na kuapishwa Septemba 24, 2008.

Mei 9, 2009, baada ya ANC kushinda Uchaguzi Mkuu Afrika Kusini, Zuma aliapishwa kuwa Rais wa Nne. Januari 12, 2009, ikiwa ni miezi minne kabla ya Zuma kuingia madarakani kama Rais wa Afrika Kusini, Mahakama ya Juu ya Rufaa Afrika Kusini, iliibadili hukumu ya Jaji Nicholson, kwamba Mbeki hakuingilia mashtaka dhidi ya Zuma, ingawa haikuwa na msaada wowote kwa Mbeki.