UCHAMBUZI: Ufugaji ni nguzo ya viwanda vya maziwa nchini

Muktasari:

Bila maziwa ya kutosha, usindikaji wenye tija hautakuwepo. Kwa mantiki hiyo, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa ni kiungo na sehemu muhimu ya mtandao mzima wa viwanda vya maziwa nchini.

Uhai na mafanikio ya viwanda vya usindikaji wa bidhaa za maziwa nchini, kwa kiasi kikubwa utategemea uzalishaji na upatikanaji wa maziwa ya ng’ombe kutoka kwa wafugaji hususan wadogo.

Bila maziwa ya kutosha, usindikaji wenye tija hautakuwepo. Kwa mantiki hiyo, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa ni kiungo na sehemu muhimu ya mtandao mzima wa viwanda vya maziwa nchini.

Ili kuvifanya vishamiri, jitihada lazima zianzie katika ufugaji wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa. Katika nchi zilizo tambua umuhimu na thamani ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, bidhaa ya maziwa hutambulika kama ‘dhahabu nyeupe.’ Ni bidhaa iliyo wakomboa wanyonge wengi kiuchumi.

Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ni ‘kiwanda rafiki’ kwa Watanzania wengi wenye kipato cha chini na kati vijijini. Ni shughuli ya kiuchumi ambayo ikipewa msukumo stahiki, ina uwezo mkubwa wa kuwakwamua mamilioni ya wananchi kutoka katika lindi la umasikini.

Ni sekta ambayo haihitaji teknolojia au mtaji mkubwa usioweza kupatikana. Ni aina ya mradi unaowezekana kwa Watanzania wengi wenye dhamira ya kujinasua kiuchumi.

Kinachokosekana ni utashi wa dhati wa serikali, mikakati na mipango thabiti na shirikishi, inayotekelezeka kutoka kwenye vituo visivyo pungua 15 vya uzalishaji wa ng’ombe wa kisasa nchini.

Vituo vya uzalishaji na mafunzo vipewe msukumo ili kuwanufaisha wafugaji waliopo na wote waliodhamiria kuanza ufugaji wa kisasa katika wilaya mbalimbali nchini ambako hali ya hewa na mazingira yanaruhusu.

Baadhi ya vituo vya uzalishaji wa ng’ombe wa kisasa ni Shamba la Asas lililopo mkoani Iringa pamoja na lile la Kibebe na SaoHill. Lipo pia shamba la Kitulo, mkoani Njombe na Mabuki la Mwanza. Yapo mashamba ya utafiti; Mpwapwa, Tanga na Uyole. Vipo vingine ambavyo ni Ngerengere na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) bila kusahau mashamba ya LITI, Molomo, Rongai, Malonje, Sanya Juu na Dakawa.

Vituo hivyo vina ng’ombe wa kisasa wasiopungua 13,000 na endapo vikishirikishwa ipasavyo, vinaweza kuleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.

Katika vituo na mashamba yanayomilikiwa na sekta binafsi, taratibu zinaweza kufanyika, kama misamaha ya kodi kwa shughuli zote za kama motisha mojawapo katika kuchochea jitihada hizo.

Ingawa Tanzania ni nchi ya tisa duniani, na ya tatu katika bara la Afrika kwa idadi kubwa ya ng’ombe wa maziwa wengi ni wa kienyeji ambao wana uwezo mdogo wa kuzalisha maziwa kwa siku. Kwa bei iliyopo sasa, ng’ombe wa kisasa anakadiriwa kutozidi Sh700,000.

Unywaji wa maziwa nchini unakadiriwa kuwa ni wastani wa lita 45 kwa kila Mtanzania kwa mwaka. Wakenya wana wastani wa lita 145 kwa mtu mmoja kwa mwaka. Na kiwango kinachokubalika kimataifa, ni wastani wa lita 200 kwa kila mtu kwa mwaka.

Maziwa yaliyosindikwa yanaonekana kama vile ni bidhaa ya anasa kwa Watanzania wengi. Lita moja ya maziwa freshi yaliyosindikwa inagharimu Sh2,000 na hayapatikani kwa urahisi kila mahali.

Ili viwanda hivi viweze kutosheleza mahitaji ya kitaifa na kushindana kimataifa ni lazima vijengewe uwezo wa kuzalisha maziwa yenye uwezo wa kukaa muda mrefu bila kuharibika na kuzalisha maziwa ya unga ambayo kilo moja yake inahitaji lita 8.5 za maziwa freshi.

Mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ni pamoja na kuwa na sera makini na mipango shirikishi.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya uchumi. Anapatikana kwa: 0683 555 124.