Ufundishaji wa mitihani unawadumaza wanafunzi

Wanafunzi wakifanya mtihani.Wanafunzi wanaofundishwa kwa kupitia mitihani ya zamani wanakosa ari ya kujiamini. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Pamoja na Serikali yetu kuweka nguvu kubwa katika sekta hii, bado majibu kuhusu kitu kinachosababisha elimu yetu kushuka hakijapatikana au hakijashughulikiwa na hivyo Taifa letu linakosa dira katika eneo hili.
  • Ukiachilia mbali Serikali, pia wapo wadau mbalimbali ambao nao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa ya kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu, lakini huko nako hakuna majibu ya msingi.

Elimu ya Tanzania imekuwa ikishuka kila kukicha, na siku hizi linaonekana ni jambo la kawaida kabisa! Maswali ni mengi kuliko majibu.

Pamoja na Serikali yetu kuweka nguvu kubwa katika sekta hii, bado majibu kuhusu kitu kinachosababisha elimu yetu kushuka hakijapatikana au hakijashughulikiwa na hivyo Taifa letu linakosa dira katika eneo hili.

Ukiachilia mbali Serikali, pia wapo wadau mbalimbali ambao nao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa ya kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu, lakini huko nako hakuna majibu ya msingi.

Katika makala haya, sitegemei kutoa majibu ya kwa nini elimu yetu inashuka siku hadi siku, bali nitaongelea jambo moja ninalofikiri kuwa linachangia kushuka kwa elimu, hasa ufaulu wa wanafunzi.

Katika shule nyingi kumeibuka mtindo wa walimu kufundisha kwa kutumia mitihani iliyopita na kutoa mazoezi mengi bila kujali kama wanafunzi hao wameshafundishwa vya kutosha na kuelewa ama la.

Walimu wengi wa shule za msingi wanatumia mbinu ya kuwapa wanafunzi mitihani iliyopita, ili wajipime kama wataweza kufaulu mitihani yao. Mitihani hii wakati mwingine hufanyika siku za Jumamosi.

Jambo hili ukiliangalia vizuri, utaona kuwa si sahihi kwani wanafunzi kama wafanyakazi nao wanahitaji kupumzika. Lengo la shule sio kufaulu mitihani pekee, bali ni mwanafunzi kuelewa mambo ili yamsaidie maishani.

Kwa wanaokumbuka zamani, wanafunzi walikuwa wanatoka shuleni mapema, na sikumbuki kama niliwahi kuona wanafunzi hasa wa shule za kutwa wakiwa shuleni hadi saa kumi na moja jioni.

Utaratibu huu uliwasaidia wanafunzi kurudi nyumbani mapema kwa ajili ya kufanya usafi wa mwili, nguo zao na pia kusaidia kazi za nyumbani na kucheza.

Shughuli hizi kwa namna moja au nyingine zilimsaidia mwanafunzi kuelewa umuhimu wa kufanya kazi na zilimfanya alinganishe anachofundishwa shuleni na hali halisi ya maisha ya mwanadamu na mazingira yanayomzunguka.

Pia utaratibu huu, ulimwezesha mwanafunzi kupumzisha akili yake tayari kwa masomo ya siku inayofuata.

Hata hivyo, kwa sasa sio rahisi tena kuwa na mazingira yaliyopita, kwani hata idadi ya wanafunzi imeongezeka hivyo kuilazimu Serikali kuanzisha mikondo mingi na wanafunzi kusoma kwa zamu.

Hii imesababisha baadhi ya wanafunzi kuingia darasani mchana na kutoka jioni huku wakikosa nafasi ya kupumzisha akili zao.

Hili nalo ni tatizo kubwa. Hebu fikiri wewe kama ni mfanyakazi, uwe unakwenda kazini kila siku bila kupumzika; Hivi utakuwa na tija kweli? Turudi katika lile tatizo kubwa la kufundisha kwa kutumia mitihani iliyopita.

Kwanza ni vema tukajiuliza ni kitu gani kimesababisha walimu kupenda kutumia mbinu hii ya kuwapa wanafunzi mitihani iliyopita kama sehemu ya mazoezi.

Miaka ya nyuma, walimu walifundisha kwa kutumia silabasi bila kujali mitihani itatoka vipi.

Wakati huo wanafunzi waliingia katika chumba cha mtihani bila hata kujua karatasi ya mitihani inafananaje.

Kwa sekunde chache kabla ya kuanza kufanya mtihani, wengi tuliutumia muda huo kuiangalia karatasi kwa umakini kabla ya kuanza kusoma maswali.

Kwa mwanafunzi aliyefundishwa vizuri, atajibu maswali kwa kujiamini bila hofu yoyote, na ni ukweli usiofichika kuwa hata swali lingetungwa kwa ujanja wa namna gani bado mwanafunzi aliyeiva vizuri atajibu tu!

Hii inaonyesha kuwa mwanafunzi akifundishwa vizuri hatakuwa na shaka yoyote, na wala hatahitaji mazoezi mengi ya mitihani iliyopita, kwani uelewa uliowekwa kichwani kwake na walimu wake unatosha kujibu maswali yoyote alimradi yawe yanahusiana na yale aliyofundishwa.

Hili linajidhihirisha kwa kuangalia matokeo ya mitihani ya Taifa ya zamani na sasa.

Angalia jinsi wanafunzi wa siku hizi wanavyofeli, licha ya kufundishwa na kufanya mazoezi ya mitihani iliyopita.

Nafikiri ni vema kwa wadau wa elimu kuangalia jambo hili na kulishughulikia. Mara nyingi Watanzania tumekuwa wagumu kutafuta mbinu mbadala.

Kwa mfano, kama tumeona njia hii ya kutumia mitihani iliyopita haitusaidii, kwa nini tuendelee kuing’ang’ania?

Kwa nini tusirudi tulipotoka ambapo walimu walitunga maswali wao wenyewe kutokana na walichofundisha?

Utaratibu huu wa kutumia mitihani iliyopita unapaswa kupigwa vita, kwani pamoja na kwamba hausaidii ufaulu, pia unadidimiza uwezo wa mwalimu kuwa mbunifu katika ufundishaji.

Kimsingi, mwalimu huyu wakati wote hatofikiri namna ya kutunga swali wala kujali kama wanafunzi wameelewa anachofundisha.

Kwa upande wa mwanafunzi, naye anakosa ile nafasi ya kufundishwa vizuri. Pia hatahangaika kujisomea yale yote aliyofundishwa, kwani atajikita tu katika kujibu maswali ya mitihani iliyopita. Matokeo yake akili yake itadumaa.

Pia mitihani ikibadilika au kutungwa kwa ujanja zaidi, mwanafunzi huyu hataweza kutumia elimu yake kujibu swali, kwani tayari atakuwa ametaharuki katika chumba cha mtihani

Ni vema sote tukaelewa kuwa Taifa hili halitasonga mbele kwa kutumia ujanja ujanja tu. Ni lazima kuwe na bidii katika kila jambo, badala ya kuwa Taifa la wachakachuaji