Uhuru wa kujieleza kisiasa mitandaoni hatarini

Muktasari:

  • Kule China, mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Blogu na google hazipatikani. Lakini watu wamepata njia za kuizunguka hiyo marufuku.

Nilipokuwa China kwa masomo ya Shahada ya Udaktari wa Falsafa, nilipata ujuzi wa mambo kadhaa ambayo sikuyatarajia.

Kwanza, nilijifunza lugha ya Kichina na utamaduni wao ikiwemo chakula. Kumbe bwana kuna chura wakubwa kama kuku na ukimkuta anachomwa utasema ni kuku.

Pili, nilijifunza kuishi katika nchi ambayo kuna ukandamizaji mkubwa wa uhuru wa kujieleza.

Katika hili la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, nilijifunza kuwa, hata ubane njia za watu kujieleza, watu hutafuta tu namna ya kutetea uhuru wao huu.

Kule China, mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter, Blogu na google hazipatikani. Lakini watu wamepata njia za kuizunguka hiyo marufuku.

Kwa kawaida, Wachina wana mitandao yao ya kijamii ambayo Serikali ina udhibiti kamili na uwezo wa kufuatilia kila kinachoendelea.

Mitandao yao ni pamoja na Sina Weibo, Wechat, QQ, Sina Weibo, Renren, Pengyou, Douban, Diandian, Youku.

Ukiacha mitandao ya kijamii, kule China pia kumkosoa rais na Serikali ni jambo la hatari. Kwa hiyo, ukiingia katika mitandao yao ya kijamii, utakuta sifa tu za rais, hakuna ukosoaji. Watu wanaogopa.

Hata hivyo, licha ya makucha ya Serikali na mabavu ya kudhibiti maudhui katika mitandao, watu wametafuta njia nyingine za kukosoa bila kujulikana.

Nasikia watu wamepata namna nyingine ya kuwataja wakuu wa nchi bila kutaja majina yao, yaani matumizi ya mafumbo.

Jinsi Serikali inavyokuwa ‘janja’ katika kung’amua mafumbo, ndivyo watu walivyotumia mafumbo magumu zaidi.

Usidhani hayo ni mambo ya China tu, hata Tanzania watu wameanza kutumia mafumbo katika kuisema Serikali.

Mimi ni mwanachama wa Jamii Forums wa muda mrefu lakini situmii jina langu halisi. Naipenda Jamii Forums kwa sababu ni kielelezo cha uhuru mkubwa wa kujieleza na majadiliano uliopo Tanzania. Juzi nikaingia katika mtandao wa huo nikakutana na posti iliyoandikwa kwa mafumbo.

Jamaa kaandika:  “Mwaka 2020 kuna uchaguzi kijijini kwetu, mfalme anayetawala sasa ni katili, hashauriki na kila mtu anamwogopa, mpaka wasaidizi wake wa karibu kabisa.”

Nilipoona hii nilicheka. Nilicheka zaidi baada ya kusoma maoni ya wachangiaji wengine.

Mchangiaji mmoja aliandika: “Inaelekea tupo kijiji kimoja....maana nasi mfalme wetu hataki tumwambie lolote kuhusu njaa tuliyonayo, ukimtuma hata mjumbe wa kata akamweleze tulivyopigika, yeye anamjibu kuwa wananchi wake walizoea kupiga dili, sasa eti wacha tulimie meno.”

Mwingine akahoji: “Hivi mfalme bado mshauri wake mkuu ndiyo yule mfalme wa jirani aliyemshauri tununue njiwa badala ya maksai wakati kijiji chetu kinategemea kilimo?”

Na kuna huyu mchangiaji aliyedai: “(Mfalme) anaamini ana majibu ya Mungu kwa kijiji chake. Hakuwa na ndoto ya kuwa mfalme. Inasemekana ameanza kuota sasa namna ya kukipeleka kijiji mbele”.

Watu wawili wakamaliza kabisa mjadala kwa hitimisho mujarabu: “Kumbe siku JamiiForums tukidukuliwa na bwana yule bado tuna njia nyingi za kuwasilisha mada zetu!” Mwingine akaandika: “Ndiyo tuanze kujifunza mbinu za kukwepa mkono wa sheria.”

Na kweli watu wameanza kujifunza mbinu za kuijadili Serikali bila kutaja watu moja kwa moja.  Magufuli  ameanza kupata a.k.a nyingi  – maarufu zaidi ya ile aliyoiomba kutoka kwa Mpoto: Sizonje.

Watu wanaogopa

Watu wanaogopa hususan wanaposhuhudia Serikali ‘ikipaniki’  kwa sababu watu  wamemwita rais majina asiyoyapenda.

Watu wanahofu zaidi wanaposikia Serikali inatafuta taarifa za watu katika majukwaa yao ya kupumulia kisiasa: Mitandao ya kijamii.

Mitandao hii ya kijamii imekuwa muhimu katika kupashana habari na kubadilishana maoni.

Changamoto zake ni kiduchu ukilinganisha na faida zake lukuki katika nchi ambayo watu wengi hawana muda wa kufuatilia habari katika vyombo vya habari vya asili, redio,  runinga na magazeti.

Licha ya faida kibao za mitandao ya kijamii siyo kisiasa, hata kiuchumi na kijamii, miezi michache iliyopita Rais John Magufuli alinukuliwa kusema anatamani malaika ashuke aje kuizima mitandao ya kijamii, ambayo amekuwa akituhumu watumiaji kwa kuandika mambo yasiyofaa hasa ukosoaji.

Rais inamuuma hata watu wanaposema tu ndege hazina kasi! Kujibu uzushi huo haitoshi, akatamani hiyo njia inayotumiwa kukosolea isiwepo kabisa – kuwe na giza kisiasa.   Jitihada za kudhibiti mitandao ya kijamii zikifanikiwa, watu wakiogopa kutoa maoni na kujadiliana utakuwa ni msumari wa mwisho katika jeneza la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni ya kisiasa.

Ni msumari wa mwisho kwa sababu huko nyuma, kumekuwa na marufuku dhidi ya maandamano ya kisiasa na vilevile dhidi  mikutano ya hadhara na ya ndani. Kama vile haitoshi, hatua kali zimewahi kuchukuliwa dhidi ya vyombo vya habari vya machapisho na hata utangazaji.

Lakini tukajifariji kuwa waache wadhibiti maudhui ya vyombo vya habari na hata mikutano ya kisiasa. Madhali tuna mitandao ya kijamii tutapashana habari na kuendesha mijadala huko.

Kinachoelekea kutaka kutokea sasa ni kubanwa pumzi, tusipumue tena kisiasa hata kwenye majukwaa yetu wenyewe wananchi ambapo tunapeana tunapashana habari, umbeya, tetesi, nadharia za uongo na kubuni juu ya tafsiri ya matukio ya kisiasa – kwa ujumla tupo huru.

Tuacheni tupumue

Mitandao ya kijamii ni majukwaa ya wananchi ya kupumulia kisiasa. Kupumua ni kitendo cha kutoa hewa chafu na kuvuta safi. Wote tuliohai tunapumua. Pumzi zikikata, kwa sababu yoyote ile tunakufa. 

Tuacheni tupumue tutoe hewa chafu ya  fukuto la hisia  iwe hasira au furaha, kwa aidha mazuri tunayofanyiwa au mabaya.

Natamani viongozi wa Serikali yetu wangeelewa kuwa huu ukosoaji, hizi hasira, haya maneno makali yanayotolewa, ni msaada mkubwa kwao kwani ni njia bora ya kupima joto la kisiasa na kujua maoni ya wananchi. Viongozi wajanja huacha mijadala hiyo iendelee ikomae wakijua inasaidia kuwajua wananchi wao. 

Pia, watu wanapotoa hisia wanaondoa fukuto moyoni ambalo likikosa pa kutokea hutokea yale ya Libya na Syria. Kule Libya, baadhi yao  wanaamini licha ya nchi yao  kuvurugika, zama za sasa ni bora kuliko zama za Muammar Ghadafi. Hizi siyo stori. Nimekutana na wa Libya wanaoamini hivyo. 

Najua wakuu wa Serikali wana hoja kibao za kutetea wanachofanya. Na labda hata wanachofanya huenda ni sahihi kisheria. Lakini haya yanatokea yana athari kubwa katika ujenzi wa demokrasia yetu. 

Siyo sahihi kuzipima kauli na hisia zinazotolewa kisiasa kwa jicho la sheria. Utashtaki wengi na huenda hata utafunga wengi. 

Uongozi lawama. Uongozi ni utumishi wa watu.  Viongozi wawe na ngozi ngumu, wakubali kusemwa vibaya, kukosolewa, kuitwa majina wasiyoyapenda, kuchekwa, kukejeliwa, kudhihakiwa na wale wanaowatumikia.  Nimalize kwa maneno ya Profesa Issa Shivji niliyoyakuta katika akaunti yake ya Twitter. Amesema: “Panda hofu, vuna hasira. Kandamiza uhuru, pata ukimya. Hasira na ukimya zikichanganyika, zinanyesha laana za mababu”.