Ukizubaa tu, wamekuliza

Muktasari:

Tambo hizo huwa zinaibuka kutokana na kila mmoja kujivunia ubora wa wachezaji kuwa ni zaidi ya mwenzake.

Mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga unavuta hisia za wengi huku tambo za hapa na pale zikiibuka kutoka kwa mashabiki wa timu hizo.

Tambo hizo huwa zinaibuka kutokana na kila mmoja kujivunia ubora wa wachezaji kuwa ni zaidi ya mwenzake.

Hata hivyo katika kila timu kuna wachezaji hatari wanaoangaliwa sana na mashabiki na hata kuwatia tumbo joto timu pinzani.

Hawa ni baadhi ya wachezaji nyota wanaotarajiwa kutikisa katika mchezo huo utakofanyika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, lakini watachungwa sana uwanjani wasilete madhara.

 

Ibrahim Ajib - Simba

Mshambuliaji huyu ni hatari sana uwanjani na ndiye roho ya Simba kwa sasa. Mabeki wa Yanga wanatakiwa kuwa naye makini hasa anapokaribia lango lao kwani ni mzuri na mwenye maamuzi ya haraka.

Ni mzuri katika kufunga lakini ni hatari kwa pasi za mwisho kwa wenzake, sifa yake kubwa inayowafurahisha mashabiki wa timu hiyo ni uwezo wake wa kuwatoka wachezaji wengi wa timu pinzani kwa chenga zake za maudhi.

 

Juma Abdul - Yanga

Mashabiki wengi wanasema huyu ndiye beki bora wa kulia kwa sasa nchini kutokana na soka yake anayoionyesha uwanjani.

Simba watamungalia sana katika mechi yao kwani ni mzuri katika kupandisha mashambulizi lakini ni hatari sana katika upigaji wa krosi. Amechangia mabao mengi katika kikosi cha Yanga msimu uliopita na hata msimu huu kutokana na krosi zake maridadi. Kila akipanda katika lango la wapinzani na kutaka kupiga krosi mashabiki wengi wanahesabu kuwa ni bao.

Beki huyu ndiye anastahili kuchungwa sana na Simba katika mchezo huo kuliko mtu yoyote kwani mara nyingi ushindi wa Yanga huwa unaanzia kwake.

 

Laudit Mavugo- Simba

Raia wa Burundi ambaye Simba wana mategemeo naye makubwa katika ufungaji magoli, hivyo atatakiwa kuthibitisha hilo kwa kuhakikisha anifunga Yanga ili aendelee kuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo. Wengi watamuangalia hasa mabeki wa Yanga watakuwa makini naye kwani ameonyesha makeke kwenye mechi chache tu alizoichezea Simba kwa kuifungia mabao matatu.

Licha ya kwamba wakati mwingine anaongoza kwa kukosa mabao ya wazi, lakini ni mtu hatari anapokuwa katika lango la wapinzani, hivyo katika mchezo wa Jumamosi ni mchezaji atakayekuwa akichungwa sana na Yanga.

 

Amissi Tambwe - Yanga

Mfungaji bora wa msimu uliopita ambaye msimu huu tayari ameanza safari ya kutetea nafasi yake kwani amefunga mabao matatu mpaka sasa.

Ni hatari sana kwa mabao ya vichwa, hivyo mabeki wa Simba wanapaswa kumchunga sana kwani wakizembea tu atawalaza mapema Jumamosi kama alivyowafanya msimu uliopita.

 

Shiza Kichuya - Simba

Wanamuita Kiberenge kwa jinsi alivyo na kasi na hivyo wengi kusema kuwa anaweza akawa mrithi wa Mrisho Ngassa ambaye soka lake linaelekea ukingoni.

Mpaka sasa ameifungia timu yake mabao mawili na antazamia kuwa mwiba mkali katika mchezo wa Jumamosi na Yanga wanafahamu kuwa watakuwa na kazi ya kumkaba ili kuhakikisha haleti madhara.

Ana sifa ya kasi na kupandisha mashambulizi huku pia akiwa na uwezo wa kufunga mabao kwa staili zote, ndani ya eneo la hatari na hata nje ya eneo la hatari, hivyo Yanga wanapaswa kuwa naye makini.

 

Donald Ngoma - Yanga

Msimu uliopita aliwafunga Simba bao moja Yanga ikipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mzunguko wa pili wa ligi, hivyo hata Jumamosi ana nafasi kubwa ya kutamba katika mchezo huo.

Ni mshambuliaji msumbufu, mwenye kasi na anayelijua goli, hivyo mabeki wa Simba lazima wanampangia mikakati huko waliko kwani wanaijua shughuli yake.

Alizua tafrani msimu uliopita alipowafunga Simba huku pasi ya goli ikitoka kwa beki wa pembeni, Hassan Kessy aliyemrudishia vibaya kipa wake na mpira kunaswa na mfungaji. Tukio hilo lilimuondoa Kessy katika kikosi cha Simba na hivi sasa wako wote Yanga.

Mabeki wa Simba wanapaswa kuwa naye makini kwani ni mchezaji ambaye anaweza kuwasababishia kadi muda wowote kama wakimkaba kizembe kwani ana kasi na ni mjanja sana uwanjani na ndiyo maana haikushangaza kuona msimu uliopita beki Abdi Banda akitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 20 tu baada ya kumfanyia madhambi Ngoma.

 

Moh’d Hussein ‘Tshabalala’ - Simba

Hivi sasa anataka aitwe Zimbwe na siyo Tshabalala ingawa itachukua muda mrefu kwani wengi wamelizoea jina hilo.

Mmoja wa mabeki wa pembeni anayekuja juu kwa sasa na haikushangaza msimu uliopita kuibuka mchezaji bora chipukizi.

Sifa yake kubwa ni uwezo wa kupandisha mashambulizi na kupiga krosi za mabao kwa wenzake na mabao mengi waliyofunga Simba msimu huu amechangia kwa kiasi kikubwa kutokana na krosi zake mahiri. Yanga inabidi wawe naye makini kama hawataki kupata madhara katika lango lao, kama wakimuacha acheze anavyotaka basi wanaweza wakajikuta wakilazwa mapema Jumamosi

 

Thaban Kamusoko - Yanga

Wanamuita fundi kutokana na soka la kiwango analolionyesha uwanjani, pasi zake, nguvu na akili zimewavutia mashabiki wengi Yanga na timu pinzani.

Ni mzuri katika kutoa pasi za mwisho na hata mipira ya faulo, hivyo Simba wanatakiwa kuwa naye makini sana.

Hutumia vizuri dimba la 18.

‘Simba, Yanga zote zina udhaifu’