Ukweli ni upi kuhusu kujiuzulu kwa Jumbe?

Muktasari:

Kilichoelezwa mara kwa mara ni kwamba alijiuzulu nyadhifa zote hizi tatu Januari 30, 1984 kule Dodoma baada ya kufanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

Mengi yamezungumzwa, lakini mengi yamefumbiwa macho juu ya maisha na msimamo wa kisiasa wa aliyekuwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, aliyefariki Jumapili iliyopita na kuzikwa siku ya pili yake.

Kilichoelezwa mara kwa mara ni kwamba alijiuzulu nyadhifa zote hizi tatu Januari 30, 1984 kule Dodoma baada ya kufanyika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC).

Kikao hiki cha NEC ambacho hadi hii leo kimekuwa kikitolewa maelezo ya utatanishi kilijadili kile kilichoelezwa wakati ule na kwa muda mrefu baadaye kama kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa visiwani na kuutikisa mustakabali wa Muungano.

Yapo mambo mengi ambayo ni ya utatanishi na yamefunikwa kama vile Watanzania na hasa Wazanzibari hawana haki na hawastahiki kujua kilichotokea Dodoma.

Kilichokuwa wazi ni kwamba ipo tofauti kubwa ya maelezo yaliyotolewa kuhusu Jumbe wakati alipoachia ngazi za uongozi na baada ya kuiaga dunia.

Wakati aliposemekana kujiuzulu kule Dodoma tuliambiwa aliichafua hali ya hewa ya kisiasa na kutaka kuidhoofisha nchi kwa kutaka Muungano ufanyiwe marekebisho na kupendekeza kuwapo mfumo wa Serikali tatu, moja ya Zanzibar, ya pili ya Tanganyika na nyingine ni ya shirikisho.

Hapo ndipo palisikika msemo wa ‘moja na moja haiwezekani kuwa tatu’ uliotolewa na baba wa taifa, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.

Walikuwapo waliosema moja na moja haiwezekani kuwa moja, isipokuwa moja mara moja ndiyo moja. Falsafa hizi ziliwakanganya Watanzania na hadi hii leo hayapo maelezo ya wazi ya kilichofichwa na wanasiasa ndani ya falsafa hizi.

Mzee Jumbe alinyooshewa vidole kama mtu aliyetaka kuudhofisha Muungano kwa kushauri kuwapo marekebisho ili uwe wa serikali tatu.

Hata hivyo, baada ya kifo chake na wakati wa mazishi yake alielezwa kama kiongozi ambaye alikuwa jasiri na mwaminifu na aliyeupenda na kuutetea Muungano. Ingelikuwa sifa hizi alipewa wakati akiwa hai, angeweza kuhoji kulikoni?

Ilikuwaje hata akawa mtu ambaye hakuutakia mema Muungano na kujizulu uongozi, lakini ikawa kinyume chake baada ya kuiaga dunia?

Ukweli ni kwamba mambo ya utatanishi juu ya uongozi wa Mzee Jumbe na kilichosababisha aachie ngazi ni simulizi ndefu, lakini nitagusia machache na kuacha wasomaji watafakari na labda watagundua kilichojificha.

Hebu tujiulize yafuatayo:

Hivi Mzee Jumbe alijiuzulu au alilazimishwa kujiuzulu?

Mzee Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar. Sasa kwa nini asitangaze kujiuzulu akiwa visiwani na badala yake afanye hivyo Dodoma?

Mzee Jumbe alikuwa kiongozi wa watu wa Zanzibar sasa ilikuwaje ajadiliwe na watu ambao siyo Wazanzibari juu ya masuala ya Zanzibar katika kikao cha NEC Dodoma?

Wengi wanaona ilikuwa sahihi kwa kikao cha NEC kuamua hatima yake ndani ya CCM, hata kumfukuza katika chama. Lakini wapo watu (wakiwamo wanasheria) wanaoona kuwa haikuwa sahihi kwa kile kikao cha NEC kuamua hatima ya Mzee Jumbe kwa Serikali ambayo yeye alikuwa ndiye Rais.

Watu wenye mtazamo huu wanasema njia sahihi ambayo ingefaa kutumika kuamua hatima yake kama kiongozi wa Zanzibar ingekuwa ni kuwaachia Wazanzibari wenyewe kufanya uamuzi.

Kwa kweli hapa upo utatanishi na Watanzania na hasa watu wa visiwani wanayo haki ya kupatiwa ufafanuzi juu ya uhalali wa hatua iliyopelekea mzee Jumbe kujiuzulu (au kulazimishwa kujiuzulu) kule Dodoma.

Jambo jingine ambalo limejitokeza ni kwamba mapendekezo ya Mzee Jumbe ya kutaka Muungano wa Serikali tatu mwaka 1984 na kuzusha mtafaruku wa kisiasa juu ya Muungano ndicho kilio kilichosikika kwa sauti kubwa katika siku za karibuni.

Kauli hizi zilisikika mitaani, kwenye vyombo vya habari, katika mikutano ya kukusanya maoni ya Tume ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na katika Bunge la Katiba lililofanyika Dodoma.

Suala ni je, hizi kauli zilizofanana na za Mzee Jumbe kwa sasa hazichafui hali ya kisiasa?

Demokrasia ya kweli hujadili masuala kama haya kwa upana, ukweli na uwazi. Hili halipaswi kunyamaziwa na ni vyema likajadiliwa ili pasiwapo utatanishi kwa watakaopitia kumbukumbu za historia ya nchi yetu siku zijazo.

Tutakaa kimya hadi lini?

Kukalia kimya masuala haya siyo vizuri kwa sababu ukimya unatoa tafsiri nyingi na nyingine huwa zinaongezwa chumvi na fitna na matokeo yake ni kudhoofisha badala ya kuimarisha Muungano wetu.

Wapo watu, hasa wale wenye misimamo ya kihafidhina wanaweza kusema kufanya hivyo ni kutonesha vidonda. Lakini ukweli ni kwamba kidonda bado kipo na ni kwa kukitonesha na kukisafisha ndiyo unaweza kukiwekea dawa na kukitibu. Tusione tabu kukitonesha kama kweli tunataka kupata dawa itakayotibu kidonda.

Kwa sasa Mzee Jumbe hatunaye tena, ametangulia mbele ya haki, lakini katika hii dunia yetu aliyoiaga tulikuwa hatujamtendea haki. Ni kweli hatuwezi tena kusikia kauli yake juu ya nini hasa kilichotokea Dodoma, kabla ya hapo na baada ya kujiuzulu lakini yapo maandishi aliyoyaacha juu ya suala hili, wapo watu waliokuwapo Dodoma katika kikao kilichomwondolea madaraka ya uongozi katika Serikali ya Zanzibar, ya Muungano na ndani ya chama alichoshiriki kukianzisha CCM.

Vilevile, wapo waliopata simulizi za ana kwa ana juu ya suala hili kutoka kwa Mzee Jumbe mwenyewe. Maeneo yote haya yanaweza kusaidia kuupata ukweli na kumaliza utata uliogubika juu ya kilichotokea. Tufanye hivyo badala ya kuwaachia watu wanaojikomba kuwa wanalijua vyema suala hili kupotosha jamii.

Nimejaribu mara mbili kupata maelezo na hisia za Mzee Jumbe juu ya kilichotokea Dodoma. Kwa bahati mbaya mara zote alikuwa akitabasamu na kumshukuru Mungu na kumalizia kwa kusema historia itamkumbuka na kumhukumu.

Lazima nikiri nilifarijika, ijapokuwa nilishangaa kwa kiasi fulani kusikia Mzee Jumbe aliyeelezwa wakati wa kujiuzulu kama mtu aliyeichafua hali ya hewa ya kisiasa anazungumzwa katika taarifa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na viongozi kama alikuwa mzalendo kindakindaki, aliyeipenda nchi yake, jasiri na mwaminifu.

Hizi ni zama za ukweli na uwazi. Ni wajibu wetu kutafuta ukweli na uwazi wa suala hili ili kuweka sawa kumbukumbu za historia ya nchi yetu. Ukweli hauogopwi bali hukabiliwa na ndiyo utakaotuacha huru.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]