Ukweli ufahamike, uongo ujitenge sakata la CUF Z’bar

Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad (katikati), msaidizi wake, Issa KheirHussein (kushoto) na Mkurugenzi wa masuala ya nje wa chama hicho,Ismail Jussa katika Mahakama ya ICC, The Hague, Uswisi. Picha ya CUF 

Muktasari:

Kwa muda mrefu Serikali za nchi nyingi ziliweka kinga kwa viongozi wao kushitakiwa kwa makosa ya mauaji, udhalilishaji, ubaguzi na uvunjaji wa haki za binadamu.

Katika dunia ya leo na hasa unapozungumzia utawala bora masuala ya haki za binadamu kuheshimiwa ni ya msingi na hayana mjadala.

Kwa muda mrefu Serikali za nchi nyingi ziliweka kinga kwa viongozi wao kushitakiwa kwa makosa ya mauaji, udhalilishaji, ubaguzi na uvunjaji wa haki za binadamu.

Kinga hii ilikuwa ni ya kukataa kuingiliwa katika mambo yake ya ndani, hali iliyosababisha madikteta kufanya ukatili walioutaka kwa wale waliowaona wapinzani wao au waliotofautiana nao kisiasa.

Mambo yamebadilika na upepo wa mageuzi unavuma kwa kasi isiyozuilika. Masuala ya haki za binadamu siku hizi hayana mpaka na hii ndiyo iliyosababisha kuundwa kwa mahakama za kimataifa kwa ajili ya masuala haya.

Tanzania imejijengea heshima na sifa katika uthamini utu wa mtu na umuhimu wa kuheshimu haki za msingi za binadamu. Tofauti na nchi nyingi imekuwa haina kigugumzi katika kuonyesha inaheshimu haki za msingi za binadamu.

Hili limewekwa wazi katika Katiba na imeridhia bila ya shinikizo la mikataba ya kimataifa na kuanzishwa kwa mahakama za kimataifa. Katika kuonyesha ushirikiano wake mkubwa kwa masuala haya, ilikubali Arusha kuwa na Mahakama ya Kimataifa iliyowahukumu na kuwafunga watu kadhaa waliodaiwa kuhusika na mauaji ya halaiki ya Rwanda.

Hapo hapo Arusha pia ndipo makao makuu ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binamamu na kiongozi wake wa hivi sasa ni Mtanzania, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani.

Vile vile, Tanzania ni moja ya nchi 124 zilizotia saini na kuridhia kuwamo kwa Mahakama ya The Hague. Tulitia saini mkataba wa kuikubali mahakama hiyo Desemba 29, 2000, tukauridhia Agosti 20, 2002 na kuukubali kutuhusisha katika shughuli zake Novemba Mosi, 2002.

Hatua hizi tatu zilikuwa kielelezo cha kujiamini kwamba tunaposema tunaheshimu maisha ya watu na haki za binadamu tunazungumza hivyo siyo mdomoni tu, bali kutoka moyoni.

Uamuzi wa Tanzania ulikuwa kielezo cha kupevuka katika masuala ya utawala wa haki na sheria ambapo huwa hapana kinga ya mtu kuweza kushtaki au kushtakiwa.

Mahakama mbili za Arusha, moja iliyowashughulikia waliotuhumiwa kuhusika kwa njia moja au nyingine na mauaji ya Rwanda na ile ya Afrika zimekuwa zikifanya kazi zake sambamba na ile ya The Hague.

Tumeona viongozi wa nchi mbalimbali na wa dini, wanasiasa na watu wa kawaida wakifikishwa katika mahakama hizi tatu na katika baadhi ya kesi, hasa zile zilizofanyika Arusha tumesaidia kutoa huduma kuhakikisha zinafanya kazi zilizopelekea kuanzishwa kwake.

CUF yatua The Hague

Sasa nchi yetu imepata jaribio la baadhi ya watu wetu kufikishwa katika mahakama ya The Hague na walioasilisha madai ni Chama cha CUF.

Sina uwezo na sina haki ya kusema madai haya ni kweli au ya kinafiki. Ni mahakama ndiyo huamua je, mlalamikaji amewasilisha madai ya kweli au ya ubunifu kupaka matope hao aliodai kuhusika na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Kinachonishangaza ni kusikia kelele za lawama kwa hatua iliyochukuliwa na CUF na wapo wanaodai kwa kufanya hivyo viongozi wake wanafanya uchochezi na kuipaka nchi matope katika macho ya jumuiya ya kimataifa.

Nionavyo mimi hii ni nafasi nzuri kwa uongozi wa Tanzania ambao kumbukumbu zinaonyesha kujali maisha ya watu na kuheshimu haki za binadamu kujisafisha zaidi hapa nyumbani na nje.

Kwa kawaida mtu ambaye hakutenda ubaya huwa hana wasiwasi wa kushtakiwa na huona anapopata nafasi ya kujibu shutuma ndiyo anapata kuthibitisha huyo anayelalamika ni mnafiki na mzandiki.

Katika utawala bora mtuhumiwa huwa hana hatia mpaka mahakama imwone hivyo kutokana na ushahidi au uwongo uliowasilishwa mahakamani.

Sasa kama madai ya CUF inayodai kuwa na vielelezo si ya kweli, kama wengi tunavyoamini, kwa nini pawapo hofu na shaka kwa hatua ya kwenda The Hague?

Katika hali ya kawaida ni vigumu kuwa na vithibitsho vya mtu kufanya kosa, kama la kupiga watu ovyo au kuuawa, kama mambo hayo hayajatendeka.

Labda hiyo mahakama iwe ya kuigiza na siyo yenye mahakimu wa kweli na uadilifu tuliotarajia hata tukaweka wino wa kukubali kuanzishwa kwake na kuridhia ifanye kazi.

Tumeona katika mahakama ya mauaji ya halaiki ya Rwanda na hata ya The Hague siyo kila aliyefikishwa mahakamani amepatikana na hatia.

Watu mbalimbali, wakiwamo viongozi mashuhuri wamesafishwa majina yao na waliokuwa wakipeperusha bendera za kudai walihusika na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu wamepelekwa na kupoteza heshima ya kuwa watu wa kweli katika jamii na jumuiya ya kimataifa.