Ulanzi, kinywaji pori chanzo cha neema na migogoro ya kijamii

Muktasari:

  • Pembezoni mwa Barabara ya Tanzam kijijini Tanangozi, kitongoji cha Kilindi baiskeli, magari, pikipiki zimeegeshwa kusubiri na kupakia bidhaa hii pendwa kwa baadhi ya watu msimu wa masika.

Ni asubuhi kila ninayemwona barabarani ameshika ndoo ya plastiki ya lita 20, kila mmoja anasogea kituoni kukabidhi mzigo wake kwa mnunuzi wa jumla wa ulanzi.

Pembezoni mwa Barabara ya Tanzam kijijini Tanangozi, kitongoji cha Kilindi baiskeli, magari, pikipiki zimeegeshwa kusubiri na kupakia bidhaa hii pendwa kwa baadhi ya watu msimu wa masika.

Ulanzi ni kinywaji kinachotokana na mmea wa muanzi unaotoa majimaji kama utomvu wa mpira lakini hiki ni kimiminika laini kama maji ya kunywa chenye ladha ya utamu.

Maji haya yanakusanywa kutoka katika mti wa muanzi kwa kutumia kifaa maaalum kama chupa kinachoitwa mbeta. Ugemaji wake ni mara tatu kwa siku, asubuhi ambapo ulanzi unaondolewa kutoka kwenye mbeta na kuwekwa kwenye maplastiki ya ujazo wa lita 20 au ndoo ndogo ndogo.

Mchana ni kugema au kupyatila kama inavyojulikana ambapo mmea huu unakatwa kidogo kwenye ncha ya juu pasipo kutoa ulanzi kutoka katika mbeta na hatimaye jioni mgemaji anatoa ulanzi kama zoezi la asubuhi.

“Huu ni msimu wa neema, wakati huu kila unayekutana naye kijijini ana uso wa bashasha na anaonyesha hana wasiwasi na maisha yake,” anasema mwanakijiji anayejitambulisha kwa jina moja la Mwarabu.

Mwarabu anasema ulanzi unanywewa na watu wengi Iringa, wapo wasiopenda kujulikana kuwa wanakunywa, hivyo wanapelekewa nyumbani moja kwa moja.

Kwa miaka takriban 10 sasa, Mwarabu anasafirisha ulanzi kwa baiskeli kutoka Tanangozi kwenda Iringa mjini umbali wa kilomita 28.

Ni biashara inayohusisha wanawake na wanaume ingawa kwa sehemu kubwa wanaume ndiyo wagemaji na wanawake ni wabebaji wa kupeleka kwa wanunuzi barabarani.

Mzee Titus Mwegelingoha anasema magari yamekuwa yakisafirisha ulanzi toka miaka ya mwanzo ya 1960, baadaye baiskeli na sasa bodaboda nazo zimeingia kazini.

Mianzi ilifikaje Tanangozi?

Mwegelingoha anasema mimea ya mianzi ilifikishwa Tanangozi mara ya kwanza na watu wa kabila la Wabena waliokuwa wakitoka Njombe waliokuwa wakisafiri kwenda Tanga na Kilosa kwenye mashamba ya mkonge.

‘Hawa hawakuwa na nia ya kutuachia mianzi hapa ilitokea bahati mbaya tu, mmoja wao alikuwa anaumwa na kwa wakati huo kulikuwa na mzee mmoja aliyejulikana kama Gonelamenda Mwakinyamagoha ambaye naye alikuwa ametokea huko huko Njombe na wenzie walikuwa wakifikia kwake walipokuwa wakisafiri kuelekea Tanga na Kilosa hivyo aliwashauri kuwa haikuwa vizuri kusafiri na mizigo huku wakiwa na mgonjwa, walikubaliana naye na mianzi ile wakaiacha kwake.’’

Mwegolingoha anasema walipokubaliana na ushauri wake yeye akachukua mianzi ile na kuanza kupanda maeneo karibu na kwake. Siku hizo kulikuwa hakuna magari, wasafiri wengi walitembea kwa miguu.

Mwegolingoha anasema kuwa nia yao ilikuwa kwenda kupanda huko Tanga na Kilosa ambako walikuwa wakitarajia kuanzisha maisha mapya katika maeneo mapya kwa sababu walikuwa wamezowea kunywa walipokuwa huko Njombe.

Kwa hiyo ulanzi ule ulipofikia hatua ya kuzaa na kutoa mimea mipya, Mwakinyamagoha alianza kugema na watu wengine walipoonja wakaona ni kinywaji kitamu, wakaomba kwenda kupanda katika maeneo yao na hivyo ukasambaa eneo kubwa la kijiji cha Tanangozi na vitongoji vyake.

“Hii ilikuwa mimea ya porini kama ilivyo mianzi na miti mingine lakini Wabena waligundua kuwa ni kinywaji baada ya kuona mianzi ikiwa michanga ikiliwa na panya inatoa maji maji na walipoonja yale maji na utamu wake wakaona ni kinywaji na kuanza kugema,’’ anasema Mzee Mwegelingoha ambaye na yeye anagema ulanzi ambao amerithishwa na baba yake. Ulanzi mwingi unatoka maeneo ya pembezoni kama Mgama, Makete na Mlenge.

Anasema ulanzi umekuwa mwajiri na msitiri wa maisha ya watu kwa kipindi cha nusu mwaka toka unapoanza kuota mwezi Novemba hadi unapokauka Mei mwishoni kwa baadhi ya maeneo lakini yapo maeneo ambayo ulanzi unakuwepo kwa kipindi cha karibu mwaka mzima kutokana na matunzo ambayo wagemaji wa maeneo hayo wanatoa kwa mimea hii.

Kuhifadhi ulanzi

Anasema ulanzi unaweza kuhifadhiwa kwa kipindi cha mwaka mzima kwa kutumia njia ya asili ambayo ni kuchuja kwa kuondoa lile povu mpaka liishe na kubaki maji maji pekee na baadaye kuweka kwenye mtungi na kufunika vizuri.

Mtungi huu unatumbukizwa ardhini na kufukiwa, ulanzi utabaki na ladha ile ile ya siku ya kwanza lakini utakuwa na nguvu ya ajabu kwa anayekunywa kwa sababu kiasi kidogo tu atakuwa amelewa kama hana uzoefu na kinywaji hicho.

Anasema hadi sasa hakuna njia ya kisasa ya kuhifadhi kinywaji hiki kwani miaka ya nyuma aliwahi kutembelewa na vijana waliokuwa na nia ya kujaribu kuhifadhi katika chupa za kioo au plastiki lakini hawakurudi tena na inavyoonekana walishindwa kupata ule utaalamu ambao ungeweza kuhifadhi kinywaji hiki kiweze kutumika wakati wa kiangazi kwa sababu wakati wa msimu maelfu ya lita za ulanzi yanamwagwa kwa kukosa wateja na kwa vile hakuna uhamasishaji unaofanyika ili kuwavuta watu wengine wa mikoa mbalimbali waweze kupenda na kunywa.

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Makete miaka ya 1970 hadi 1990 mwanzoni, Tuntemeke Sanga aliwahi kushauri bungeni zitafutwe mbinu za kuhifadhi ulanzi.

Anasema wenyeji wa Iringa na eneo dogo la Dodoma bado hawapati mapato ya kutosha kutokana na kazi ngumu wanayofanya kwa sababu mgemaji wa ulanzi mara nyingi hawezi kufanya shughuli za kilimo vizuri kwa sababu muda mwingi wa siku unatumika kuhudumia kinywaji hicho.

‘Unaanza kugema saa 11 asubuhi, unamaliza saa mbili hadi unamkabidhi mnunuzi ni karibu saa nne na ikifika saa tano asubuhi unarudi kupyatila (ugemaji wa mchana) na jioni saa kumi unarudi tena kugema, siku imekwisha,’’ anasema Mwegolingoha kwa masikitiko kidogo.

Anasema vijana wengi kwa sasa hawavutiwi na kazi ya ulanzi, wanaona wakitumia muda mfupi kwa siku kwa vibarua vya kulima na kupalilia mashamba, wanapata fedha nyingi kuliko kutegemea ulanzi na hivyo baadhi ya mianzi iliyoachwa na wazee ikiwa mapori.

Anasema ulanzi wa hadi lita 100 unaweza kupatikana kwa siku katika eneo la eka moja. Kwa sasa lita 20 za ulanzi zinauzwa kwa bei ya Sh 3,000.

Shukuru Aloyce, mkazi wa Kilindi, anasema ana watoto watano, mmoja anasoma sekondari na waliobaki shule ya msingi, anawatimizia mahitaji yao kama viatu, sare za shule na mengineyo kila mwaka kwa kugema na kuuza ulanzi.

‘Ulanzi umekuwa mkombozi kwangu kwa sababu hata kilimo ninachoendesha nategemea mtaji wa mapato ya ulanzi, naweza kununua mbolea, kulipa vibarua wa kulima na kupalilia kutokana na akiba ambayo nimeweka kwa kuuza ulanzi wakati wa masika.’’ Anasema Shukuru, mmoja wa wanawake wachache ambao wamefanya ugemaji ulanzi kama shughuli ya ujasiriamali wa kudumu.

Anaendelea kusema kuwa wapo wagemaji wengine ambao kila mwaka wananunua ng’ombe na wanyama wadogo kama mbuzi na kondoo.

Hata hivyo anasema mwaka huu umebei si nzuri kwa sababu wanywaji wakubwa wa ulanzi wako Mtera mkoani Dodoma ambako wavuvi wanasema hawapati samaki wengi hivyo hakuna ujio wa watu wa mikoa mingine wanaokwenda kununua samaki huko.

Kwa bei ya huko, ndoo ya lita 20 hununuliwa kwa Sh6,000 lakini mwaka huu imeshuka hadi Sh 3,000 na hivyo kuna baadhi ya wanunuzi hawafiki kijijini kununua ulanzi.

Mohamed Mbugi, mnunuzi na msambazaji ulanzi kwa miaka 29 sasa, anasema kumekuwa na manufaa makubwa kwake kimaisha tangu alipoanza kazi hii.

“Nilianza kusafirisha lita 60 kwa siku nikitumia baiskeli kwenda Iringa mjini, baadaye nikawa nakodi gari na leo nina gari langu ninalotumia kusafirisha ulanzi kwenda Dodoma ambako nina wateja wa kudumu, hivyo nimepiga hatua.’’ Kwa sasa anasafirisha lita 8,000 kwa siku.

Anasema wapo wasambazaji wengine wanaojaribu kuanzisha masoko mapya maeneo ya Mlandizi na Ilula wilayani Kilolo mkoani Iringa na Mikumi na Kilombero mkoani Morogoro.

Mbugi amefanikiwa kujenga nyumba katika kijiji cha Mlandege, ambayo ameipangisha. Pia ana viwanja na mashamba ambayo amenunua kwa pato la ulanzi, anaongeza kuwa ana watoto 16, wengine wamesoma na wapo wanaosoma na wote anamudu kuwapatia mahitaji muhimu.

Exaud Mwakitosi ambaye ni mzoefu wa biashara hii anasema ulanzi upo katika madaraja matatu; mwepesi wenye ladha kama sukari (mtogwa) ambao haupendwi sana na wanywaji wazoefu kwa sababu unalewesha mapema lakini inadhaniwa kuwa ni dawa ya kusafisha tumbo, huu unapendelewa sana na wale wanaoanza kutumia kinywaji hiki, upo wa ladha ya kati ambao si mkali wala mtogwa, huu unapendelewa na wale wasio wazoefu na wa mwisho ni ule mchungu unaoitwa mkangafu, huu ni kwa wazoefu wanaotaka kunywa mwingi kwa sababu licha ya uchungu lakini hauleweshi mapema.

Ulanzi na migogoro ya kijamii

Robert Lawa, Diwani wa Kata ya Mseke anasema msimu wa ulanzi ni wa neema kwa wakazi wa eneo lake kwa sababu wananchi wanakuwa na uwezo kifedha na hata michango mbalimbali ya kuendesha shughuli za kimaendeleo kama za ujenzi wa madarasa au zahanati inakuwa rahisi kupata wakati huu.

Hata hivyo anasema licha ya ulanzi kuonekana chanzo cha neema kwa kuwaingizia wananchi kipato lakini wakati wa ulanzi kunakuwa na matatizo ya kijamii kwani huu ni wakati wa mizozo mingi ya kifamilia na hata ugomvi wa mtu mmoja mmoja.

Anasema ndoa nyingi huwa kwenye matatizo kwa sababu watu wanakuwa na fedha na wengine kuamua kuingia kwenye mahusiano mapya au michepuko kwa sababu tu wana fedha.

“Huu ni wakati wa mimba nyingi zisizotarajiwa na kutelekezana kwa wanandoa,’’ anasema Diwani Lawa.

Ulanzi unapatikana kwa wingi mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma na Mbeya.

[email protected], 0783165487