Umeme kizungumkuti Wizara ya Nishati na Madini

Muktasari:

Mwaka mmoja baada ya kuteuliwa kuwa mbunge kisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhungo aliwahi kukaririwa akisema baada ya muda, Tanzania itajitegemea kwa nishati ya umeme.

Kutoka kuwa na mpango wa kuzalisha umeme wa kukidhi mahitaji ya ndani hata kuuza nje ya nchi, Serikali inapanga kununua megawati 400 kutoka Ethiopia.

Mwaka mmoja baada ya kuteuliwa kuwa mbunge kisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhungo aliwahi kukaririwa akisema baada ya muda, Tanzania itajitegemea kwa nishati ya umeme.

Profesa Muhongo aliyeteuliwa mwaka 2012 aliyasema hayo Julai 2013 na kubainisha kwamba, mapinduzi yanayotazamiwa kufanyika kwenye sekta ya nishati na madini ikiwamo mradi wa uzalishaji umeme wa Kinyerezi, itakuwa suluhu ya kudumu ya uhaba wa umeme nchini.

“Mipango yetu ifikapo mwaka 2014, tayari tutakuwa na umeme wa ziada wa megawati 500 ambao tutauuza nje ya nchi,” alisema Profesa Muhongo.

Kutekeleza lengo hilo, alisema Serikali imebainisha maeneo inayotazamia kuyawekea mkazo kuzalisha umeme wa kutosha na kuyataja kuwa ni uendelezwaji wa gesi asilia kutoka mkoani Mtwara na utumiaji wa makaa ya mawe. Pia, alisema Serikali inakusudia kuimarisha vyanzo vya umeme kutokana na upepo, jua na maji.

Alyasema hayo wakati wa kusainiwa kwa makubaliano ya maelewano baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya China Power Investment (CPI).

“Ili kufanikisha lengo la kukuza uchumi, inatupasa kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika… tunakadiria ifikapo mwaka 2015 tutakuwa na umeme wa ziada, hatua itakayotufanya tuuze kiwango kikubwa,” alisema.

Alisema kutokana na mipango iliyoandaliwa, umeme utachukuliwa kama bidhaa ambayo itatafutiwa masoko nje na kuuzwa. Aliyasema hayo wakati Tanesco ikiingia makubaliano na CPI kuendeleza mradi wa Kinyerezi, uliokuwa katika hatua ya tatu kati ya nne ukitarajiwa kuzalisha megawati 600.

Kununua

Siku hazigandi, mpango uliotarajiwa kukamilika ndani ya uongozi wa Serikali ya awamu ya nne haujatimia na miaka miwili baadaye, msimamo mpya umetolewa, Serikali itanunua megawati 400 kutoka nchini Ethiopia.

Mabadiliko haya yanaelezwa baada ya matazamio kuonyesha ongezeko la mahitaji ya ndani na kubainishwa kwa vyanzo vya kukabiliana na ongezeko hilo. Wakati Serikali ikisisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda, ndoto ya kujitegemea kwa nishati hiyo bado haijatimia.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka anasema makubaliano ya kununua umeme wa bei nafuu kutoka Ethiopia, utasaidia kukidhi mahitaji nchini na kufanikisha Tanzania ya viwanda.

Dk Mwinuka anasema mahitaji ya umeme nchini yanapanda kila siku kutokana kuongezeka kwa watu na utekelezaji wa sera ya viwanda, hivyo umeme huo ni muhimu.

“Utatusaidia sana kwa sababu uwezo wetu kwa sasa ni kuzalisha megawati 1,400, ila baada ya kukamilika mradi wa Kinyerezi awamu ya kwanza na ya pili zitaongezeka megawati 425 na tukiongeza tutakaonunua kutoka Ethiopia, tutakuwa na zaidi ya megawati 2,000 ambao utatosheleza mahitaji,” anasema Dk Mwinuka.

Anasema Ethiopia ina umeme mwingi nafuu unaozalishwa kutokana na maji ambao uwekezaji wake ni wa gharama ndogo, tofauti na gesi au mafuta uwekezaji wake ni nafuu lakini umeme wake ni ghali.

“Umeme wetu wa maji ni Sh80 kwa uniti moja lakini wa vyanzo vingine bei yake zipo juu,” anasema Dk Mwinuka.

Pia, anasema kuna vyanzo vingi vya umeme wa maji nchini lakini vinazalisha kidogo tofauti na Ethiopia ambako wanavyo vichache vyenye uwezo wa kuzalisha nishati hiyo nyingi, kwani haitakuwa gharama kubwa kuununua kwani tayari umefika nchini Kenya hivyo utaunganishiwa Namanga.

Kwa maoni ya Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benedict Mongula anasema japo hafahamu uhalisia wa mpango wa kuuza na kununua umeme nchini, anadhani mikakati iliyowekwa kuuza umeme nje imeshindikana.

“Mikakati ya nchi ni kuzalisha umeme wa uhakika ila wa bei nafuu. Sijui kwa nini mpango umebadilika kutoka kuuza mpaka kununua. Huenda mahitaji yameongezeka kutokana na sera ya uchumi wa viwanda,” anasema Profesa Mongula.

Anasema kama umeme unaozalishwa hautoshi lazima kutafuta vyanzo vingine, ikiwamo kununua kutoka nje au wawekezaji wa ndani na kutahadharisha kuwapo umakini ili kutokuwapo kwa mikataba mibovu.

Mipango

Kwenye mkutano wa nchi zinazounda Umoja wa Ushirikiano wa Masuala ya Umeme (EAPP), uliofanyika Januari, zilikubaliana kuuziana umeme ili kuongeza uhakika upatikanaji na kuchangia maendeleo.

Mwenyekiti wa mkutano huo wa 12 wa Baraza la Mawaziri kutoka EAPP, Profesa Muhongo alisema muda wa kuuziana umeme nafuu umefika ili kuondokana na utokanao na mafuta ambao ni ghali.

Kufanikisha kuuziana nishati hiyo, Waziri Muhongo alisema upo mkakati wa kujenga mradi wa kilovoti 400 za umeme kutoka Tanzania hadi Kenya na kilovoti 400 kutoka Zambia hadi Tanzania. Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutahakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Mpaka sasa Tanzania inanunua umeme kutoka nchi jirani. Licha ya megawati 400 zinazotarajiwa kutoka Ethiopia, Profesa Muhongo anasema tunanunua megawati 17 kutoka Uganda, megawati nne kutoka Zambia na megawati moja Kenya.

Anasema Tanzania itaendelea kununua umeme kutoka nje ya nchi ili kukidhi mahitaji na badala ya kununua umeme wa mafuta unaozalishwa nchini ni bora kufanya hivyo kutoka, Uganda, Ethiopia au kwingineko ambako ni nafuu.

Wanachama wa EAPP wanajumuisha Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Ethiopia, Djibout, Libya na Misri.

Wadau

Mhadhiri wa uchumi wa UDSM, Profesa Hamphrey Moshi anasema kununua umeme kutoka Ethiopia haina madhara yoyote bali ni mhimu kwa kuwa nchi inafanya mapinduzi ya viwanda ambayo yanaihitaji nishati hiyo kwa wingi na uhakika.

“Ethiopia ni majirani zetu, wapo vizuri katika uzalishaji wa umeme nafuu. Nchi yetu inahitaji umeme mwingi na wa uhakika. Si jambo la ajabu nchi kununua umeme kutoka nje na kutoa mfano Zambia wanatumia umeme wanafanya hivyo kutoka Afrika Kusini,” anasema Moshi.

Dk Jehovaness Aikaeli wa chuo hicho pia anasema ushirikiano huo ni mzuri katika uhusiano wa kimataifa lakini unapaswa kufanywa katika mambo ambayo hakuna namna ya kukabiliana nayo zaidi ya kufanya hivyo na siyo changamoto ambazo zinahitaji uthubutu kutatuliwa.

“Kufundishwa riadha na Waethiopia ni sawa kwa kuwa wao wamefanikiwa zaidi kuliko sisi lakini suala la umeme hatukutakiwa kuwaza kununua kutoka nje bali kutumia vyanzo vyetu kuzalisha kwwa kutumia rasilimali kama gesi, makaa ya mawe na maporomoko ya maji tuliyonayo,” anasema Dk Aikaeli.