Unajua sababu ya matunda kudondoka machanga?

Miti kudondosha matunda ni jambo la kawaida endapo itapandwa katika ardhi isiyokuwa na virutubisho sahihi.

Muktasari:

KWA UFUPI
Ardhi ikiwa na  kiwango kidogo cha magneziamu (Mg),  pia ikiwa na kiwango cha juu cha Potasiam (K) na Boroni (B). Hivyo  kabla hujaandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha matunda ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya udongo ili upate uhakika wa kujua unachotaka kukipanda.

Kuna wakati  miti ya matunda kama miembe, mipapai,  miparachichi na mingine,  hudondosha matunda wakati yakiwa bado machanga,  kitendo ambacho ni hasara kwa wakulima.

 Baadhi ya miti hiyo huanza kudondosha matunda muda mfupi baada ya kuanza kuzaa na hii hutokea baada ya maua kujitenga na tunda.

Hii imekuwa changamoto kubwa kwa wakulima na wengi wamekuwa wakiulizia kuhusu kadhia hii.

Ili kuliweka sawa jambo hili, leo  tutaongelea miti ya  miembe, mipapai na parachichi .

Kwa upande wa miembe, kuna sababu lukuki zinazoweza kusababisha mti kupukutisha matunda ambayo hayajakomaa.

Miongoni mwa  sababu hizo ni pamoja na hali ya hewa au mvua kuzidi, magonjwa ya mmea, wadudu au uhaba wa rutuba na mbolea. Pia uwekaji mbolea ya kukuzia katika kipindi kisichotakiwa.

Mti wa mwembe unapaswa kupata kiwango stahiki cha maji katika ukuzaji. Epuka kumwagilia kiasi kikubwa cha maji kwa kufikiri unafanya vizuri kwani hiyo inaweza kusababisha mti kudondosha matunda yakiwa machanga. Kumbuka kuwa  miti ya miembe iliyokomaa haihitaji maji wakati wote.

Mwembe mdogo unahitaji kumwagiliwa maji ya kutosha mara mbili tu kwa  wiki kwa kipindi cha mwaka mmoja na baada ya hapo ni mara 1 kwa siku nne  au tano.

Kwa kawaida miti ya miembe hukua na kuzaa vizuri katika mazingira ya uoto wa kitropiki, mazingira ambayo kwa kawaida licha ya kupata mvua hayana baridi sana. Hata hivyo, mti wa mwembe uliokomaa unaweza kustahimili mazingira yaliyo na joto kidogo.

Nini ufanye? Weka uzio kwenye mti wako, yaweza kuwa matawi au mifuko ili kuulinda mti dhidi ya upukutishaji majani. Usiondoe majani wala matawi yaliyoanza kunyauka acha yadondoke yenyewe.

Matunda yakiwa madogo  yanaweza kushindwa kustahimili kukua endapo hali ya hewa itabadilika kutoka joto kuwa baridi. Baridi huathiri kiini cha embe katika mbegu hali ambayo husababisha tunda kuzalisha aina fulani ya gesi (ethylene) ambayo husababisha tunda kudondoka kabla ya wakati wake.

Kumbuka mbolea ikizidi au ikipungua inaweza kusababisha mti kudondosha matunda yake, hivyo ni vyema kuhakikisha unafuata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuweka mbolea.

Unashauriwa kutumuia mbolea iliyo na virutubisho na kuthibitishwa kitaalamu kwa ajili ya miti ya matunda na iliyo na kiwango sahihi cha naitrojeni (N), Fosiforas (phosphorous P) na Potasiam (K). Kwa pamoja madini haya  huufanya mmea kupata virutubisho muhimu.

Muhimu

Zingatia sana katika uchaguzi wa aina ya mbolea; chagua mbolea ambayo ina kiwango kikubwa cha P na K ukichagua mbolea ilio na kiwango kikubwa cha  Nitrojeni (N), hii inaweza kuharibu maua.

Unaweza pia kutumia mbolea ya mabaki ya mimea na wanyama katika kukuza miti yako.

Aidha, uongezaji mbolea kiholela pia unaweza kuathiri mmea.

Ni muhimu kuzingatia sababu zinazosababisha mti kudondosha matunda kabla hayajakomaa, kwani matunda yanapodondoka huchochea mti kuzalisha kemikali ya ethylene ambayo husababisha matunda mengine kuendelea kudondoka.

virutubisho vya mti na aina ya udongo

Miti kudondosha matunda ni jambo la kawaida endapo itapandwa katika ardhi isiyokuwa na virutubisho sahihi.

Mfano mzuri wa hali hii ni pale ardhi ikiwa na  kiwango kidogo cha magneziamu (Mg),  pia ikiwa na kiwango cha juu cha potasiam (K) na Boroni (B). Hivyo  kabla hujaandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha matunda, ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya udongo ili upate uhakika wa kujua unachotaka kukipanda.

Kujua sifa za udongo wako na virutubisho vilivyopo au vinavyokosekana, mkulima anatakiwa kupima udongo wake, jambo linalofanywa na wataalamu au hata wakulima wenye maarifa ya upimaji kwa kutumia kifaa maalumu.

Miti ya mipapai

Kwa papai, mti hudondosha matunda kabla ya kukomaa endapo maua yake hayajachavushwa. Kumbuka ili tunda liweze kupatikana, ni lazima ua lake lichavushwe. Hivyo hakikisha unakuwa na miti zaidi ya mmoja ili kuwezesha zoezi la uchavushaji kuwa la mafanikio.

Miti ya parachichi

Kuhusu parachichi, tatizo kubwa la matunda  kuharibika kabla ya wakati, ni utando wa buibui ambao unaweza kudhibitiwa kwa mkulima kupuliza dawa kitaalamu, kumwagilia miti  sambamba  na kuondoa matawi yaliyonyauka na kukauka. Ni  muhimu kuhakikisha utoaji wa matawi unaenda sambamba na usafi wa shamba na kuondoa majani na vichaka.

Makala haya awali yalichapishwa katika Gazeti la Monitor la Uganda.