Usalama migodini muhimu, utiliwe maanani

Muktasari:

Januari 25, mwaka huu, kulitokea ajali ya kufukiwa na kifusi kwa wachimbaji 15 wa mgodi wa dhahabu RZ ulioko eneo la Nyarugusu mkoani Geita.

Usalama mahala pa kazi ni suala la kisheria linalolenga kulinda masilahi ya mfanyakazi kwa upande mmoja na mwajiri kwa upande mwingine.

Januari 25, mwaka huu, kulitokea ajali ya kufukiwa na kifusi kwa wachimbaji 15 wa mgodi wa dhahabu RZ ulioko eneo la Nyarugusu mkoani Geita.

Katika mgodi huo unaomilikiwa na wawekezaji kutoka China, wachimbaji wadogo 15 walifukiwa na kifusi cha udongo na kukaa ndani kwa siku nne.

Baada ya juhudi za siku nne mchana na usiku wachimbaji wote 14 raia wa Tanzania na mmoja Mchina waliokolewa. Hii ni baada ya shughuli za uokoaji kufanyika kwa kutumia zana za kisasa za uchimbaji kutoka migodi mikubwa iliyopo jirani pamoja na juhudi binafsi za wachimbaji wadogo waliotumia mbinu na uzoefu wao wa asili kuokoa maisha ya wenzao.

Pamoja na wachimbaji wote kuokolewa, kasoro kadhaa zilibainika ambazo ni lazima zifanyiwe kazi kuepusha maafa makubwa siku zijazo.

Mgodi kukosa ramani

Shughuli za uokoaji ingawa zilifanikiwa, lakini haikuwa kazi rahisi kutokana na mgodi huo kutokuwa na ramani ya kuonyesha njia kuanzia kuingia mgodini hadi eneo walipofunikwa.

Ilibidi waokoaji wafanye kazi kwa kubahatisha hadi walipofanikiwa kubaini walipo.

Kwa mujibu wa kanuni ya 36 hadi 40 ya sheria ya madini, kila kampuni au mgodi inapaswa kukaguliwa na mamlaka husika kuhakikisha usalama na afya kazini pamoja na utunzani wa mazingira.

Mchoro na ramani kuonyesha hatua, njia na maeneo yote ya mgodi ndani na nje ni kati ya mambo muhimu yanayosisitizwa kwenye kanuni hizi. Lengo mojawapo ni kurahisisha shughuli za uokoaji pale ajali inapotokea lakini hili halikufanyika.

Ushahidi uliopatikana katika mgodi wa RZ baada ya ajali kutokea umedhihirisha kuwa kanuni hiyo haikuzingatiwa na hakuna mtu aliyewajibishwa.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba hata nguzo za miti zilizotumika kushikilia udongo mgodini zilibainika kuoza na inawezekana ikawa ni miongoni mwa sababu za ajali hiyo iliyotishia maisha na usalama wa wachimbaji waliofukiwa na kusababisha taharuki kubwa.

Maofisa madini kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na Kanda ya Ziwa hawakutimiza wajibu na majukumu yao ipasavyo. Wataalam na watendaji wenye dhamana ya kusimamia usalama na afya kazini waliruhusu au hawakuzuia shughuli za uchimbaji kuendelea bila kuzingatia usalama na afya za wachimbaji chini ya ardhi.

Swali la kujiuliza ni je, wakaguzi wanaotembelea migodi na kukagua usalama wamewahi kukagua mgodi wa RZ?

Kama walikagua hawakuona nguzo zilivyooza huku mgodi huo ukiwa hauna ramani kuonyesha maeneo ya uchimbaji?

Sina uhakika, lakini napata hisia kwamba yawezekana makosa kama haya hayapo kwenye mgodi wa RZ pekee, bali katika migodi mingine maeneo mbalimbali nchini.

Tayari Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Merdard Kalemani aliagiza kusimamishwa kwa shughuli katika mgodi huo kupisha uchunguzi.

Pamoja na kuagiza uchunguzi, Dk Kalemani pia ameagiza mkaguzi aliyekugua na kuruhusu mgodi huo ahojiwe na kuwajibishwa kwa kutotimiza wajibu.

Nadhani muda umefika kwa ukaguzi wa kina kufanyika kwenye migodi yote nchini, hasa yale yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo na wa kati ili kujiridhisha na usalama na afya ya wachimbaji.

Ukaguzi huu unaweza kufanyika hata kwenye migodi mikubwa kutokana na ukweli kwamba binadamu tuna tabia ya kupuuza au kuzembea kufuata taratibu za kisheria kama tulivyoshuhudia kwenye tukio la moja ya migodi mikubwa nchini kubainika kutokuwa na choo kwa ajili ya wachimbaji wanaokuwa na shifti za zaidi ya saa sita chini ya ardhi.

Kampuni hiyo ilipigwa faini ya Sh10 milioni na Baraza la Taifa Usimamisi wa Mazingira (Nemc) na kuamriwa kurekebisha kasoro hiyo.

Wakati tukimshukuru Mungu kwa kuwaokoa wachimbaji wote wa mgodi wa RZ, ni vyema tukazingatia usemi wa wahenga wa kuziba ufa kuepuka kujenga ukuta.

Kila mwenye dhamana ya kusimamia sheria ya usalama migodini na atomize wajibu wake bila kusukumwa wala kusimamiwa.

Wizara ya Nishati na Madini kupitia kwa maofisa na wataalam wake walioenena maeneo yote iliko migodi wasingoje hadi maafa mengine yatokee ndipo ukaguzi ufanyike. Hapana! Tujenge utaratibu wa kukagua migodi mara kwa mara kulinda maisha ya wachimbaji.

Muda wa wataalamu kushinda maofisini kwenye viyoyozi umepita. Waende migodini kufanya ukaguzi kulinda afya na usalama wa Watanzania pamoja na mazingira.

Rehema Matowo ni Mwandishi wa gazeti hili Mkoa wa Geita, anapatikana kupitia 0756 91 96 91.