Utafiti wabaini tishio la kuwa na mikoa ya wasomi na isiyo na wasomi

Muktasari:

  • Wakati mikoa hiyo ikifaulisha kwa kiwango cha juu, ipo ambayo hushikilia mkia, sio kwa mara moja bali ni kila wakati.

Kila yanapotangazwa matokeo ya mitihani ya ngazi mbalimbali nchini, huwa ipo mikoa vinara wa ufaulishaji.

Wakati mikoa hiyo ikifaulisha kwa kiwango cha juu, ipo ambayo hushikilia mkia, sio kwa mara moja bali ni kila wakati.

Mwaka 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilazimika kuziagiza Wizara wa Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwenda mkoani Mtwara kuchunguza sababu za mkoa huo kufelisha wanafunzi wengi.

Mkoa huo katika matokeo ya kidato cha pili 2016, kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zilitoka huko na moja Tanga.

Hali hii ndiyo iliyoifanya shirika la Twaweza kufanya utafiti kujua kinachosababisha kuwapo kwa tabaka kati ya maeneo yanayoongoza na inayoshikilia mkia.

Twaweza wanasema ipo hatari ya kuwapo kwa mikoa ya wasomi na ile isiyo wa wasomi ikiwa tabaka hilo litaendelea kuwapo.

Wakati mikoa mingine ikiwa na miundombinu inayochangia kuwapo kwa ufaulu, ipo inayohaha kwa kukosa miundombinu ikiwamo umeme, maji, vifaa vya kufundishia, kujifunzia na uhaba wa walimu.

Akisoma matokeo ya utafiti huo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema asilimia 38 ya wanafunzi wenye umri wa miaka kati ya tisa na 13 nchini hawawezi kufanya majaribio ya darasa la pili.

Anasema utafiti huo uliowahusisha wanafunzi 197,451 kutoka katika shule za msingi 4,750, unaonyesha kwamba wilaya ya Iringa Mjini inaongoza kwa ufaulu wa asilimia 75 katika majaribio ya kusoma Kiingereza, Kiswahili na hesabu rahisi wakati wilaya ya Sikonge ilifanya vibaya kwa asilimia 17.

INAENDELEA UK 14

INATOKA UK 13

Eyakuze anasema asilimia 42 ya watoto kutoka katika kaya maskini walifaulu majaribio ikilinganishwa na asilimia 58 ya watoto kutoka katika kaya zenye uwezo.

Anasema asilimia 74 ya watoto watatu kati ya wanne ambao mama zao wana elimu ya sekondari au elimu ya juu walifaulu majaribio yote matatu ikilinganishwa na asilimia 46 ya watoto ambao mama zao hawakusoma.

“Asilimia 64 ya watoto mkoani Dar es Salaam wenye miaka tisa hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio yote matatu, lakini mkoani Katavi, ni asilimia 23 tu ya watoto wanaoweza kufaulu majaribio hayo,” anasema.

Wakati katika utafiti huo, watoto wawili kati ya 10 (asilimia 16) wenye umri wa miaka 11 wako nyuma kimasomo mkoani Dar es Salaam, mkoani Katavi idadi hiyo ni watoto saba kati ya 10.

“Takwimu hizo za Uwezo zinaonesha kuwa maeneo wanapoishi watoto yana mchango mkubwa katika kujifunza kwa watoto hao kuliko umasikini, kiwango cha elimu ya mama, iwapo mtoto amesoma shule ya awali au hata watoto wenye udumavu. Ukweli huu ni changamoto kwa watunga sera kuelekeza juhudi na rasilimali kwenye wilaya au sehemu hizi,” anasema.

Kuhusu matabaka hayo

Anasema matabaka hayo yanajitokeza kwenye jamii hali ambayo ikiachwa iendelee kutakuwa na maeneo yenye wasomi na wasiosoma.

Anasema mbali na matabaka kuwepo kulingana na maeneo, hata huduma kwenye shule zinatofautiana kati ya shule na shule.

Akitoa mfano katika mkoa wa Dar es Salaam nusu ya shule ambazo ni asilimia 51 zina huduma ya umeme wakati katika mkoa wa Geita ni shule mbili kati ya 50 ndizo zenye umeme.

Anasema mkoa wa Geita shule za msingi zinazopata maji ni asilimia 12 ya shule zote wakati katika mkoa wa Kilimanjaro asilimia 78 ya shule zina huduma hiyo.

“Mkoa wa Kilimanjaro wanafunzi 26 wanatumia choo kimoja lakini mkoani Geita wanafunzi 74 wanatumia choo kimoja,” sehemu ya matokeo ya utafiti yanaonyesha.

Alisema asilimia tano ya shule mkoani Geita zinatoa huduma ya chakula cha mchana wakati Kilimanjaro ni asilimia 79.

Alisema mkoa wa Kilimanjaro una uwiano mzuri kati ya walimu na wanafunzi ambao ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 36 ikilinganishwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 52 mkoani Katavi.

Wadau wazungumzia utafiti

Mchambuzi wa siasa, Profesa Mwesiga Baregu anasema Serikali inatakiwa kuandaa mjadala wa kitaifa ili kuzungumzia kuhusu matabaka yanayojitokeza katika elimu.

“Tunatakiwa kuangalia tunayasaidia vipi maeneo haya ambayo matokeo ya mitihani kila mwaka yanakuwa mabaya vinginevyo tutakuwa na matabaka katika nchi yetu,” anaeleza.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Luka Mkonongwa anasema matokeo ya utafiti huo yanaonyesha hali halisi iliyopo kwenye shule.

“Kuna matabaka katika shule zetu, kuna watoto wanaosoma shule katika mazingira mazuri wengine wanapata shida katika kupata elimu,” anasema.

Anasema walimu wanaofundisha kwenye maeneo yenye mazingira magumu wanatakiwa kupewa motisha ili kuleta usawa.

Kwa upande wake, mmiliki wa Shule ya Sekondari ya Kifai Modern, Joseph Mmbando anasema shule za msingi za Serikali zitaendelea kufanya vibaya hadi hapo Serikali itakapoamua kuwathamini walimu.

“Nashangaa mwalimu mkuu wa shule ya msingi anasimamia watoto zaidi ya 3,000 lakini anasimamiwa na kamati ya shule ambayo ina watu wasiokwenda shule, kutakuwa na nini hapo zaidi ya kumpiga majungu?” anahoji.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga anasema ipo haja kwa Serikali kuwekeza kwenye elimu kwa kuhakikisha mikoa haipishani katika mahitaji muhimu ikiwamo walimu na miundombinu.

“Kama tatizo ni walimu au miundombinu basi mikoa yenye hali ngumu inapaswa kuangaliwa kwa ukaribu zaidi. Hii itasaidia kuwa na ufaulu usiopishana kwa kiwango kikubwa kati ya mkoa na mkoa,” anasema.