Wednesday, October 11, 2017

Uteuzi wa Katibu wa Bunge na Katiba dhaifu!

 

        Rais John Magufuli amemteua Steven Kigaigai kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akichukua nafasi ya Thomas Kashilila ambaye uteuzi wake umetenguliwa na imeelezwa kuwa atapangiwa majukumu mengine. Kigaigai alikuwa msaidizi wa karani msaidizi kwenye baraza la mawaziri na amefanya kazi kwenye kamati ndogo ya Katiba na Bunge ambayo iko chini ya baraza la mawaziri akifanyia kazi zake Ofisi ya Rais, Ikulu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ibara ya 87 (1), Katibu wa Bunge la Tanzania anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka miongoni mwa maofisa waandamizi (wa juu) wanaoshikilia madaraka katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba hiyo hiyo kwenye ibara ya 88 (2) imeeleza kuwa madaraka ya Katibu wa Bunge ni kuwa mtendaji mkuu wa mhimili wa Bunge na kutekeleza kazi za Bunge kwa mujibu wa Katiba.

Ukiachilia mbali Katiba, iko sheria ambayo imeweka masharti ya kutekeleza ibara za Katiba ambazo nimezitaja hapo juu, sheria hiyo ni Sheria ya Utawala wa Bunge ya mwaka 2016 ambayo imezungumzia mamlaka na uwepo wa Katibu wa Bunge na kuweka masharti ya uteuzi wake katika kifungu cha 7 (1 -2) cha sheria hiyo. Katika kifungu cha 7(3) sheria imeeleza kuwa Katibu wa Bunge atateuliwa na Rais kutoka kwenye majina matatu yaliyopendekezwa kwake na Tume ya Huduma ya Bunge kamati ya bunge. Kifungu hicho kinasisitiza kuwa uteuzi wa katibu huyo wa Bunge unapaswa kuzingatia masharti yaliyowekwa kwenye Katiba ya Tanzania katika ibara ya 87.

Wabunge ambao ni wajumbe wa Tume ya Huduma ya Bunge wanaeleza kuwa hawakuwahi kushiriki kwenye mchakato wa kuteua katibu wa Bunge na wanashangazwa kwamba Rais amemteuaje ikiwa kamati hiyo haikuhusishwa kama Katiba inavyotaka? Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameeleza kwamba utaratibu huo haukufuatwa na hivyo Katiba imevunjwa. Zitto ana maana kuwa Rais hakupokea majina matatu kutoka kwenye tume ya utumishi na badala yake aliteua bila kuihusisha.

Sote tunakubaliana kuwa kimamlaka Rais ndiye anamteua Katibu wa Bunge. Mjadala wa ni kiasi gani Rais amefuata masharti yote ya sheria na Katiba kabla ya kumteua mhusika hilo ni jambo ambalo kwa sasa hatutalijadili. Mantiki ya mjadala wa sasa ni kujionea namna gani Rais wa Tanzania ana madaraka makubwa sana mpaka juu ya mihimili mingine. Na kama alivyowahi kunukuliwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, kwamba “…katiba ya Tanzania inanipatia mamlaka makubwa mno, hata ya kuwa dikteta” (maneno yangu).

Wosia wa Mwalimu uko wazi kabisa, kwamba Taifa letu likiwa tayari linapaswa kubadilisha Katiba yake haraka ili mamlaka yanayotolewa na Katiba hiyo kwenda kwa mihimili mikuu ya nchi na idara zake yaweze kuendana na wakati uliopo na yazingatie mahitaji ya msingi ya Taifa kwa wakati husika hasa kwa kujikita kwenye udhibiti wa mamlaka ya viongozi wa umma akiwamo Rais.

Jaji Mkuu na majaji

Kwa mujibu wa Katiba hiyo hiyo ya Tanzania, Jaji Mkuu na majaji wenzake wanateuliwa na Rais Tanzania baada ya michakato kadhaa ndani ya Serikali na mahakamani.

Pamoja na kuwa Katiba imejaribu kuweka utaratibu kuwa Rais anapaswa kuletewa majina kadhaa, ukweli ni kuwa ukuu wa Rais kikatiba nyakati zingine unamfanya aachane na sharti hilo na ajiteulie tu mtu anayemhitaji na hakuna anayeweza kumuhoji. Na hata ikitokea watu wakahoji ikiwa uteuzi fulani umepitishwa kwenye tume za uteuzi kabla ya kumfikia Rais kwa maamuzi? Jibu kwa watu hao litakuwa rahisi sana kutoka serikalini, kwamba “Serikali imezingatia utaratibu”.

Ikumbukwe kuwa watu ambao wamo kwenye hizo tume hadi mwenyekiti wa tume mara nyingi wanateuliwa na Serikali na hususani Rais. Kwa hiyo ni watu wanaotenda kazi kwa kumuogopa Rais na wasipofanya hivyo wanaweza kuondolewa kwenye nyadhifa hizo wakati wowote. Ili kulinda nyadhifa zao lazima wakae kimya, wasiseme jambo lolote lile na mkakati wa Serikali unakuwa ni kuwawahi na kujibu malalamiko au wasiwasi ya wananchi kwa jibu la “Rais amefanya uteuzi husika kwa kuzingatia katiba na sheria”.

Hizi serikali za Ki-Afrika zinajiendesha chini ya mazingira magumu sana, mkishatoa mamlaka makubwa sana kwa Rais hutumia mwanya huo huo kudhibiti hata kila mhimili na kudhibiti hata wale ambao wangelimuhoji kisheria.

Kwa hiyo ni rahisi kusema kwamba Mahakama ya Tanzania na Bunge la Tanzania viko kwenye wakati mgumu mno kwa sababu Rais wa Tanzania anayo mamlaka makubwa sana ya kupanga safu za uongozi na utendaji za vyombo hivyo moja kwa moja, kibinadamu Rais hawezi kuweka watu watakaokuja kumhoji, na ndicho kinachotokea.

Madhara yake

Madhara ya nguvu ya Rais katika uteuzi ni kubwa mno. Nguvu hiyo inaathiri moja kwa moja ukuu na uhuru wa Mahakama na Bunge. Ikiwa Rais wa Tanzania ndiye anateua Jaji Mkuu na majaji (kwa utaratibu wa kikatiba na kisheria ambao una mianya mingi ya kudhibitiwa na Rais – haujafungwa) na tena Rais wa Tanzania ndiye anateua Katibu wa Bunge na huku kwa sasa akiwa na nguvu juu ya Spika wa Bunge (kwa sababu Rais ni mwenyekiti wa chama anachotoka Spika wa Bunge) – ndipo tunapaswa kukubaliana kuwa Tanzania inahitaji mabadiliko makubwa sana ya Katiba. Madhara ya hali ya sasa ni kuwa Bunge na Mahakama kila mara vinazongwa na Serikali na vinatekeleza matakwa ya Serikali kirahisi. Madhara yake ni kuwa pamoja na uwepo wa kinga za majaji na viongozi wa Bunge, bado kinga hizo siyo kitu chini ya Rais. Rais anaweza kabisa kisirisiri au kwa wazi akamshinikiza jaji ajiuzulu na mhusika asipofanya hivyo Rais anaweza tena kwa siri au kwa wazi kumshughulikia mhusika bila kujali kuwa ana kinga.

Wakati huo huo Rais anaweza kabisa kulizonga Bunge kwa namna nyingi, anaweza kutumia vikao vya chama chake kumtishia spika wa bunge, anaweza kutumia vyombo vya dola, anaweza kumnyima fedha za kufanya masuala muhimu ya kibunge na kibinafsi na mengine mengi.

Ukiyatafakari masuala yote haya ndipo unakubaliana na Rais Barack Obama wa Marekani alipowaeleza wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Ghana kwamba “Afrika inahitaji taasisi imara, haihitaji viongozi imara”.

Kazi za Katibu wa Bunge

Ukisoma sheria ya Bunge unagundua kuwa kazi za Katibu wa Bunge ni za kuliwakilisha bunge na mkuu wa bunge ni Spika, siyo Rais. Kichekesho ni kuwa Katiba yetu bado inatoa mwanya kwa Rais kuteua Katibu wa Bunge ili afanye kazi za Bunge ambalo linaisimamia Serikali ambayo rais ni kiongozi wake, haiwezekani!

Ndiyo kusema kuwa pale bungeni Rais anateua Spika (maana mchakato wa kumpata anayegombea uspika unafanywa chini ya Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama), Rais anateua pia Katibu wa Bunge kusimamia kazi zote za Bunge. Rais anateua Waziri Mkuu ambaye anaiwakilisha Serikali inayokwenda bungeni kusimamiwa na Bunge ambalo viongozi wake wakuu watatu (Spika, Naibu Spika na Katibu wa Bunge) wanateuliwa na Rais moja kwa moja au kwa njia za mlango wa nyuma.

Ndiyo kusema kuwa tayari Bunge la Tanzania limezingirwa kila sehemu, Mahakama ya Tanzania imezingirwa kila sehemu. Mihimili hii miwili imezingirwa kila mahali, kusini, kaskazini, magharibi, mashariki, na mzingiraji ni rais wa Tanzania kutokana na mamlaka ya kikatiba aliyonayo. Hii ni hatari kweli kweli.

Katiba ya Warioba

Katiba ya Warioba ilikuja na misingi mizuri ya kuanzia kujenga Taifa lenye taasisi imara, kwa bahati mbaya rasimu ile ikatupwa kapuni baada ya CCM kuizingira kwa kutumia nguvu zile zile za Rais (wakati huo Jakaya Kikwete), mchakato ule ukafa na Rais wa sasa hana mpango tena na Katiba mpya au Katiba ile au kuuhuisha mchakato ule. Hapo ndipo Taifa linakaa kwenye mtanzuko mkubwa sana wakati Rais akiendelea kutumia madaraka yake kudhibiti mihimili mingine ya dola.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii na Kisiasa, Mtafiti, Mwanasheria na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com/ Tovuti; juliusmtatiro.com.     

-->