Uwekezaji kwenye mawese utamaliza uhaba wa mafuta ya kula nchini

Muktasari:

  • Wakati Malaysia ni mzalishaji wa pili duniani wa mafuta hayo baada ya Indonesia, Tanzania inaagiza mafuta ya kula kutoka nje hasa taifa hilo la Asia.
  • Inakadiriwa, tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese huagizwa kila mwaka ili kukidhi mahitaji nchini, licha ya uwezo wa kuzalisha mbegu za mafuta tofauti.

Tanzania na Malaysia zina hali ya hewa inayokaribiana kwa kukuza michikichi, inayozalisha mafuta ya kupikia aina ya mawese.

Wakati Malaysia ni mzalishaji wa pili duniani wa mafuta hayo baada ya Indonesia, Tanzania inaagiza mafuta ya kula kutoka nje hasa taifa hilo la Asia.

Inakadiriwa, tani zisizopungua 400,000 za mafuta ya mawese huagizwa kila mwaka ili kukidhi mahitaji nchini, licha ya uwezo wa kuzalisha mbegu za mafuta tofauti.

Tanzania inazalisha karanga, alizeti, ufuta, pamba na mafuta ya mawese lakini karibu asilimia 50 ya mafuta ya kula ni kutoka nje hasa Malaysia.

Malaysia ni ya pili kwa ukubwa duniani kwa uzalishaji mafuta ya mawese, inasema Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa na kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi kama uwekezaji sahihi wa kilimo cha michikichi utafanyika.

Wiki iliyopita, Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) kilikuwa mwenyeji wa Bodi ya Mafuta ya Mawese ya Malaysia (MPOB) kwa ajili ya semina ya kiufundi, ambayo ilikuwa na lengo la kuhamasisha Watanzania kushiriki katika kilimo biashara cha michikichi.

Bodi hiyo inataka kubadilishana ujuzi na wakulima wa ndani kwa kuandaa safari za kujifunza na misaada mingine ya ufundi.

Malaysia ilizalisha tani milioni 20 za mafuta ya mawese katika mwaka 2015, ambazo zilikuwa asilimia 32 ya jumla ya uzalishaji wa kimataifa ambao ni tani milioni 62.8. Taarifa za bodi hiyo zinaonyesha.

“Hatukuwa tunazalisha mafuta ya mawese Malaysia. Zao hili lilitoka Afrika Magharibi kisha tukalikuza na baadaye kufanya nchi yetu kuwa ya pili kwa uzalishaji, baada ya Indonesia. Tunadhani, Tanzania pia inaweza kuwa mzalishaji mwingine mkubwa kama Malaysia ukizingatia hali ya hewa ya nchi hizi mbili inakaribiana,” alinukuliwa ofisa mmoja wa bodi hiyo.

Mawese Tanzania

Mafuta ya mawese nchini yanazalishwa kwa wingi katika Mkoa wa Kigoma ambako michikichi ilianza kulimwa miaka ya 1920, kwa mujibu wa tathmini ya uwezo wa mbegu za mafuta ya kula zinazozalishwa Tanzania; ripoti iliyotolewa na Chama cha Watendaji wa Mafuta ya Kula Tanzania (Teosa) mwaka 2012 kwa msaada wa taasisi ya kusaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini, Best-Dialogue.

Kilimo hiki kilipewa umuhimu zaidi katika miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990, baada ya kuanzishwa kwa teknolojia ya usindikaji kwa ushirikiano wa Shirika la Viwanda Vidogovidogo nchini (Sido) na Kituo cha Chakula na Lishe (TFNC).

Kigoma inazalisha zaidi ya asilimia 80 ya mafuta ya mawese nchini na asilimia 20 iliyobaki inatoka wilayani Kyela, mkoani Mbeya. Sido ilichochea teknolojia ya kusaga mbegu za mawese na kutengeneza sabuni katika ngazi ya ujasiriamali mdogo na wa kati.

Hata hivyo, mabonde ya Mto Rufiji na Kilombero yanatajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye uwezekano wa kustawisha michikichi kwa wingi na kuiongezea Tanzania uwezo wa kuzalisha mafuta ya mawese, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Kampuni ya African Green Oil iliripotiwa kuwa na mpango wa kuendeleza hekta 20,000 ifikapo mwaka 2020. Hadi mwaka 2009, kampuni hiyo ilikuwa imepewa hekta 5,000 na ilipanda hekta 435 kwa ajili ya majaribio. Katika Wilaya ya Bagamoyo iliyopo mkoani Pwani, Kampuni ya Tanzania Biodiesel Plant ilikuwa na hekta 16,000 kwa ajili ya kilimo hicho wakati Kampuni ya Infenergy ilikuwa imepewa zaidi ya hekta 5,000 katika Wilaya ya Kilombero kwa ajili ya lengo hilohilo.

Mkakati

Ili Tanzania ifanikiwe na kujitosheleza kwa mafuta ya kula, wadau wanasema mambo kadhaa yanahitaji kufanyika ili kukabiliana na changamoto zilizopo katika maendeleo ya sekta hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Teosa, Rashid Mamu anasema kuna masuala ya ufundi na kisera ambayo lazima yashughulikiwe kwanza ili kuendeleza sekta ya uzalishaji mafuta.

“Kuna changamoto ya mitaji, kusambaza mbegu sahihi na upatikanaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa kupitia mbegu za mafuta ya kula,” anasema.

Mamu anasema Serikali haitengi bajeti ya kutosha kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya mbegu za kisasa ambazo zitasaidia kuboresha uzalishaji na kuwawezesha wakulima kuwa na uhakika wa mavuno yanayokidhi uwekezaji wao.

Kuna aina nyingi za mbegu zenye uwezo tofauti wa uzalishaji. Mamu anatoa mfano wa mbegu chotara ya alizeti ambayo inaruhusu uzalishaji wa magunia 30 kwa eka moja na mbegu za kienyeji ambazo huzalisha magunia matatu kwa eka, lakini wakulima wengi hutumia za asili ambazo hutoa mavuno kidogo kutokana na gharama kubwa za kununua mbegu za kisasa.

“Kilo moja ya mbegu ya kisasa ya alizeti, kwa mfano huuzwa Sh37,000... mkulima gani mdogo anaweza kumudu bei hiyo?” anahoji na Mamu na kuongeza:

“Serikali inapaswa kuwasiliana na mamlaka zake na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya mbegu bora, iwe ni kwa ajili ya mafuta ya mawese au alizeti kwa kuhusisha vituo vya utafiti kufanya hivyo.”

Upatikanaji fedha

Suala jingine analosema kuwa changamoto, ni fursa ya kupata fedha. Anasema kuna upatikanaji mdogo wa huduma za fedha hasa maeneo ya vijijini ikiwamo masharti magumu ya mikopo inayohitaji dhamana na viwango vikubwa vya riba.

Mamu anasema badala ya kuwaambia wawekezaji kuendesha mashamba makubwa ya kilimo cha michikichi kisha kuzalisha mafuta ya mawese, Serikali inapaswa kuwasaidia wakulima wadogo kuboresha mashamba yao na wakati wa usindikaji.

Masoko

Anasema soko la mafuta ya kula hasa ya mawese linapaswa kuundwa ndani na nje ya nchi, ili kuvutia wawekezaji zaidi katika uzalishaji wa mbegu za mafuta.

Mamu anasema soko la ndani limejaa mafuta kutoka nje, hali ambayo inawakatisha tamaa wakulima na wawekezaji wengine kuzalisha zaidi.

Ukurasa wa mazingira bora ya kufanya biashara umerudi kwenye gazeti la Mwananchi kila Alhamisi ukiwa na lengo la kuunga mkono jitihada za wajasiriamali nchini. Kwa maoni tuma ujumbe mfupi kwenda namba 0786240172 ukianza na neno RB kwa gharama za kawaida za ujumbe au baruapepe: [email protected]