Viazi lishe fursa mpya ya biashara, lishe

Muktasari:

Viazi vimekuwa vikitumika kama chakula cha asili kwa kuchemshwa na kuchomwa na wakati mwingine hukatwa na kukaushwa kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu.

Zao la viazi limekuwa likilimwa kwa muda mrefu nchini. katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na ni la pili kwa kulimwa baada ya mahindi.

Viazi vimekuwa vikitumika kama chakula cha asili kwa kuchemshwa na kuchomwa na wakati mwingine hukatwa na kukaushwa kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu.

Hata hivyo, viazi hivyo vya asili havikuwa na virutubisho vya kutosha kwa lishe ya jamii, ndiyo maana Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Ukiriguru mkoani Mwanza imefanya utafiti wa mbegu za viazi kwa kuviwekea virutubisho hasa vitamin A.

Mradi huo unaofadhiliwa na mfuko wa Bill and Melinda Gates na Jukwaa la Kilimo (Ansaf) unatekelezwa nchini, huku katika Kanda ya Ziwa ukihusisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.

Katika Mkoa wa Mwanza kuna wilaya za Misungwi na Sengerema na halmashauri ya Buchosa, wakati Mkoa wa Shinyanga uko katika eneo la Shinyanga vijijini. Mkoani Kagera upo katika wilaya za Karagwe na Kyerwa.

Ofisa Kilimo Msaidizi wa Ukiriguru, Baker Chirimi anasema walianza kwa kufanya utafiti wa mbegu bora za viazi kabla ya kuanza kuzisambaza.

“Kuna aina saba za mbegu tunazozalisha zikiwa kwenye makundi ya kawaida. Kundi la lishe, yaani viazi vya karoti vipo vya Ukiriguru 05, Kabode na Mataya. Kundi la pili la viazi vyeupe lina mbegu za Mazao na Naspoti 11,” anasema Chirimi.

Pamoja na mbegu hizo, anasema kuna mbegu za nyongeza katika kundi la kwanza ambazo ni Mlezai na Kakamega na kundi la pili kuna nyongeza ya New Dimbuka na Polyster.

“Huwa tunazitenga mbegu hizi tunapozigawa kwa wakulima ili tusiwachanganye. Lakini kwenye maonyesho yetu huwa tunaziweka zote ili wajifunze,” anasema Chirimi.

Anaeleza kuwa mbegu hizo zimefanyiwa majaribio kwenye mashamba darasa kwenye kituo hicho kati ya miaka minane hadi 10, hata hivyo kwa sasa wamepunguza muda huo hadi kufikia miaka sita.

Jinsi mbegu zinavyogawanywa

Chirimi alisema kinachofanyika ni kugawa mbegu katika wilaya kwa kutumia wanafunzi wa shule za msingi kwa mpango unaoitwa ‘sambaza marando faster’.

“Kwanza tunaainisha kata katika wilaya ambako tunachagua kijiji kimoja na hapo tunachagua shule moja ya msingi. Katika shule hiyo tunachagua wanafunzi 200 wanaotoka katika kaya tofauti,” anasema.

Wanafunzi hao huchaguliwa kutoka kaya tofauti na kupewa mbegu 120 kila mmoja zikiwa kwenye makundi ya aina nne tofauti. Baada ya hapo wanafunzi wao huelekezwa kuwapa wazazi wao ambao nao hupata mafunzo ya kuzipanda.

Anasema viazi hivyo hukomaa baada ya miezi miwili na mkulima hutakiwa kugawa mbegu 240 kwa wakulima wengine.

Ufanisi wa mradi

Akizungumzia ufanisi wa mradi huo, anasema viazi vimeongeza usalama wa chakula kwa wakulima kwa sababu awali walikuwa wakipata tani mbili kwa ekari moja, lakini kwa viazi hivi mkulima anaweza kupata hadi tani sita za viazi kwa ekari moja.

“Mkulima akitumia njia bora za kilimo atapata chakula na ziada ya kuuza. Gunia moja la viazi linauzwa kati ya Sh30,000 hadi Sh40,000.

Wasemavyo wakulima

Wakizungumzia kilimo cha viazi wilayani Misungwi, baadhi ya wakulima wanasema wamepata mafanikio makubwa.

Amos Khamis wa kijiji cha Mapilinga alisema alianza kulima viazi lishe Februari 2017 na amegundua tofauti na viazi vya asili.

“Tangu nimeanza kilimo cha viazi lishe, nimeona vinatoa viazi vingi kuliko viazi vya kawaida. Kama kuna uwezekano tuboreshewe. Kwa eneo hili nategemea kuvuna magunia 50 wakati yale malando ya zamani nilikuwa napata magunia 10 katika ekari hii moja.

Natarajia kukabiliana na njaa katika familia yangu na natarajia kufanya biashara.

Naye Veronica Simon wa kijiji hicho anasema aliletewa mbegu ya viazi na watoto wake kutoka shule mwaka 2016 na ndipo alipoanza kustawisha.

“Nina jumla ya watoto wanane, awali tulikuwa tunapata shida ya chakula kutokana na ukame, lakini sasa tunafaidika na viazi hivi, kwa sababu vinazaliana kwa wingi kuliko viazi vya kawaida.

Veronica alisema ana shamba la ekari moja la viazi huku pia akilima mazao mengine ya chakula. Anasema anatarajia kuvuna magunia 70 ya viazi atakavyotumia kwa chakula na kufanya biashara.

“Tangu nimeanza kilimo hiki, nimeshagawa mbegu kwa wakulima zaidi ya 20 kama mradi unavyotaka,” anasema Veronica.

Cecilia Tondogoso wa kijiji cha Amani wilayani Sengerema, anasema alipokea mradi huo mwaka 2015 na mpaka sasa wamenufaika mara mbili.

“Tumenufaika mara mbili kwa kupata chakula cha kutosha na vitamin. Kwa mfano, unaweza kulima nusu ekari ukavuna magunia 12, lakini nilipoanza viazi hivi nilipata magunia 16. Viazi hivi naviuza na kutumia kwa chakula,” anaeleza.

Hata hivyo, anasema tatizo la ukame limeathiri kilimo hicho na upatikanaji wa chakula kwa ujumla.

Bwana shamba wa kata ya Kishinda, Kassim Maira anasema wamekuwa wakiwaunganisha wakulima katika vikundi ili kuwawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo hicho.

“Mpaka sasa tuna vikundi 23 kwa zao la mpunga na tunaendelea kuunganisha vikundi vya wakulima wa viazi, ili kutatua changamoto za fedha, masoko na pembejeo,” anaeleza.

“Tuna mpango wa kuongeza uzalishaji wa viazi ili tusindike na tuuze unga wake kwa kuwa una soko kubwa. Changamoto iliyotukwamisha ni ukame uliotokea mwaka jana,” alisema Maira.