Wadau; Mitalaa chanzo cha wahitimu kutoajirika

Muktasari:

  • Tafiti zinaonyesha nusu ya wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za Afrika Mashariki hawaajiriki.

Wazazi wengi wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuwasomesha watoto wao ili baadaye waje kuwa na maisha bora.

Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda, ndoto ya wazazi wengi kuwa elimu wanayoipata watoto wao itawasaidia kuishi maisha bora kwa kuajiriwa ama kujiajiri, inatoweka.

Kutoweka kwa ndoto za wazazi sio pigo lao pekee, bali ni pigo kwa taifa zima.

Tatizo ni mitalaa

Katibu Mtendaji wa Chama cha Waajiri katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAEO), Dk Aggrey Mlimuka anasema kuna tatizo katika baadhi ya mitalaa ya vyuo, kwani haijibu changamoto katika soko la ajira.

Anasema ni muhimu sasa vyuo vikuu na vyuo vingine, vikapitia upya mitalaa yao ili iendane na soko la ajira.

Dk Mlimuka anasema katika nchi za Afrika ya Mashariki hivi sasa, tafiti walizofanya zinaonyesha karibu nusu ya wahitimu wa vyuo hawana sifa stahiki za kuajirika. “Hili tatizo ni kubwa sio Tanzania pekee bali ni nchi zote za Afrika ya Mashariki, hivyo ni muhimu kama ambavyo nimemsikia Rais mstaafu Benjamin Mkapa akishauri kuwepo kwa mjadala wa kitaifa juu ya elimu,” anasema.

Anasema kuna haja kuwa na uhusiano kati ya mitalaa inayofundishwa vyuoni na mabadiliko katika soko la ajira ili wahitimu waweze kuajirika.

INAENDELEA UK 14

INATOKA UK 13

Dk Mlimuka anasema wao kama waajiri changamoto ya kukosa vijana wenye sifa stahiki imekuwa ni tatizo kubwa na hivyo baadhi yao kulazimika kutafuta watalaamu nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Tatizo la uhaba wa wafanyakazi wenye sifa stahiki kwa sasa linazikabili sekta nyingi, hali ambayo inaweza kuathiri pia ubora wa huduma.

Nicolaus Negre, mkurugenzi wa hoteli za Chemchem zilizopo wilayani Babati anasema ni huzuni wazazi wanapojinyima na kutumia fedha zao kidogo kuwasomesha watoto, lakini wanapomaliza masomo wanakosa ajira kutokana na upungufu wa sifa.

“Ni muhimu vijana wanapomaliza masomo yao wajimudu kimaisha na hii itawezekana wakipata kazi ama wakijiajiri. Lakini kama wanakosa sifa ni tatizo,” anaeleza.

Mbinu mbadala kupata sifa za kuajirika

Ili kukabiliana na tatizo la vijana wanaohitimu vyuo kukosa ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri, mikakati kadhaa imeanza kuwekwa na waajiri .

Dk Mlimuka anasema moja ya mikakati ya kukabiliana na hali hiyo ni kuhimiza mafunzo kwa vitendo kazini na uanagenzi.

Anasema mpango huo utawezesha vijana kuajiriwa na kupatiwa mafuzo kazini ili waweze kumudu kazi.

“Pia sasa tunahimiza vijana walio vyuoni kupata muda wa mafunzo sehemu za kazi, ili wakimaliza masomo waweze kuwa na uwezo wa kufanya kazi,” anasema.

Athari za wahitimu kukosa sifa

Baadhi ya waajiri na wahitimu wa vyuo wanaeleza kuwapo kwa athari ambazo tayari zinaonekana kutokana na kukosekana kwa elimu stahiki kulingana na mazingira ya sasa.

Dk Mlimuka anasema hivi sasa baadhi ya waajiri wameanza kufuata wataalamu nje ya nchi katika baadhi ya sekta ili kuwapa kazi japo ni gharama kubwa.

“Sisi kama waajiri tunapenda sana kuajiri wazawa katika kazi, lakini kama wakikosa sifa ndio sababu tunatoka kutafuta wenye sifa sehemu nyingine ili kuongeza uzalishaji,” anaeleza.

Mdau wa elimu, Dk Jeremiah Kaaya anasema kukosekana kwa sifa stahiki kwa vijana wanaohitimu vyuo kunachangia wengi kushindwa kujiajiri na kubaki mitaani wakisubiri kuajiriwa.

“Kama kijana amepata mafunzo ya kutosha anapaswa kuwa na uwezo wa kujiajiri na kuna fursa nyingi zipo kulingana na taaluma zao. Lakini kama ukiona wahitimu wote wanalalamikia ajira ujue kuna tatizo,” anasema.

Happy Mtani anakiri baadhi ya wahitimu kuwa na udhaifu sehemu za kazi na bila msaada inakuwa ngumu kufanya kazi.

“Ni kweli, nadhani kuna matatizo kidogo katika mafunzo vyuoni jambo ambalo linatupa wakati mgumu kufanya kazi. Lakini kama waajiri wakiwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa vitendo itasaidia,” anasema.

Anasema mtu hapaswi kuona aibu kujifunza tena akiwa kazini kwa kuwa ni wazi elimu inayotolewa vyuoni haikidhi mahitaji ya soko la ajira.

“Mimi hivi sasa nasoma, kuna ambao wananicheka kuwa nasoma Memkwa (Mpango wa elimu kwa waliokosa), lakini nawaeleza mimi nimebaini upungufu na elimu ya vitendo na lugha ambayo nasoma inaboresha utendaji kazi wangu,” anasema.

Serikali yachukua hatua

Katibu mkuu wa Wizara ya Kazi, Eric Shitinde akizungumza tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu, anasema Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali.

“Serikali imeandaa mwongozo wa Taifa wa uanagenzi na mwongozo wa Taifa wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo ili waweze kuajirika,” anasema.

Akizungumza katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo, Shitinde alisema hadi sasa tayari vijana 3,660 wameandikishwa kupata mafunzo mbalimbali ya kuwajengea ujuzi kwa njia ya uanagenzi na 1,447 wamehitimu.

Anasema, sera ya Taifa ya ajira ya mwaka 2018 inaendelea kukamilishwa na hivi karibuni itapelekwa kwenye baraza la mawaziri.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nayo imekuwa na maboresho kadhaa, ikiwemo kuvizuia kufanya udahili vyuo visivyo na sifa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amekuwa na utaratibu wa kufanya ziara za kushtukiza katika vyuo ili kubaini kama vina sifa za kutoa elimu au vinginevyo.

Hatua hiyo imezaa matunda kwa kuwa vyuo kadhaa vimezuiwa kuendelea na udahili hadi vifanye maboresho.