Wafanyabiashara kuweni wakweli kuliko kuwapa shida wananchi

Muktasari:

Nataka ujumbe huu, uwafikie kutokana na ukweli kuwa wengi wao, hawasemi ukweli kuhusiana na sakata za kupanda bei ya sukari na mafuta nchini.

Kuna usemi maarufu kuwa ‘Msema kweli ni mpenzi wa Mungu’. Naomba usemi huu uwafikie wafanyabiashara wa sukari na mafuta ya kula kote nchini.

Nataka ujumbe huu, uwafikie kutokana na ukweli kuwa wengi wao, hawasemi ukweli kuhusiana na sakata za kupanda bei ya sukari na mafuta nchini.

Inawezekana wana sababu za kuficha ukweli, lakini naamini kama kweli wana nia njema ya kutotaka kuwapa mzigo mkubwa wananchi, wanapaswa kusema ukweli.

Wananchi wamekuwa wakipiga kilele kupanda bei ya mafuta ya kupikia na sukari katika maeneo mengi, lakini pindi serikali inapotaka kuchukua hatua utasikia kauli kutoka kwao kuwa wana akiba ya kutosha.

Sasa swali la kujiuliza kama wana akiba ya kutosha iweje leo, bei ya sukari ipande kutoka 2,200 hadi kufikia kati ya Sh2,600 hadi 3,000 kwa kilo moja.

Wanasema kuna akiba ya mafuta lakini ni kwa nini bei imepanda kutoka Sh25,000 kwa lita 10 katika maduka ya jumla hadi kufikia kati ya Sh31,000 hadi 35,000 kwenye maduka ya jumla.

Kimsingi walio wengi tunaamini, kuna jambo linafichwa hapa, kwani haiwezekani bei ya sukari kuendelea kupanda halafu tuelezwe kuna akiba ya kutosha.

Nionavyo mimi kuna tatizo lipo na wafanyabiashara walio wengi hawataki kusema ukweli, labda wanahofu au wanataka kuwakomoa wananchi.

Kama katika maghala yao wanasema kuna akiba ya kutosha, licha ya uzalishaji kupungua tunapaswa kujua tatizo lipo wapi bei kuendelea kupanda mbona maduka ya rejareja kuna shida.

Tumeona jinsi tatizo hilo, lilivyoibuliwa bungeni lakini hakuna suluhu na tumeona hadi Rais John Magufuli alikwenda Bandarini kufuatilia suala la mafuta yaliyokuwa yamezuiwa.

Binafsi, naamini sakata la kupanda bei ya sukari na mafuta nchini, ni zaidi ya wengi wanavyofikiri, kwani kama kuingiza nchini bidhaa hiyo, inaelezwa masharti yamepunguzwa.

Katika viwanda na mashamba, tunaelezwa kuna mazingira mazuri na uwekezaji sasa tatizo lipo wapi?

Naamini wafanyabiashara mmoja mmoja ama kupitia mabaraza yao, wanawajibu kutoka hadharani na kueleza tatizo ni nini.

Hivi karibuni katika jiji la Arusha, Mkuu wa wilaya hii, Gabriel Daqqaro na kamati yake ya ulinzi na usalama, walitembelea maghala yote ya chakula jiji la Arusha kwa lengo moja tu, kujua kama kuna upungufu ama la ili bei iweze kujadiliwa.

Lakini kwa taarifa ya mkuu wa wilaya kwa vyombo vya habari, anasema maghala yote bado yana sukari na mafuta ya kutosha licha ya uzalishaji kupungua.

Mkuu huyo wa wilaya akaonya bei ya sukari isipande zaidi ya Sh2,600 kwa kilo na sambamba na mafuta na kuagiza watendaji wa serikali ngazi ya kata na mitaa kusaidia kutoa taarifa kwa watakaopandisha bei.

Lakini, mitaani bado bei juu na haipatikani kama ilivyo kawaida na si Arusha tu ni maeneo mengi hapa nchini, hali hii ndio inasukuma kutaka kujua tatizo ni nini, hofu, mgomo baridi ama kuna zaidi.

Jiji Dar es Salaam baada ya shehena ya mafuta kuanza kutolewa bandarini, ilitarajiwa pia bei kupungua lakini bado kuna tatizo.

Naamini kama wafanyabiashara wakiwa wakweli, wataweza kututoa katika mkwamo huu na watueleze tatizo ni nini.

Ni ukweli ulio wazi kuna biashara zinafungwa, maduka yanafungwa na wafanyabiashara hawachukui mikopo tena kwenye mabenki, swali la kujiuliza kuna tatizo gani.

Naamini serikali ina fursa nzuri kuingilia kati suala hili na kufanya uchunguzi mzuri kubaini kuna tatizo gani nchini.

Inawezekana ufumbuzi upo ndani ya wafanyabiashara wenyewe ama ndani ya Serikali na vyombo vyake, lakini kuficha ukweli si suluhu.

Wahenga walisema mficha ugonjwa mauti humuumbua, chonde chonde wafanyabiashara msifiche maradhi haya kwani wanaopata shida ni watu masikini tena wa vijijini.

Wito wetu tunawaomba kuwa wakweli kwa Serikali, mseme tatizo ni nini ili hatua zichukuliwe lakini mkiendelea kuwafurahisha viongozi kwa kauli kuwa mna sukari na mafuta ya kutosha wakati mtaani kuna shida hamuwatendei haki Watanzania.