Wanawake wanapojizeesha kwa vipodozi visivyofaa

Muktasari:

Wengi wamekuwa wakitumia kioo kujiridhisha kuwa wamependeza kwa namna walivyojipamba kwa vipodozi vya aina mbalimbali

Mwanamke urembo ni kauli maarufu miongoni duniani kote. Hii inatokana na ukweli kwamba wanawake wengi hasa katika maeneo ya miijini hupenda kujiremba. Hata hivyo baadhi yao wamekuwa wakikosea kujipamba hivyo kuonekana kituko badala ya kuvutia.

Wengi wamekuwa wakitumia kioo kujiridhisha kuwa wamependeza kwa namna walivyojipamba kwa vipodozi vya aina mbalimbali.

Mtaalam wa masuala ya urembo nchini, Shekha Nasser akizungumzia makosa ambayo yanafanywa na wanawake wengi wakati wanapojipodoa, hali ambayo imewafanya wasiwe na mvuto tofauti na matarajio yao.

“Urembo kwa mwanamke ni jambo la kuvutia lakini kuna mambo muhimu ya kuzingatia ili kupendezesha uso na mwili kwa ujumla. Muhimu ni kuonekana unavutia zaidi popote utakapotokelezea na watu au mtu anayekuona akikusifu awe anamaanisha na siyo kukusanifu,” anasema Shekha.

Anasema mambo kadhaa ambayo yanapaswa kuzingatia ili kumfanya msichana au mwanamke aonekane mrembo ni pamoja na kuutambua vyema uso wako ulivyo na rangi ya ngozi yako.

Anasema kwanza kabisa uso kabla ya kuwekewa vipodozi unapaswa kuwa katika hali ya usafi hivyo uso wako kwa maji ya uvuguvugu na sabuni kisha kukausha vizuri na kitaulo laini.

“Hata hivyo, maandalizi ya kujipamba uso yanatofautiana na mazingira kwa kuwa anaweza kujipambia nyumbani ambapo kuna baadhi ya vifaa wengine hawana, hivyo huchagua saluni yenye vifaa vya kisasa kutimiza kusudi lao,” alisema.

Anasisitiza kutumia cleanser yoyote ni vizuri zaidi kuondoa uchafu kwenye uso wako kwa kutumia pamba, baada ya hapo unaosha tena uso kwa maji ya uvuguvugu na kuukausha kabla ya kupaka foundation (poda maalum yenye unyevunyevu).

“Inatakiwa kupakwa kwa kutumia kifaa maalumu kisafi au pamba kutumia ukianzia katikati kwenda chini na juu, hatua hii itatoa nafasi ya kusambaa vyema baada ya hapo unatakiwa kupaka poda kavu inayoendana na ngozi yako juu ya foundation. Hapa kuna makosa hufanywa wengine hupaka zisizo za rangi zao,” alisema.

Shekha ambaye pia ni Mkurugenzi wa Chuo cha Urembo cha Manjano Beauty Academy, anasema kwa kawaida wenye ngozi za asili ya Afrika kuna njano kwa mbali tofauti na wazungu ambao wao wana rangi nyekundu.

“ Unaweza kuona mtu kajipodoa lakini kageuka kuwa kituko kwa kukosa mvuto kwa sababu katumia vipodozi bila kuzingatia ngozi yake. Yaani yeye ana ngozi ya Kiafrika halafu anapaka poda ya mtu mwenye ngozi nyeupe kama Mhindi au Mzungu,” alisema.

Anasema kuna haja ya kila mwanamke anayependa kujipodoa kuwa makini katika ununuzi wa vipodozi kwa kutambua ngozi yake. Mfano poda ya Mac zipo za aina mbili kuna Warm tone yenye manjano wakati Neutron haina.

“Ukiangalia upambaji wa sasa umekuwa na nakshi nzuri zaidi kutokana na poda zinazotumika zimezingatia mahitaji ya ngozi,” alisema.

Alisema ushahidi wa mambo anayoelezea umekuwa ukionekana kwa mabibi harusi ambapo wengi hujitahidi kuhakikisha wanapambwa kwenye saluni zenye vifaa, ambapo huwasaidia wengi kuonekana wenye mvuto wa tofauti na alivyozoeleka.

“Wanawake wengi wamekuwa wakipata shida kwenye nyuso zao kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutumia vipodozi visivyo na ubora lakini pia kupenda kula vyakula ambavyo vina mafuta mengi kama vile chips,” anasema Shekha.

Pilly Amiri wa Kithuraaah Collection naye ni mjuzi kwenye masuala haya ya urembo anaeleza kuwa urembo wa uso ni utumiaji wa vipodozi sahihi, ili kuremba na kuongeza nakshi na umaridadi katika mwonekano.

Anasema pamoja na mambo mengine uso kuongezea mwonekano, ambapo alitaja vitu vinavyohitajika kuwa ni pamoja na eye shadow, eye pencils, bronze, mascara, eye liner, brushes, powder, lipstick na lipliner.

Alisema vitu hivyo vinapaswa kupakwa kwa ustadi ikiwa ni pamoja na kuzingatia rangi ya ngozi na nguo na siyo kubahatisha.

“Lakini kwa mtu ambaye ana uwezo mdogo lakini anataka kujiongezea mvuto usoni mwake anapaswa kuwa na vitu vitatu na akaweza kubadili mwonekano wake vitu hivyo ni wanja, poda ya kawaida au akiweza ile yenye manjano na lipstick,” alisema.

“Vipodozi hivi havipaswi kupakwa uso ukiwa na mafuta, kwani husababisha jasho. Unalowana na kuweka michirizi inayoleta mwonekano mbaya au hata wanja ukiwa wa mafuta usipoudhibiti wa kupaka na poda kidogo unasambaa,” alisema Pilly.

Alibainisha kuwa pia katika utunzaji endelevu wa urembo wa uso, inatakiwa kuondoa vipodozi usoni kwa maji na sabuni au kwa kutumia mafuta ya nazi.

“Mafuta ya nazi yanaweza pia kutumika kuondoa vipodozi usoni, kwani inashauriwa kuitoa kabla ya kuingia kulala ili kuendelea na ngozi nzuri yenye afya ni lazima kuiondoa,” alisema.

Katika kitabu chake cha Afya na Urembo wa Msichana, Clifford Majani ambaye ni mwanataaluma wa tiba ya binadamu na mshauri nasaha kutoka taasisi inayoshughulika na utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR-Mbeya Medical Research Centre, Tanzania), anasema jamii inalo jukumu la msingi la kuwapa mwongozo wasichana kuhusu urembo salama.

Alieleza kuwa kuna uhusiano wa karibu sana kati ya afya na urembo wa msichana.

Afya bora inafanya msichana aonekane mrembo lakini pia matumizi ya vipodozi na vitu vingine vya urembo, huathiri afya ya mtumiaji kwa uzuri au kwa ubaya.

Majani alieleza kuwa urembo ni swala linalotokana na mtazamo wa jamii kwa wakati uliopo, ni kile jamii inachoamini kuwa kinavutia hisia, hata kama kwa hakika si urembo katika jamii nyingine.