Wanawake wasimame kwenye nafasi zao katika familia

Lilian Kimola

Muktasari:

  • Uvivu ni hali ya kutopenda kufanya kazi au kufanya katika kiwango hafifu.
  • Mara nyingi mtu mvivu hapendi kuishughulisha akili yake na kujikuta akifanya vitu vyepesi huku akiogopa changamoto za kimaisha zinazojitokeza mbele yake.

Dar es Salaam. Kama kuna jambo la hatari na linaloweza kuangamiza ya mwanadamu hasa mwanamke ni uvivu.

Uvivu ni hali ya kutopenda kufanya kazi au kufanya katika kiwango hafifu.

Mara nyingi mtu mvivu hapendi kuishughulisha akili yake na kujikuta akifanya vitu vyepesi huku akiogopa changamoto za kimaisha zinazojitokeza mbele yake.

Mwimbaji wa Muziki wa Injili nchini, Lilian Kimola anasema bidii kwenye kazi ndiyo siri ya mwanamke yeyote kuelekea kwenye mafanikio na kwamba, wengi wapo wengi wanaojikuta kwenye nyakati ngumu kwa sababu ya uvivu.

“Binafsi kila ninachokifanya huwa naweka bidii mbele nikiamini kuwa kuna mafanikio makubwa mbele yangu. Ubunifu, kujitambua, kutobweteka, kujiamini na kumcha Mungu ndiyo siri kubwa,’anasema.

‘Wanitosha’ ni kati ya nyimbo zinazomfanya muimbaji huyo kuwa kati ya waimbaji wa nyimbo za injili nchini wanaokuja kwa kasi kutokana na aina ya uimbaji wake.

Ucheshi na tabasamu usoni kwake ni moja ya sifa zinazomfanya aendelee kung’aa katika muziki wa Injili.

Alianza kusikika mwaka 2008, alipoachia wimbo wake wa kwanza uliyoibeba albamu yake ya ‘Niwe wa Kwanza’.

Lilian anasema siri ya mafanikio ya mwanamke ni kujitambua na kutobweteka kwa kuwa ‘ombaomba’ kwa yeyote, hata kama mtu huyo yupo tayari kutoa misaada.

“Kuwa ombaomba ni sawa na utumwa, utegemezi ni sawa nakuuza maisha yako kwa mwingine kwa sababu lazima kuna kitu atahitaji kwako. Atataka kuendesha maisha yako hivyo, hutaweza kufanikiwa kamwe,” anasema.

Anasema pamoja na muziki wa Injili, ameamua kujikita kwenye biashara za msimu kama vile kuku, samaki au nguo ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la familia yake.

Lilian ni miongoni mwa majina ya waimbaji wa muziki wa Injili nchini yaliyoteuliwa kuwania Tuzo za ‘Gospo Award’.

Anasema kilichosababisha aingie kwenye tuzo hizo ni wimbo wake wa ‘Wanitosha’ kupendwa zaidi jambo ambalo anamshukuru Mungu. Wimbo huo aliutoa mwaka jana, baada ya kutoa albamu yake ya pili ambayo ipo sokoni.

Kujikita kwenye biashara

Awali Lilian alikuwa akiishi mkoani Tanga ambako ndiko alikoanzisha kazi ya muziki ambako aliifanya albamu yake ya kwanza, kabla ya kuhamia jijini Dar es Salaam ambako anaendelea na kazi hiyo.

“Wapo wanaoamini muziki mikoani haulipi na wengine huwa wanadhani nilihamia Dar kwa sababu hiyo hapana. Moja ya vitu vilivyonisukuma kuja huku ni familia yangu na biashara,” anasema.

Anakiri kuwa ukweli ni kwamba kwa Tanzania muziki peke yake haulipi hivyo ni lazima ziwepo kazi nyingine zinazoweza kuchangia, kipato chake na familia yake.

Anawashauri wanamuziki wanawake, kutobweteka na majina na badala yake wafanye kazi hata wanazoona ni za kawaida ili kujiongezea kipato.

Nafasi ya mwanamke kwenye jamii

Liliana anasema mwanamke ndio msingi wa jamii imara na kwamba, ikiwa anashindwa kusimamia maadili ni dhahiri kuwa jamii itaporomoka.

“Kuna wakati nililazimika kusimamisha shughuli zangu zote zikiwamo za muziki kwa ajili ya malezi ya watoto, walipokuwa niliendelea na harakati zangu na nilifanya hivyo kwa makusudi kwa sababu nilihitaji kuwajengea wanangu msingi imara,” anasema.

Anasema maadili ya Taifa huanza kwenye msingi wa familia na kwamba, ikiwa wanawake watashindwa kusimama kwenye nafasi yao katika kuwalea watoto wao.