Wasomi, wadau wakubali Lugha ya Kiswahili itumike nyanja zote nchini

Muktasari:

  • Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) iliratibu mdahalo huo na kuhudhuriwa na mamia ya wadau na wapenzi wa Kiswahili waliofurika katika Ukumbi wa Nkrumah.

Wanazuoni na wadau wa Kiswahili hivi karibuni walikutana na kufanya mdahalo wa kihistoria kuhusu matumizi ya Kiswahili nchini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kwa pamoja, walitazama kama ni wakati muafaka kwa Kiswahili kutumika katika nyanja mbalimbali nchini.

Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) iliratibu mdahalo huo na kuhudhuriwa na mamia ya wadau na wapenzi wa Kiswahili waliofurika katika Ukumbi wa Nkrumah.

Balozi wa Heshima wa Kiswahili, Mama Salma Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi alisema Kiswahili kinaweza kutumika katika maeneo mbalimbali hivyo kinahitaji kuendelezwa. Mgeni rasmi, alibainisha, kama zilivyo lugha nyingine, Kiswahili bado hakijitoshelezi kwa kila jambo.

Ni kawaida kwa lugha nyingi kuazima maneno kutoka nyingine. “Hatutakuwa tumefanya jambo la ajabu ikiwa lugha yetu itaendelea kuchukua maneno kutoka katika lugha za kigeni pale inapobidi,” alisema.

Zipo pande mbili zinazolumbana kuhusu matumizi ya Kiswahili na kila upande una hoja zake. Alisisitiza lugha yetu haina budi kuenziwa na kupewa kipaumbele katika matumizi. Aliwapongeza marais wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua mbalimbali walizochukua kukiendeleza Kiswahili.

Dk Mkabwa Manoko wa Ndaki ya Kilimo na Uvuvi ya UDSM alijikita zaidi katika utoaji maarifa kwa mwanafunzi na uhusiano wake na utoaji wa huduma kwa wananchi baada ya kuhitimu masomo.

Alisisitiza kwamba, uwezo wa mwanafunzi kupokea na kuelewa kile anachofundishwa hutegemea lugha inayotumika kumfundishia. Akitoa mfano wa wanafunzi anaowafundisha, alieleza baada ya kuhitimu watakuwa wagani wanaotegemewa kuwahudumia wananchi.

Alisema mara kadhaa matatizo hutokea kwa sababu ya changamoto za lugha. Wahitimu hukabiliana na changamoto ya kutowatumikia wananchi ipasavyo kwa sababu wamefunzwa kwa Kiingereza ilhali wanahudumia kwa Kiswahili. Dk Manoko alinukuu tafiti za wataalamu wengine kutoka Ulaya na Afrika: “Wote wanaonyesha kujifunza kwa lugha ya kigeni humfanya mwanafunzi kukosa ubunifu, kupoteza uelewa na kutofaulu kwa kiwango cha juu.”

Kwa msimamo wake, alisema mabadiliko yafanyike na Kiswahili kitumike kwani wanafunzi wataelewa zaidi, watafaulu kwa kiwango cha juu na kumudu majukumu yao wawatumikiapo wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Adolf Mkenda alisema hapingi matumizi ya Kiswahili ila kinapaswa kujitosheleza kwanza.

Alitanabahisha kuwa kutokana na kutojitosheleza, hata watunga sera huamua kuwapeleka watoto wao nje ya nchi au shule za kimataifa kuepuka tatizo hilo.

Katika hoja hiyo, Dk Said Sima wa Idara ya Hisabati ya UDSM alisema: “Ni lazima tukubali kuanza kufundisha kwa lugha yetu hata kama kuna ugumu.”

Kwa uzoefu alioupata sehemu mbalimbali, alisema kumfundisha mwanafunzi kwa lugha anayoijua, kunamfanya aelewe masomo yake vizuri zaidi. Alitoa mfano wa Afrika Kusini ambako mtihani mmoja unatungwa kwa lugha mbili, Kiingereza na Kiafrikana na wanafunzi wanaruhusiwa kuchagua mtihani ulioandikwa kwa lugha wanayoipenda.

“Wale waliochagua uliotungwa kwa Kiafrikana walifaulu zaidi kuliko waliojibu kwa lugha ya kigeni,” alisema na kueleza kuwa alifanya utafiti katika shule moja ya sekondari jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa wale waliojibu mtihani uliotumia Kiswahili walifanya vizuri zaidi kuliko waliojibu wa Kiingereza.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Anna Mghwira alisema: “Lugha yoyote inaweza kutumika kufundishia ikieleweka.” Alipendekeza Kiswahili kikuzwe kwanza ndipo kianze kutumika.

Mhadhiri Mwandamizi chuoni hapo, Profesa Kitila Mkumbo alibainisha kuwa lugha yoyote inaweza kutumika kufundishia na kwamba si sababu ya kumfanya mtu afeli katika masomo yake. Alieleza, “Katika utafiti tulioufanya, tumepata sababu 15 za mwanafunzi kufeli katika masomo yake lakini lugha si mojawapo.”

Pia, profesa huyo alisema kujadili suala hilo ni udhaifu wa kukwepa Kiingereza badala ya kuchukua hatua za kukiboresha ili kukifahamu zaidi ya ilivyo.

Kwa upande wake Dk Bashiru Ally, alifafanua kuwa lugha zote ni sawa ingawa baadhi huona Kiingereza ni bora zaidi kuliko Kiswahili. “Hakuna lugha yenye hadhi zaidi ya nyingine,” alisema.

Alikumbusha, wakati fulani katika historia, Kiingereza kilikuwa duni kikilinganishwa na Kilatini au Kigiriki. “Jamii zilizowekeza katika lugha zake zimepiga hatua zaidi kimaendeleo. Kiswahili kitumike kwani ni lugha ya ukombozi,” alisema.

Profesa Abdalah Saffari alieleza kuna tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu matumizi ya Kiswahili na kuonyesha kina uwezo wa kuchukua jukumu hilo pasi mashaka. Alishutumu kudharau tafiti ambazo matokeo yake yangesaidia kuleta mabadiliko katika jamii yetu. Hata hivyo alitanabahisha: “Mabepari hawatakubali Kiswahili kitumike kwa kuwa kwao Kiingereza ni mradi.”

Dk Adolf Mihanjo wa UDSM alisema: “Hata siku moja huwezi kutenganisha maarifa na lugha ya binadamu.’ Aliifafanua kauli hiyo kuwa, katika historia ya lugha, nchi nyingi za Ulaya ulifika wakati ziliamua kuachana na Kilatini, lugha iliyotawala dunia kwa wakati huo na kuamua kuandika na kufundisha kwa lugha zao wenyewe ndipo yakatokea mapinduzi ya viwanda. Alisisitiza Kiswahili kitumike.

Profesa Kulikoyela Kahigi wa Tataki alisema muda mwafaka wa kutumia Kiswahili ikiwa ni pamoja na kufundishia, ulishapita. Alieleza: “Katika kufanya hivyo changamoto za istilahi hazikosekani lakini zimekuwa zikitatuliwa.”

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Shy-Rose Bhanji, alisema midahalo hii inahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote. Alisisitiza matumizi ya Kiswahili kwani ni lugha rasmi ya Bunge la Afrika Mashariki.

Alisema, yeye pamoja na wabunge wangine wamekipigania Kiswahili na jitihada zao ni endelevu. Alitoa wito kwa kila mmoja kukipenda, kukienzi na kukitukuza. Yeye anaona kwamba sasa ni wakati mwafaka wa Kiswahili kutumika katika nyanja anuwai bila kikwazo.

Wanafunzi wa shahada ya uzamivu wa Kiswahili kutoka Ghana na Zimbabwe walieleza kuwa wanaona fahari kukisoma Kiswahili. Walisisitiza kuwa ni lugha inayowaunganisha Waafrika wote hivyo hainabudi kuenziwa.

Waliwashangaa wanaokipinga na kushadadia lugha za kigeni. Aaron Mukandabvute alisema kuzipenda lugha za wengine wakati yetu ipo ni jambo la ajabu. Aidha, Ma Jun, mwanafunzi kutoka China alieleza namna Kiswahili kilivyo kiungo kati ya mataifa haya mawili na anaona umuhimu mkubwa wa kujifunza.

Mwenyekiti wa mdahalo huo, Profesa Martha Qorro alisema tafiti nyingi zimeonyesha Kiswahili kitumike kufundishia na Kiingereza kifundishwe kama somo lakini kiboreshwe katika ufundishaji wake.

Alibainisha kuwa ufundishaji wa Kiingereza ni tatizo nchini kwani walimu wengi wana uwezo mdogo kuwafundisha wanafunzi hata hivyo alisema Kiswahili pia hakiruhusiwi katika shule za sekondari kama lugha ya mawasiliano kwa wanafunzi.

Alifafanua, matumizi ya Kiingereza yanawatenga wasomi na jamii ambayo haiijui lugha hiyo tofauti na jamii nyingine zitumiazo lugha zake hivyo mawasiliano baina ya wasomi na wanajamii kuwa dhahiri.

Aliwapinga wanaosema kutumia Kiingereza ni kujiweka karibu na mataifa mengine duniani kwa kueleza kuwa darasani hakuna suala hilo. “Mwanafunzi akifundishwa kwa Kiswahili na akazielewa lugha nyingine, dhana ya umataifa inabaki palepale. Mwanafunzi hujifunza vyema lugha ya pili au ya tatu anapokuwa na msingi bora katika lugha yake,” alisema.

Alisisitiza, kujua Kiingereza si kuelimika na kuwataka watu kutenganisha elimu na lugha hiyo. “Elimu itolewe kwa lugha ambayo wanafunzi wanaielewa.,” alisisitiza.

Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya, alitanabahisha kuwa, Kiswahili kimepiga hatua kubwa. Alisema: “Katika mihimili mitatu ya serikali, bunge na serikali hutumia Kiswahili; changamoto bado ipo katika mhimili wa mahakama.”

Hata hivyo, alieleza kwamba jitihada zinafanyika ili mhimili huo ufike pahali utumie Kiswahili. Alieleza kuwa jitihada zinazofanywa za kukiendeleza Kiswahili, bado kitapigwa vita kwa sababu maendeleo yake yanahofiwa kuwa yataondoa masilahi ya watu.

Alisisitiza kuwa, ili kufanikisha azma ya matumizi ya Kiswahili katika nyanja zote, wadau wa Kiswahili hawana budi kuongeza kasi, kuweka mikakati, serikali kutenga fedha ili kuwezesha mchakato wa matumizi ya Kiswahili.

Lakini, la muhimu zaidi ni sekta na wizara zote kushirikiana katika kufanikisha jamo hili. Alieleza pia kuwa, Wizara ya Elimu itashirikiana na Taasisi ya Elimu kuangalia machapisho ya Kiswahili yaliyoandikwa ili kuendeleza jitihada zinazofanywa.