Wasomi wasiwe makuwadi wa umasikini

Baadhi ya wahitimu wa elimu ya juu waklwa kwenye mahafali. Wasomi wanapaswa kuwa dira ya kuwaongoza Watanzania kutoka kwenye umasikini. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Maneno hayo kimsingi yanatafsiri kubwa kwamba chuo kikuu ni mahali panapostahili kuitumikisha akili kwa asilimia kubwa, kwa kuamua kufikiri kwa undani juu ya kila jambo.

Alipokuwa akizindua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwalimu Julius Nyerere alisema:

Chuo kikuu ni mahali ambako watu wanaandaliwa kuwa na akili ya kujitegemea. Pia ni mahali ambapo panafanya msomi awe mtu wa kuchanganua mambo na kutatua changamoto zinazomkabili kisayansi, kinyume na hapo hicho sio chuo kikuu’

Maneno hayo kimsingi yanatafsiri kubwa kwamba chuo kikuu ni mahali panapostahili kuitumikisha akili kwa asilimia kubwa, kwa kuamua kufikiri kwa undani juu ya kila jambo.

Msomi na hasa mwanachuo anatazamiwa kuwa mtu wa mtazamo chanya katika kutanzua mambo tofauti na yule asiyefikia ngazi hiyo.

Mara zote msomi anatakiwa kutafuta maarifa mapya kila uchao ili kujua namna sahihi na iliyo bora katika kuyakabili mazingira yanayomzunguka. Kumbe msomi lazima ajenge hulka ya kupenda kusoma sana vitabu, kwani atapata maarifa mengi tena bila gharama kubwa!

Mtu anayesoma vitabu vya kumjenga, kamwe hawezi kufanana na yule asiyefanya hivyo kwani hawa ni watu wawili tofati kabisa kimtazamo.

Mathalani, inampasa msomi kuwa mtu wa kubaini zaidi fursa kuliko matatizo tu bila kuyatafutia suluhisho.

Mara nyingi wasomi wetu wamekuwa si watu wa uthubutu katika kufanya yale ambayo yanaweza kuwa na manufaa na tija katika kujikomboa na kuwa huru kifikra na kiuchumi.

Wengi tunaamini kuwa msingi wa mafanikio ni fedha, na hivyo husubiri mwaka mpya wa fedha Serikali iongeze mishahara na mengineyo, lakini huu ni mtazamo hasi kwani msingi wa mafanikio si fedha pekee bali ni nidhamu na mipango ya kutimiza kile unachotaka kukitekeleza.

Niulize maswali kadhaa inachukua kiasi gani cha fedha kuanzisha wazo kichwani? inachukua fedha ngapi kuweka mipango katika karatasi? Inachukua kiasi gani cha fedha kwenda kujifunza kwa waliofanikiwa kuhusiana na jambo unalotaka kulifanyia kazi?

Niongeze, inachukua kiasi gani kujitolea kufanya kazi fulani bure upate uzoefu wa ujuzi unaotaka kuwa nao maishani?

Ni rahisi sana kuanza na wazo na kuliwekea miundombinu kulifikia na mara zote anza polepole, lakini uwe na malengo ya kwenda mbele.

Changamoto ameumbiwa mwanadamu, hivyo kukata tamaa ni dhambi kubwa na kwa kadri siku zinavyokwenda tumia matatizo kama fursa kwako. Kulalamika siku zote ni laana, na laani hiyo huota usugu na kujenga kansa ya kuwa mwoga wa kuthubutu katika maisha.

Siku za nyuma kulikuwa na msemo; mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe’. Mimi nasema mtaji wa masikini ni nidhamu ya kuutumia ubongo vizuri na kuwa na dira ya kujua unataka kwenda wapi na kwa namna ipi.

Bila kufanya hivyo nashawishika kuchukua maneno ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliyesema: “ Itakuwa mtu huyo alipewa ubongo kimakosa kwani kwake yeye uti wa mgongo pekee ungemtosha.”

Mbali na changamoto za kimasomo, ilitazamiwa kuwa chuo kikuu pawe ni kitovu cha tafiti nyingi ambazo kimsingi zingeweza kusaidia kukiendesha chuo na nchi kwa ujumla, kwani tafiti nyingi huibua mambo mapya na mazuri kwa uhai wa vyuo na taifa.

Kwa mfano, moja kati ya mahitaji ya wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia ilikuwa ni dawa ya kuoshea vidonda wanavyopata wapiganaji.

Wamarekani wakatumia fursa hii kuanzisha Chuo Kikuu cha Edinburgh ambacho kilianzisha dawa ya kuosha vidonda iitwayo ‘Eusol’ neno ambalo kirefu chake ni ‘Edinburgh University Solution of Lime.

Mpaka leo dawa hiyo imepewa jina la chuo chao, chuo kikuu cha Ricoh waligundua mashine ya kuchapishia karatasi wakaipa jina la chuo chao yaani “Richo machine.

David Gestetner, mzaliwa wa Hungary 1879 aligundua mashine ya kurudufishia karatasi akaiita Gestetner. Hizo zote ni fursa zilizopatikana na vyuo hivyo kupitia matatizo au changamoto zilizokuwa zikiwakumba.

Kwa wenzetu kila penye tatizo waliligeuza kuwa fursa. Na katika vyuo hivi bila shaka uhusiano katika muktadha wa taaluma baina ya mwalimu na mwanafunzi ni mazuri kwani wanategemeana.

Tofauti na mahali pengine, ikiwamo hapa kwetu kwani asilimia kubwa wawezeshaji hawana ushirikiano na wengine.

Wanachotaka wao ni kuthaminiwa kuliko kuthamini, kuogopwa na kutaka watambulike kwa nafasi zao za usomi hata kama wakati mwingine hawana sifa na vigezo stahiki

Nitoe wito kwa wasomi kuacha tabia ya kulaumu tu Serikali au mtu yeyote, tafuteni njia sahihi kuliko kulaumu tu.

Kulaumu hufanya akili iwe na mgandamano wa fikira za uovu, lakini kama umetafuta njia sahihi ya kulitatua jambo, utaona mbele kuna nuru na mwanga.

Frank Chalamila ni mwalimu, mtafiti na mshauri binafsi mambo ya elimu.

0717-707187

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz