Yahya Jammeh atajificha wapi?

Rais wa Gambia aliyemaliza muda wake, Yahya Jammeh akiondoka kwenye kituo cha kupigia kura katika mji wa Bangul Desemba Mosi, mwaka jana. Picha ya AFP

Muktasari:

Mbwembwe za Bunge la Gambia za kumwongezea siku 90 madarakani hazitafua dafu mbele ya ukweli kuwa muda wake umekwisha.

Rais wa Gambia, Yahya Jammeh muda wake umemalizika lakini anaendelea kung’ang’ania kubaki madarakani.

Kiongozi huyo hana pa kujificha kwani muda wowote kutokea sasa atakimbia madarakani.

Mbwembwe za Bunge la Gambia za kumwongezea siku 90 madarakani hazitafua dafu mbele ya ukweli kuwa muda wake umekwisha.

Mkwara wake wa kutangaza hali ya hatari haumaanishi chochote mbele ya vikosi vya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) vitakavyoongozwa na Senegal na Nigeria.

Tayari mawaziri watano wameshajiuzulu kumkimbia, baadhi ya mabalozi hawamuungi mkono kabisa na mbaya zaidi mshirika wake wa karibu ambaye ni Makamu wa Rais wa Gambia ameshajiuzulu wadhifa huo kabla muda wa uongozi wa Jammeh haujamalizika rasmi juzi. Jammeh amebakia mwenyewe na jeshi lake. Je, jeshi la Jammeh litahimili vishindo vya majeshi ya Ecowas?

Tulivyomng’oa Idd Amin

Kwa sababu Jammeh amejificha nyuma ya kichaka cha jeshi lake, naomba niliite jeshi hilo ‘kijeshi’. Tukumbushane kuwa, miaka ya mwishoni mwa 1970 wakati Jeshi la Tanzania liliivamia Uganda na kuikomboa kutoka mikononi mwa Idd Amin, Tanzania ilipata hasara kubwa kijeshi, kiuchumi na kiusalama.

Hasara na hatari zilizoikabili Tanzania zilikuwa za lazima kabla ya vita ya Uganda, wakati wa vita na baada. Baada ya vita ya Uganda, athari za vita hiyo kiuchumi zimedumu hadi leo, lakini hatari za kiusalama na kiuchumi zimepungua au hazipo kabisa.

Wakati ule, kutangaza vita dhidi ya Uganda ilikuwa ni jambo hatari zaidi. Uhatari huo ulitokana na ukweli kwamba Uganda ni nchi kubwa, ilikuwa na jeshi kubwa, ilikuwa na vifaa vya maana kijeshi na jeshi hilo lilikuwa na nidhamu kubwa.

Unaweza kusema, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza vita dhidi ya nchi yenye jeshi imara na lenye nguvu kukaribiana na Tanzania, hiyo ilikuwa hatari kubwa. Hatari nyingine ilikuwa ni uungwaji mkono wa Idd Amin kutoka kwa baadhi ya marafiki zake duniani, akiwamo aliyekuwa Rais wa Libya, Kanali Muamar Gadaffi.

Gadaffi alimuunga mkono Idd Amin kwa kila njia na yapo mataifa mengine yaliyomsaidia na kwa hiyo Tanzania ilikuwa kwenye wakati mgumu.

Kumbukumbu hiyo ya vita dhidi ya Idd Amin ituandae kufikiria athari ambazo nchi inaweza kupata inapoamua kuongoza operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya nchi nyingine huru yenye jeshi lenye nguvu na utii kwa Rais aliyepo madarakani kama ilivyo kwa Jeshi la Gambia linavyomtii Jammeh.

Jeshi la Gambia

Historia hiyo ya Tanzania kumwondoa Nduli Amin haifanani kabisa na ya majeshi ya Ecowas kumwondoa Jammeh. Nitalizungumza jambo hili kwa muktadha wa kijeshi. Jammeh hana jeshi la kumtisha mtu, ana ‘kajeshi’ ambako hakawezi kupambana na jeshi.

Jeshi la Gambia lina wanajeshi wapatao 1,000. Kikosi cha majini kina askari 125, cha anga kina askari 100 na cha ardhini askari takriban 700. Jeshi la Gambia lina magari ya kivita pamoja na ya deraya takriban 12 na nyingi kati ya hizo ziko chini ya kikosi cha ulinzi wa Rais.

Wana ndege sita za kivita zikiwamo Su-25 Frogfoot kutoka Georgia, mbili aina ya AT- 802A za kusafirisha vifaa vya kijeshi, moja ya kivita aina ya Il-62M Classic, moja ya kivita aina ya Skyban 3M na moja ya kivita mahsusi kwa shughuli za ulinzi wa anga.

Kwa upande wa jeshi la majini, wana boti tatu za kivita, ya kwanza ni Peterson kwa ajili ya kukagua malindo na mbili ziendazo kasi zilizotengenezwa nchini Hispania.

Bajeti ya Jeshi la Gambia kwa mwaka mmoja ni Dola1 milioni za Marekani. Hii ni moja ya bajeti ndogo kabisa za jeshi duniani. Kwenye viwango vya kimataifa vya kijeshi, Jeshi la Gambia linashikilia nafasi ya tisa kutoka mkiani, yaani kama dunia inapambanisha majeshi kutoka nchi 200 duniani, Gambia inashika nafasi ya 191 ikishindana na majeshi madogo kama la Bahamas.

Jeshi la Senegal

Ardhi itakayotumiwa na nchi washirika wa vikosi vya majeshi ya Ecowas ni Senegal na Jeshi la Senegal ndilo litaongoza vikosi mbalimbali kufanya operesheni ya kumuondoa Jammeh.

Ukiachilia mbali mchanganyiko wa majeshi ya nchi za Ecowas, Jeshi la Senegal peke yake lina uwezo wa kumwondoa Jammeh ndani ya muda usiozidi wiki moja.

Jeshi la Senegal lina askari 19,000. Mara 10 ya askari wa Jeshi la Gambia. Bajeti la jeshi hilo ni Dola289 milioni za Marekani, hii ni mara 289 ukiilinganisha na bajeti inayolihudumia Jeshi la Gambia kwa mwaka mmoja.

Jeshi la Senegal limeshiriki kwenye operesheni nyingi za kulinda amani na za kivita ndani na nje ya nchi hiyo. Hilo ni moja ya majeshi yenye uwezo mkubwa kabisa Afrika likiwa na magari ya deraya, magari ya kivita yenye silaha na silaha kubwa za kivita takriban 1,000.

Senegal wana dazani nyingi za ndege, boti na meli kadhaa za kivita. Hii ni nchi iliyojipanga kijeshi huku makomandoo wake wakipata mafunzo ya kutosha kutoka Ufaransa na Marekani. Kwenye viwango vya uwezo wa kijeshi Afrika, Senegal iko kati ya nchi 10 bora zilizojipanga kijeshi.

Kombinesheni ya Ecowas

Majeshi ya nchi za Ecowas yakiipa nguvu Senegal, Jammeh atakimbia madarakani mwenyewe, hataweza kuhimili mapambano dhidi ya majeshi yenye nguvu.

Tayari Nigeria imeweka bayana kuwa makomandoo wake 200 watajiunga na vikosi vya Senegal, hii itakuwa balaa kubwa kwa Jammeh ambaye kwa hakika askari wake wanahesabika, vifaa vyake vya kijeshi vinahesabika na hana msaada wa Taifa kubwa linalojipanga kumsaidia.

Jammeh atakuwa na chaguo moja tu, kutafuta nchi ya kukimbilia na kuelekea huko haraka na kwa hali hiyo atajikosesha uhalali hata wa kuwa raia mwema ndani ya Gambia. Kombinesheni ya Ecowas ni moto mkali usiosogeleka wala kuguswa na Jammeh hawezi kuuhimili.

Rais mteule Adam Barrow

Wakati Rais wa Marekani, Donald Trump ameapishwa jana huko Marekani, tayari Adam Barrow, baunsa mstaafu huko London, Uingereza, kaapishwa kuwa Rais wa Gambia. Barrow ambaye yupo nchini Senegal kwa sababu za kiusalama alikuwa na chaguo la kuapishiwa ndani ya ardhi ya Gambia, lakini si kwenye mji mkuu wa nchi hiyo.

Chaguo jingine na ambalo limetimizwa ni kumwapishia kwenye ubalozi wa Gambia uliopo Senegal ambao kidiplomasia na kisheria ni ardhi ya Gambia.

Hivi sasa Barrow ni Rais wa Gambia aliyepo nje ya nchi hiyo na muda siyo mrefu atakuwa na uhalali wa jumla ikiwa ni pamoja na kurudi kwenye Ikulu ya Banjul baada ya majeshi ya Ecowas kumaliza kazi yake.

Barrow anatarajia kuwatumia watu kadhaa waliowahi kushirikiana na Jammeh kwenye utawala uliopita. Watu hao ni pamoja na baadhi ya mabalozi wanaoiwakilisha Gambia katika mataifa mengine ambao wameweka msimamo wa kutomtambua Jammeh kama Rais wa Gambia tangu Januari 19.

Jeshi la Gambia lifanyeje?

Jeshi la Gambia lina chaguo moja mbele yake. Kujiweka pembeni kabisa. Halina uwezo wa kuendesha mapambano yoyote kumlinda Jammeh. Kama mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Gambia ana busara za kijeshi, atachukua hatua ya kuwasihi askari wake watulie kambini, wasijaribu kupambana na majeshi ya Ecowas. Hiyo itakuwa ahueni kwa askari hao ambao wataendelea kulitumikia jeshi hata baada ya ujio wa Barrow madarakani. Pia busara ya mkuu huyo wa majeshi itaiepushia nchi uharibifu wa miundombinu na makazi ya watu na vifo vya raia wasio na hatia.

Kwa sababu ni lazima majeshi ya Ecowas yashinde, mkuu wa majeshi ya Gambia anaweza moja kwa moja kushtakiwa na kufungwa iwapo jeshi lake litasalimu amri baada ya kujihusisha na mapambano dhidi ya vikosi vya Ecowas.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, mtafiti na mwanasheria. Simu; +255787536759/ Baruapepe; [email protected]/ Tovuti; juliusmtatiro.com.