Yaliyojificha juu ya tofauti za mtoto, mama wa kambo

Muktasari:

  • Kama msamiati wenyewe unavyojieleza mtoto anayeishi au kulelewa na mama huyu naye huitwa mtoto wa kambo, hutokea pale wazazi wa awali wa mtoto huyo au watoto hao wanapoamua kutengana kwa makusudi au kwa kifo kumchukua mmoja wao, hivyo mwanaume anapooa huyo mama hufahamika kama mama wa kambo kwa watoto aliowakuta kwa mumewe.

‘Mama wa kambo’ siyo msamiati mgeni kwa watu wengi. Ni neno ambalo limekuwa likitumika zaidi kwenye jamii likiwa na maana ya mama anayemlea mtoto wa mume wake au mwenza.

Kama msamiati wenyewe unavyojieleza mtoto anayeishi au kulelewa na mama huyu naye huitwa mtoto wa kambo, hutokea pale wazazi wa awali wa mtoto huyo au watoto hao wanapoamua kutengana kwa makusudi au kwa kifo kumchukua mmoja wao, hivyo mwanaume anapooa huyo mama hufahamika kama mama wa kambo kwa watoto aliowakuta kwa mumewe.

Mama huyu hupaswa kubeba jukumu zima la malezi ya mtoto au watoto na kuwatendea kama vile anavyoweza kuwafanyia watoto wake aliowazaa.

Katika jamii nyingi mama wa kambo anatafsiriwa kama mwanamke mnyanyasaji ambaye anafanya kila linalowezekana kumpa wakati mgumu mtoto au watoto anaowalea.

Hali hiyo imejengeka vichwani mwa watoto hivyo nao kujikuta wakiishi kimtego mtego na mama zao.

Tafiti mbalimbali zimefanywa na wataalamu wa saikolojia zinaonyesha kuwa watoto wengi wanaolelewa na mama wa kambo, maisha yao ni tofauti na wale wanaoishi na mama zao wa kuwazaa.

Wanasaikolojia hao kila mmoja kwa wa namna yake wamejaribu kuizungumzia dhana hii lakini bado inaendelea kuonekana mtambuka.

Mwandishi Kelly Chaplin kupitia kitabu chake cha I’am a Wicked Stepmother’ amezungumzia uhusiano uliopo kati yake na mtoto wa kambo na changamoto anazokutana nazo kumlea mtoto asiyemzaa.

Kupitia kitabu hicho na machapisho mengine ni dhahiri wenzetu wa magharibi, ni nadra kwa mtoto kumkubali mama wa kambo na akaishi naye kama ambavyo angeishi na mama yake mzazi.

Mtaalamu wa masuala ya saikolojia nchini Modesta Kamonga anasema chuki, uwoga na hofu ambao mara nyingi hujijenga katika kichwa cha mama na mtoto ni chanzo cha migogoro mingi katika familia hizi.

Anasema jamii imechangia kwa kiasi kikubwa kujenga hiki tunachokiita ‘mama wa kambo’ huku ikihusisha na ukatili na hali ya kukosa upendo kwa mtoto.

“Kwa upande wa mtoto hasa pale anapotambua kuwa anayeishi naye siyo mama mzazi, kichwani mwake anaweza kujenga chuki akiamini kwamba mwanamke huyo ndiyo chanzo cha kuivuruga familia yao, ”anasema.

Pili anaweza kuwa na hofu ya maisha na usalama endapo mama huyo atakuwa anamtesa au kumfanyia vitendo vitakavyomfanya aone utofauti.

Anasema kinamama wengi wana ile hali ya kujihami hasa wanapokuta watoto wanaojitambua. Hapa mama anaamua kumtesa mtoto kama njia ya kujilinda ili siku moja asiweze kwenda kinyume na matakwa yake.

Anafafanua kuwa pamoja na wote wawili kuwa chanzo, baba ana nafasi yake katika kuhakikisha mke na mtoto wake wanaishi kwa amani, upendo na utulivu.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Anna Maganga, msichana aliyelelewa na mama wa kambo ambaye anakiri kuwa baba ana nafasi kubwa kuhakikisha mtoto haoni tofauti ya kuishi na mama asiyemzaa.

“Kuna wakati unaweza kuona utofauti fulani lakini baba yangu alikuwa haruhusu kabisa hali hiyo ijitokeze, hivyo ilitulazimu mimi na mama tuwe kwenye mstari mmoja na mpaka sasa ni nadra kujua kwamba hajanizaa yeye” anasema Maganga.

“Nilianza kulelewa na mama wa kambo nikiwa na miaka minne, ukiondoa kasoro za hapa na pale za kibinadamu sikuwahi kujihisi mpweke kwani hata nilipokuwa na wadogo zangu bado mama alitulea kwa usawa”.

Anaongeza kusema kuwa: “Baba alikuwa akifanya kila analoweza kutuweka watoto wake pamoja bila kutubagua hali iliyochangia tupendane wenyewe kwa wenyewe kama ndugu na tumpende mama yetu pia,” anasema Maganga.

Wakati Maganga akifurahia kuwa na mama wa kambo hali ni tofauti kwa Janeth Mromi kutoka na machungu aliyopitia kwenye ukuaji wake.

“Dah hata sijui nieleze vipi kwa kifupi nimeteseka na kwa bahati mbaya baba alikuwa hataki kuelewa changamoto nilizokuwa nakutana nazo nyumbani kwani alimuamini mama kwa kila kitu:

Nakumbuka mateso yalisababisha nitoroke nyumbani na kwenda kwa shangazi maana nilikuwa napigwa licha ya kufanya kila alichokitaka mama, ”anasema.

Ushuhuda huo wa Mromi unaakisi maisha ya watoto wengi na mama zao wa kambo katika jamii nyingi za Kiafrika.

Jarida la malezi la Parents linaeleza tafiti nyingi zilizofanyika zinaonyesha mara nyingi mama na mtoto wa kambo wanashindwa kuelewana kutokana na kukosekana ukaribu kati yao.

Kwa mujibu wa jarida hilo ni muhimu mama akajenga ukaribu na mtoto kwa kumuonyesha mapenzi na wakati mwingine imani juu yake.

Inashauriwa pia mama kumpa mtoto nafasi ya kuwa na baba yake. Mama hatakiwi kumuwekea vikwazo mtoto pindi anapotaka kuzungumza au kumkaribia baba yake wakati wowote ule.

Kwa kufanya hivyo itasaidia kumjengea mtoto hali ya kujiamini na kujenga urafiki na mama hali itakayomfanya kuwa huru muda wote na kujichanganya na wenzake kama wapo.

Mama anapokuwa kwenye nyumba bila kujali watoto anawalea ni wa kwake au siyo wa kwake, bado suala la maadili lipo mikononi mwake. Mtoto anayekulia mikononi mwake anatakiwa kupewa maelekezo na mafunzo ili aweze kuishi vyema na jamii inayomzunguka.

Licha ya mitazamo mbalimbali inayoelezwa na kuhusu mama wa kambo, mtoto anapaswa kutimiza wajibu wake. Baadhi ya watoto baada ya kuambiwa na ndugu upande wa mama yake mzazi kuhusu mama anayemlea siyo mzazi wake wengi wao huanza kuonyesha dharau na kiburi.

Wanazuoni mbalimbali wanaonyesha upo uwezekano wa mtoto kuishi na mama wa kambo iwapo atatimiza wajibu wake kama mtoto, huku kukiwa na ushirikiano wa karibu baiana ya mama na baba wa mtoto. Mtazamo uliotolewa na Mromi, wapo baadhi ya wazazi huweka uadui na watoto wanaoletewa kuwalea kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kukwepa tabia za mtoto ambazo anatoka nazo kwa mama yake.

Kumekuwapo na matukio mbalimbali yanayoripotiwa polisi hapa nchini yanayohusisha watoto wa kambo kuteswa, Hali hiyo huwakuta zaidi watoto walio chini ya miaka kumi kwa kuwa ni umri ambao angalau anaweza kujielezea.

Mwanasaikolojia Kamonga anatazama pande mbili kwa kuonyesha chuki inayokuwa imetawala kwa mama au kwa mtoto. Hali hiyo inapokomaa ndiyo husababisha mama kuamua kumnyanyasa mtoto huku mtoto naye akijibu mapigo kwa kufanya tabia za kuchukiza.

Mambo muhimu ya kuzingatia

Mtaalamu wa Saikolojia wa Marekani Dk Susan Macdonald kupitia kitabu chake ya “How to live with a Step-child” anasema mama anapokuwa na mtoto wa kambo ni jukumu lake kumuonyesha upendo na kumuelekeza mwenendo mzuri anaopaswa kuufuta.

Iwapo kuna mabadiliko yoyote kutoka kwa mtoto ni vyema kumshirikisha baba yake mapema ili kupata ufumbuzi kwa pamoja.

“Ni vyema mama anayemlea mtoto kumfanya ajisikie kama sehemu ya familia kuliko kumtamkia maneno ambayo yatakaa kichwani mwake na yasiwe msaada kwenye maisha yake:

“Mtoto aliyelelewa na wazazi anapaswa kuwasikiliza wazazi wake bila kujali kama ni mama wa kambo. Watoto pia wanapaswa kuepuka tabia za uongo ili kutunza amani ya familia, ”anasema Macdonald.

Ni vyema mtoto akajengewa misingi ya kukua katika misingi ya dini, hali hiyo itamwepusha na kiburi na dharau jambo ambalo ni sumu katika makuzi yake.