Thursday, May 18, 2017

Yanayopaswa kufanywa kuimarisha mapato ya kodi

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma na Elimu ya

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Richard Kayombo akitoa semina kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hivi karibuni ikiwa ni sehemu za juhudi za kuelimisha umma kuhusu shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo. Picha ya Mtandao.   

 Serikali ina jukumu la kugharamia huduma za umma kama elimu, afya, maji, ulinzi na usalama, na miundombinu kwa ujumla wake. Huduma hizi hugharimu fedha zinazotengwa kwenye bajeti kutoka vyanzo mbalimbali.

Katika utekelezaji wa bajeti husika, huwa kunakuwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha mapato kutokidhi matumizi yaliyoainishwa, hivyo kuwapo kwa nakisi, yaani kutotosheleza kwa bajeti.

Mapato yanayokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali yamekuwa chini ya makadirio kwa miaka mingi. Utafiti unaohusu kodi uliofanywa na Taasisi ya Ushiriki (TIP) kutoa mwanga kuhusu changamoto na suluhu kuhusu mapato ya kikodi katika bajeti za Tanzania kwa ujumla na bajeti ya 2017/18 kimahususi.

Utafiti wa TIP

TIP ni kufupi cha Taxation, Institutions and Participation, mradi wa utafiti wa mambo ya kodi unaofadhiliwa na Baraza la Utafiti la Norway. Utafiti huu unafanyika Tanzania, Zambia na Angola. Mambo makuu ni kuona namna nchi hizi zinavyoweza kuongeza mapato yake ya kodi.

Mwandishi wa makala haya ni mtafiti mkuu kwa Tanzania katika mradi huu ambao unatekelezwa kwa mwaka wa tatu, ambao ni wa mwisho. Utafiti unasimamiwa na Taasisi ya Christian Michelsen Institute (CMI) ya Bergen, Norway ukiongozwa na Profesa Odd-Helge Fjeldstad.

Vyanzo fedha za bajeti

Tanzania hupata fedha za bajeti kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi. Vyanzo vya ndani ni vya kodi na visivyo vya kodi. Vyanzo vya nje ni misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo na mikopo kutoka vyombo vya fedha.

Chanzo kikuu cha ndani ni kodi. Utafiti uliowahi kufanywa ukiwamo wa TIP unaonyesha chanzo hiki hakitoshelezi mahitaji kwa sababu mbalimbali.

Kodi kama chanzo cha fedha za bajeti, kwa miaka mingi, imetoa chini ya asilimia 50 ya kiasi halisi kinachohitajika kutokana na sababu nyingi zilizopo. Kodi hizi zinajumuisha ya Ongezeko la Thamani (Vat), ambayo ni asilimia 18, kodi ya mapato ya kampuni asilimia 30, kodi ya zuio asilimia tano kwa wenyeji na asilimia 15 kwa wageni.

Nyingine ni kodi ya mafunzo ya ufundi (SDL) asilimia 4.5 ya gharama zote za mishahara ya mwajiri na kodi ya mshahara (Paye). Pamoja na mambo mengine, utafiti wa TIP umegundua changamoto kadhaa katika chanzo hiki.

Wigo finyu wa kodi

Tanzania ina wigo mwembamba wa kodi. Maana yake ni kuwa inakusanya kodi kutoka vyanzo vichache vya kodi. Hii inafanya kuwapo kwa wastani mdogo kati ya kodi na pato ghafi la Taifa.

Wakati baadhi ya nchi katika ukanda huu zikifikia wastani wa asilimia 16, Tanzania inakadiriwa kuwa na asilimia 13. Pia, idadi ya watu wanaolipa kodi ni ndogo kulinganisha na wanaotakiwa kufanya hivyo.

Pamoja na mambo mengine, kuna sekta kubwa isiyo rasmi isiyolipa baadhi ya kodi hasa ya mapato. Hata hivyo, waliopo katika sekta hii wanatumia bidhaa na huduma za umma kama wafanyavyo wanaolipa kodi.

Wigo finyu uliopo unafanya wachache walipe kodi hivyo kusababisha utitiri na viwango vikubwa. Hii siyo afya kwa uchumi kwa ujumla na kwa walipa kodi husika kimahusus.

Suluhu ya changamoto hii ni kupanua wigo wa kodi. Hii inaweza kufanyika kwa kuhakikisha kuwa kila anayepaswa kulipa kodi anafanya hivyo. Wigo wa kodi unaweza pia kupanuliwa kwa kukuza na kuongeza shughuli za uchumi na biashara.

Utitiri wa kodi

Walipa kodi nchini wanakabiliana na utitiri kwenye kila sekta na shughuli za biashara. kuna kodi nyingi tofauti ambazo ni changamoto katika utayari na uwezo wa kuzilipa.

Pamoja na wingi wa kodi, changamoto nyingine ni kutokuwapo dirisha moja la kulipa kodi zote mara moja. Kwa mlipaji, kwenda sehemu tofauti ni usumbufu kwani unagharimu muda hata fedha wakati mwingine.

Hivyo, licha ya utitiri uliopo, kutokuwapo kwa sehemu moja ya kulipia kodi hizi ni changamoto nyingine. Utafiti wa TIP unapendekeza kupunguzwa kwa kodi na kuziunganisha baadhi kwenye dirisha moja ambako zitalipwa.

Viwango vya juu

Viwango vya juu vya kodi ni changamoto ya jumla kwenye sekta karibia zote. Viwango hivi hupunguza fedha inayobaki kwa mlipaji. Kama ni kodi ya mapato ya kampuni au mwajiriwa, hupunguza mapato yake baada ya kodi.

Kwa kodi za matumizi kama vile Vat, hupunguza utayari na uwezo wa kutumia bidhaa na huduma hivyo kuathiri mwenendo wa biashara na uimara wa uchumi ikiwamo uwezo wa kupanua wigo wa kodi.

Wingi na utitiri wa kodi huathiri kwa namna hasi uwezo na utayari wa kulipa kodi na huweza kusababisha ukwepaji. Ni changamoto kuweka viwango vidogo vya kodi kwa nchi inayotaka mapato makubwa.

Hata hivyo, viwango vidogo vinaweza kuongeza ulipaji bila shuruti na kupunguza ukwepaji hivyo kupata fedha nyingi kuliko kuwa na viwango vya juu ambavyo ni wachache wanaotekeleza kwa hiyari. Changamoto ni kuwa na uthubutu wa kushusha viwango.

Ushirikishaji

Utafiti wa TIP umegundua ushirikishaji wa jamii katika masuala kadhaa ya kodi ni muhimu. Hii inajumuisha katika kufanya uamuzi wa kisera, kisheria, utaratibu na utendaji katika mambo ya kodi.

Haya ni pamoja na aina za kodi na viwango vyake bila kusahau muda wa kuanza kutoza. Hili ni kati ya jambo lililojitokeza katika utafiti wa TIP kuhusu Sheria ya Vat ya mwaka 2014.

Walipa kodi wanahitaji kushirikishwa zaidi kuhusu mambo kadhaa yaliyomo kwenye sheria hii. Haya ni pamoja na namna ya kutoza kodi hii kwa baadhi ya sekta na muda wa kuanza kutoza.

Elimu ya kodi

Kati ya changamoto zinazochangia kutopatikana fedha za kutosha ajili ya bajeti, ni elimu ndogo ya kodi. Hii inawahusu baadhi ya walipa kodi ambao hawana elimu ya kutosha kuhusu mambo ya msingi ya kodi.

Mambo haya ni kujua kodi gani zinatakiwa kulipwa, aina na viwango vya kodi, muda na utaratibu wa kulipa na mahali pa kulipia kodi husika. Pia, kuna upungufu wa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na namna ya fedha hizo zinavyotumika.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya juhudi kubwa kutoa elimu ya mlipa kodi. Hata hivyo, elimu inahitajika na inatakiwa kuwa endelevu kwa kuifanya kuwa mtambuka katika mitalaa yote, kuanzia ngazi za chini za elimu. Hii ni pamoja na kuwa na klabu nyingi za kodi shuleni na vyuoni. Pia, mlipa kodi anatakiwa kujua ni kwa vipi kodi anayolipa inamrudia kwa maana ya kuwekezwa katika mambo yanayomgusa moja kwa moja.

-->