Yapo masuala ya kuzingatia kabla ya kuwekeza katika soko la hisa

soko la hisa wakiwa kazini. Shughuli zote za uuzaji na ununuzi wa hisa hufanyika kwa mawakala ambao mara zote huwa na taarifa sahihi za kampuni zilizoorodheshwa sokoni. Mnunuzi hupewa cheti maalumu cha umiliki. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Hisa zake ziliwekwa sokoni kwa mara ya kwanza na zimekuwa zikiuzwa kuanzia Machi 9 hadi Aprili 19 dirisha hilo litakapofungwa.
  • Wakati hisa za kampuni mbalimbali zikiuzwa ni vizuri kuelimisha umma kuhusu jambo hili ambalo kwa kiasi fulani bado ni geni kwa wengi.

Kati ya mambo makubwa ya kiuchumi na kibiashara yaliyotokea Tanzania kwa Februari na Machi, 2017 ni mauzo ya hisa za kampuni mbalimbali. Miongoni mwa kampuni hizo ni ya simu za mkononi, Vodacom.

Hisa zake ziliwekwa sokoni kwa mara ya kwanza na zimekuwa zikiuzwa kuanzia Machi 9 hadi Aprili 19 dirisha hilo litakapofungwa.

Wakati hisa za kampuni mbalimbali zikiuzwa ni vizuri kuelimisha umma kuhusu jambo hili ambalo kwa kiasi fulani bado ni geni kwa wengi.

Kununua hisa

Kununua hisa ni kupata sehemu ya umiliki wa kampuni iliyoorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE). Ukubwa wa umiliki huo utategemea idadi ya hisa ulizonunua katika kampuni husika.

Kwa kadri mtu au taasisi inavyonunua hisa nyingi ndivyo umiliki wake unavyoongezeka. Kwa mfano, anayenunua asilimia moja ya hisa za kampuni huwa na asilimia moja ya umiliki wa kampuni husika.

Vivyo hivyo kwa anayenunua hisa zenye thamani ya asimilia tano ya kampuni naye anamiliki asilimia tano ya kampuni husika. Kwa maana hiyo, kukiwapo faida katika biashara husika, mwenye hisa hupata gawio la faida husika sawa na asilimia anazomiliki katika kampuni.

Mauzo ya hisa

Kampuni huuza hisa katika soko la mitaji kwa namna na sababu mbalimbali. Kabla ya mauzo ya awali, kampuni husika hupata ruhusa kutoka mamlaka dhibiti ya soko la mitaji.

Kampuni husika huandaa waraka wa matarajio au prospectus ambacho ni kitabu kinachoitambulisha kwa wanaolengwa kununua hisa. Kitabu hicho hueleza hali ya kampuni ikiwa ni pamoja na thamani yake, aina ya biashara inayofanya, mali zake, mauzo, faida na hasara, wamiliki, idadi na thamani ya hisa zote zitakazowekwa sokoni na bei ya hisa moja.

Lengo la kitabu hicho ni kumpa mnunuzi taarifa muhimu ili aweze kufanya uamuzi sahihi wa kununua au kutonunua hisa na endapo atanunua ni kwa kiasi gani afanye hivyo.

Baada ya kitabu hicho kuwekwa wazi, mauzo ya awali katika soko la msingi (primary market) hufanywa kwa kipindi maalumu kisha hufungwa, soko hilo ni pale kampuni inapouza hisa zake kwa mara ya kwanza. Baada ya hapo mauzo huendelea katika soko la upili (secondary market).

Sababu

Kampuni huuza hisa kwa sababu mbalimbali. Sababu kuu ni kukuza mtaji kutoka kwa umma badala ya kukopa kwenye taasisi za fedha au benki za biashara. Kwa mfano, kampuni huweza kuongeza mtaji kwa kuuza sehemu ya hisa zake katika soko la mitaji.

Pia, zinaweza kuuza hisa zake ili kuongeza mvuto wake kwa wawekezaji. Tanzania kwa mfano, kampuni iliyoorodhesha zaidi ya asilimia 35 ya hisa zake katika soko la hisa huweza kupata vivutio vya kikodi vinavyotolewa na Serikali.

Hata hivyo, kampuni inaweza kuuza hisa zake kwa matakwa ya sheria za nchi. Kampuni za simu na madini ni mfano wa sekta ambazo zinatakiwa kuorodhesha sehemu ya hisa zake sokoni hapa nchini.

Lengo ni kuwa na uchumi shirikishi kwa maana ya wananchi kumiliki sehemu ya uchumi. Hata hivyo, sehemu ya hisa hizo huweza kununuliwa na wawekezaji kutoka nje. Hisa zinapokuwa katika soko huongeza uwazi wa kampuni husika kwa umma. Pamoja na mambo mengine, hii husaidia udhibiti wa ukwepaji kodi unaoweza kufanywa na wahusika.

Zingatia

Ununuzi wa hisa ni uwekezaji kama ilivyo katika mwingine wowote kuna mambo kadha wa kadha ya kuzingatia. Hisa hununuliwa kwa malengo mbalimbali ambayo ni pamoja na kuweka akiba na mwisho wa siku kupata faida katika uwekezaji huo.

Ni muhimu kuelewa kuwa uwekezaji wa hisa unaweza kulipa au kutolipa. Faida za kampuni zikiongezeka wamiliki wa hisa hupata faida. Zisipoongezeka au zikishuka, huwa hakuna faida.

Ni vizuri kuwekeza katika hisa fedha ambazo hata zikipotea hutajuta sana, hivyo ni vizuri kuelewa vizuri mwenendo wa kibiashara wa kampuni husika kabla ya kuamua kununua hisa. Pia, ni vizuri kuweka lengo la kununua hisa.

Hisa zinaweza kununuliwa ili ziuzwe pale zitakapopanda bei. Pia, huweza kununuliwa ili kufaidi gawio pale faida inapotengenezwa. Malengo hayo mawili yanaweza kuchanganywa. Ni muhimu kufahamu mambo hayo kabla ya kununua hisa za kampuni uipendayo.

Jinsi ya kununua hisa

Hisa zinazouzwa kwa mara ya kwanza hupatikana kwenye soko la msingi kupitia madali au mawakala waliochaguliwa. Zinaweza kuwa benki za biashara au kampuni za udalali wa hisa.

Idadi na thamani ya hisa zinazopelekwa sokoni huwekwa wazi na kampuni husika. Bei ya hisa moja na idadi ya chini ya hisa zinazoweza kununuliwa hutangazwa. Wanunuzi wanaweza kununua kama mtu binafsi, taasisi, vikundi au namna nyingine yoyote.

Baada ya kununua, mnunuzi hupewa cheti kinachoonyesha pamoja na mambo mengine, jina, kiasi na thamani ya hisa zilizonunuliwa. Ni vizuri kuelewa kuwa kukosa kununua hisa katika soko la msingi siyo mwisho wa fursa ya kufanya hivyo.

Bado kuna nafasi ya kununua katika soko la upili. Hata hivyo ununuzi katika soko la upili hutegemea uwepo wa hisa zinazouzwa kutoka kwa wamiliki. Mara nyingi, bei katika soko la upili huweza kuwa kubwa kuliko katika soko la msingi.

Tofauti ya masoko haya mawili ipo kwenye namna ya utekelezaji wa miamala yake. Katika soko la msingi, kampuni inayouza hisa hupata fedha kutoka kwa mnunuzi au mwanahisa anayezinunua. Fedha huingia kwenye akaunti ya kampuni.

Kwenye soko la upili, mauzo hufanyika kati ya mmiliki mmoja kwenda mwingine. Kama nilivyosema hapo awali, wapo wanaonunua hisa ili waziuze zikipanda bei au kutokana na sababu nyingine yoyote. Hilo linapofanyika, kampuni husika haipati chochote kutokana na miamala inayofanyika.

Tanzania

Biashara ya hisa nchini Tanzania inafanywa DSE. Zipo kampuni kadhaa zilizoorodhesha hisa zake sokoni hapo. Mwaka huu, kampuni za mawasiliano na madini zinatakiwa kuorodhesha sehemu ya hisa zake ili kutoa nafasi ya umiliki kwa Watanzania na dunia kwa ujumla.

Miongoni mwa mambo yanayovutia ni kujua kama Watanzania watakuwa na fedha za kutosha kununua hisa zote za kampuni hizo. Hii ni fursa kwa walio tayari kununua hisa hizo.