Yawezekana mgogoro wa uongozi CUF ni sikio la kufa

Muktasari:

Serikali iliporejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, ndipo kilipoanzishwa chama cha United Front kwa upande wa Zanzibar kikiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad na upande wa Tanzania Bara kulikuwa na chama kinaitwa Civic Party kikiongozwa na James Mapalala.

Kuna methali inasema “sikio la kufa halisikii dawa”. Kwa maana kama kuna jambo limeandikiwa kuharibika, halina budi kuharibika hata kama kutafanyika juhudi nyingi. Pengine huu ndio mwisho wa CUF ambacho tangu kianzishwe kimekuwa na migogoro ya kiuongozi.

Serikali iliporejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, ndipo kilipoanzishwa chama cha United Front kwa upande wa Zanzibar kikiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad na upande wa Tanzania Bara kulikuwa na chama kinaitwa Civic Party kikiongozwa na James Mapalala.

Mwaka huohuo vyama hivi viliungana na kuzaliwa chama cha Civic United Front au CUF. Mwenyekiti akiwa Mapalala na Katibu Mkuu Maalim Seif.

Sikio la kufa lilianzia hapo ambapo mwaka 1994, Mapalala alifukuzwa uanachama, miaka michache baadaye kiliingia kwenye mgogoro mwingine wa uongozi na naibu katibu mkuu wake Bara, Michael Nyaluba ambaye baadaye alifukuzwa uanachama.

CUF iliendelea kuruka vihunzi vya migogoro ya uongozi ambapo mwaka 2003 kililazimika kumfukuza uanachama mwenyekiti wake wa Bodi ya Wadhamini, Naila Majid Jidawi. Mwaka 2015 chama hicho kiliingia kwenye mgogoro na kiongozi wake mwingine Hamad Rashid Mohamed ambaye baadaye alifukuzwa uanachama.

Mgogoro ambao unakiumiza chama hicho na pengine ile methali ya sikio la kufa halisikii dawa inaweza ikatimia ni ulioanza mwaka 2016 unaomuhusu mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba anayeungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya, baadhi ya wabunge na viongozi wengine wa chama hicho.

Kama vile chama hicho kimegawana viongozi, hivi karibuni kila upande ulifanya mkutano wake kwa kila upande kudai ulishirikisha wajumbe wa kikatiba, ajenda zilizofanana na kila upande ulitoka na maazimio ya kutuhumiana.

Mgogoro huo uliibuka kutokana na Profesa Lipumba aliyetangaza kujiuzulu uenyekiti wa chama Agosti 5, 2015, kutengua uamuzi wake huo baada ya mwaka mmoja kupita na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikamtambua.

Kurejea kwa Profesa Lipumba katika uongozi na kutambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ndiko kulikootesha mizizi ya mgogoro uliopasua uongozi ndani ya chama hicho.

Mgogoro huo umezaa makundi mawili ya wanachama, moja linaloongozwa na Profesa Lipumba na jingine likiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif. Mgogoro huo umesababisha pande hizo mbili kuburuzana mahakamani.

Hatua ya mgogoro huo ilisababisha wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif kutafuta ofisi eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam baada ya kundi la Profesa Lipumba kutwaa ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyopo Buguruni.

Mwezi uliopita ndani ya wiki kwa nyakati tofauti, kila upande uliitisha kikao chake cha Kamati ya Utendaji ya CUF kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, kisha kutoa maazimio.

Profesa Lipumba ambaye uenyekiti wake unatambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa uliitisha vikao viwili cha Kamati Utendaji na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF liliofanyika makao makuu ya chama hicho, Buguruni ambacho kilikuwa na ajenda zaidi ya tatu.

Miongoni mwa ajenda hizo, kesi za chama hizo, chaguzi ndogo za marudio za Serikali, maandalizi ya chaguzi za Serikali 2019/20, kazi za wabunge ndani ya chama hicho na hali ya kisiasa ndani na nje ya CUF.

Upande huo wa Profesa Lipumba ambao unamtambua Maalim Seif kama Katibu Mkuu wake, ulisema muungano wa baadhi ya vyama vya siasa kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hauwezi kuiondoa Serikali ya CCM madarakani hivyo liundwe shirikisho jipya.

Pia, alimtuhumu Maalim Seif kwa kukidhoofisha chama hicho kwa kutotekeleza azimio la Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la kufungua kesi Mahakama Kuu ya Zanzibar kupingwa kufuta kwa matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi na madiwani waliokabidhiwa hati za ushindi wa majimbo na shehia baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.

Profesa Lipumba, ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, anasema Maalim Seif angekuwa anahudhuria vikao vya baraza hilo lingekuwa limeshamchukulia hatua za kinidhamu, lakini kwa kuwa hafiki inakuwa vigumu ikizingatia kuwa kuna suala kuhojiwa.

“Atashughulikiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu, kwa kumpa nafasi ya kujieleza kabla ya kuchukua taratibu za kinidhamu, kisha wataleta kwenye Baraza Kuu la Uongozi kwa ajili ya hatua zaidi,” anasema Profesa Lipumba.

Maazimio hayo ya upande wa Profesa Lipumba yanapingwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar anayemuunga mkono Maalim Seif, Nassor Ahmed Mazrui kuwa upande huo hauna ubavu kumshughulikia katibu mkuu huyo kwa Lipumba siyo mwenyekiti halali wa chama hicho na kamati ya maadili anayoizungumzia haitambuliki.

Mbali na hilo, Profesa Lipumba alimtuhumu Maalim kwa madai ya kuwakumbatia viongozi wa Chadema kwa lengo la kukidhoofisha chama hicho.

Siku chache baadaye, Maalim Seif ambaye hamtambui Profesa Lipumba kama mwenyekiti wake, aliwasili jijini Dar es Salaam akitokea Zanzibar kuja kuzindua kongamano la CUF lililojadili masuala mbalimbali ikiwamo mwenendo wa chama hicho.

Katika kongamano hilo Maalim Seifa alimjibu Profesa Lipumba kuwa hawezi kwenda kuhojiwa na kamati ya maadili aliyodai kuwa ni haramu na kwamba hawana uwezo wa kumfukuza, atabaki kuwa katibu mkuu wa CUF hadi mwaka 2019 utakaoitisha uchaguzi mwingine wa chama hicho.

Baada ya kueleza hayo, siku iliyofuata Maalim Seif aliitisha kikao cha kawaida cha Kamati ya Utendaji kilichokuwa na ajenda nne kilichofanyika ofisi ya wabunge wanaomuunga mkono katibu mkuu huyo iliyopo Magomeni

Kikao hicho chini ya mwenyekiti wake, Maalim Seif kilijadili masuala mbalimbali, ikiwamo maandalizi ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho, mwenendo wa kesi zilizopo mahakamani na hali ya kisiasa.

Akisoma maazimio ya kikao hicho, Maalim Seif amewataka wanachama na viongozi wa CUF kuyapuuza yote yaliyotangazwa na Profesa Lipumba kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Pia, Maalim Seif anasema hatima ya mgogoro ndani ya chama hicho ipo mikononi mwaka mahakama ikiwa watashinda kesi yao.

Baada ya kutoa maazimio hayo siku zilizofuata Maalim Seif alianza ziara ya wiki moja Pemba iliyokuwa na lengo la kuimarisha chama hicho, ikiwa ni siku chache baada ya Profesa Lipumba kwenda huko na akisema bado wanachama wengi wa kisiwa hicho wanamuunga mkono.

Wakitoa maoni yao kuhusu mwenendo ndani ya CUF, baadhi ya wasomi wamesema mgogoro huo unawaweka kwenye wakati mgumu wanachama wa CUF wale wanaopenda mabadiliko.

Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anasema baadhi ya wanachama wanaopenda mabadiliko watashindwa kuvumilia kukaa kwenye chama ambacho viongozi wake wa juu wanatofautiana misimamo.

“Hali hii inayoendelea ndani ya CUF si dalili nzuri hasa wakati wa kuelekea 2020. Inasikitisha kwa sababu wanachama wake watashindwa badala yake watakihama chama hiki na kitakosa support (kuungwa mkono) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020,” anasema.

“Kila upande kufanya vikao siyo tatizo kwa sababu ndio afya na uhai wa chama. Tatizo vikao hivyo havizungumzii ajenda ya kuunganisha chama mezani ambayo ingewasaidia kuunganisha nguvu kwa pamoja na kuweka mazingira bora ya chaguzi zijazo,” anasema Dk Mbunda.

Dk Mbunda anasema wanaonufaika na kuvumilia hali ya mgogoro huo ni wale wanachama wenye uhusiano mzuri na waka karibu na Maalim Seif au Profesa Lipumba, lakini wale wanaopenda mabadiliko hawataweza.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema hali hiyo inawachanganya na inawapa wakati mgumu wanachama hasa wale wasiokuwa na upande wowote.

“Wanashindwa washike lipi, linalozungumzwa na Seif (Maalim) au Lipumba (Profesa), kwa sababu kila mtu anasema la kwake. Hali hii itasababisha chama kudhoofika,” anasema Profesa Mpangala.

Hata hivyo, Profesa Mpangala amewataka wanachama wa chama hicho kusubiri uamuzi wa mahakama ili kujua CUF ipi halali na ipo kwenye misingi ya kisheria,” anasema Profesa Lipumba.