Friday, July 21, 2017

ZIARA: Everton walivyotikisa D’salaam kwa saa 40

 

By Charles Abel, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ujio wa klabu ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza wiki iliyomalizika, ndio habari iliyotokea kuteka hisia za wapenzi wa soka na vyombo vya habari, ndani na nje ya Tanzania.

Timu hiyo ilitua nchini na kukaa kwa siku mbili chini ya udhamini wa kampuni ya SportPesa na ilicheza mchezo maalumu wa kirafiki dhidi ya timu kongwe ya Kenya, Gor Mahia katika mchezo ambao Everton waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Gor Mahia ilipata bahati hiyo baada ya kuilaza AFC Leopards mabao 3-0 katika mchezo maalumu wa timu zinazodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa.

Simba, Yanga, Jang’ombe Boys zilitolewa katika mashindano hayo pamoja na Tusker na Nakuru AllStars.

Msafara wageuka gumzo

Safari ya Everton kuja nchini ilianzia kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa John Lennon uliopo jijini Liverpool ambao unashika nafasi ya 13 kwa ubora katika orodha ya viwanja vya ndege nchini Uingereza.

Msafara huo ukiwa na jumla ya watu 84 ambao ni wachezaji 25, maofisa wa benchi la ufundi na utawala, waandishi wa habari pamoja na wataalamu wa tiba na lishe, walilazimika kusafiri takribani saa 10 angani na kuanzia nyakati za usiku na kutua Jumatano asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini.

Tofauti na misafara ya timu nyingine ambayo hulazimika kupitia kwenye geti la kawaida ambalo abiria wengine hutokea, msafara wa Everton ulishukia katika eneo la watu maalumu (VIP) huku ulinzi ukiwa mkali kila kona uwanjani hapo.

Muda mfupi baada ya kutua, msafara huo ulipokewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dokta Harrison Mwakyembe na baadaye uliondoka kwenda katika Hoteli ya kifahari ya Sea Cliff ambako ndiko timu ilipangwa kufikia.

Ofisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema kuwa ujio wa timu hiyo umewapa elimu ya kutosha ambayo shirikisho itatumia katika kuleta maendeleo ya soka nchini.

“Wenzetu wamepiga hatua kubwa na kama mlivyoona kuwa kuna tofauti kubwa kati yao na sisi. Naamini klabu zetu pamoja na TFF tumepata darasa tosha ambalo tukilifanyia kazi tutapiga hatua kubwa,” alisema Lucas.

Nidhamu ya ratiba

Kila ambacho Everton kwa siku zote mbili walizokuwepo Tanzania, kilikuwepo ndani ya ratiba ambayo iliandaliwa na kutolewa mapema kabla hata timu hiyo haijatua nchini ikitokea Uingereza.

Hakuna ambacho kilifanyika nje ya utaratibu uliowekwa na walijitahidi kuzingatia muda kama ulivyopangwa   kwa mujibu wa ratiba yao ilivyoonyesha jambo ambalo ni elimu tosha kwa timu zetu.

Hata baada ya kuwasili, wachezaji waliingia kwenye basi na kutulia, hakukuwa na mchezaji aliyekuwa akitangatanga kuonyesha kuwa naye yupo ama kufungua dirisha, wote walikuwa ndani wametulizana.

Baada ya kuwasili kwenye hoteli waliyofikia, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi na wale wa utawala walioambatana na timu hiyo walianza kujigawa katika makundi tofauti yaliyokwenda kushiriki matukio mbalimbali kama ratiba yao ilivyokuwa inaonyesha.

Kundi moja lililojumuisha maofisa wawili sambamba na wachezaji wanne, Ademola Lookman, Idrisa Gueye, Yannick Bolasie na nahodha Leighton Baines lilikwenda kutembelea kwenye shule ya walemavu ya Uhuru Mchanganyiko na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii.

Kwanza kwa Bolasie, Wacongoman wenzake walijipanga kumlaki, walimshangilia kuanzia JNIA hadi Sea Cliff walikofikia na walicheza muziki kumkumbusha nyumbani DR Congo.

Ratiba yao ya baada ya kufika, kwanza walitembelea kujionea majengo na vifaa vilivyotolewa na ubalozi wa Uingereza shule ya Uhuru Mchanganyiko, kucheza mechi ya kirafiki na watoto wenye ulemavu wa macho na kisha waligawa mito ya kulalia, wanasesere pamoja na skafu zenye nembo ya klabu hiyo kwa watoto hao.

Kundi lingine la wachezaji lilikwenda Uwanja wa Uhuru ambako lilifanya mazoezi ya pamoja na wachezaji wa timu ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), huku wachezaji wengine wakishiriki katika semina maalumu ya mapishi iliyofanyika katika hoteli ya Sea Cliff.

Ukiondoa makundi hayo ya wachezaji ambayo yalitawanyika kwenye maeneo mbalimbali, baadhi ya maofisa wa Everton walifanya semina maalumu kwa wanahabari huku makocha wawili wa timu hiyo wakiendesha kliniki ya soka kwa watoto wadogo pamoja na wachezaji wa vikosi vya vijana kwa timu za Yanga na Simba.

Siku ya pili, msafara wa Everton ulianzia kwa kutembelea Hospitali ya Pugu Kajiungeni na baadaye ulitembelea kituo cha utamaduni wa jamii ya Wamasai kabla ya kurudi hotelini Sea Cliff kujiandaa kwa mchezo dhidi ya Gor Mahia.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Uhuru Mchanganyiko, Anna Mshana alisema ziara ya wachezaji wa Everton shuleni kwake umekuwa na tija kwao.

“Tumezoea kuwaona kwenye luninga wakiwa wanacheza, lakini leo tumewaona moja kwa moja. Kwa kweli sisi imetupa hamasa sana kwamba kumbe tuwe tunaendelea kuwaangalia kwa sababu leo tumewaona kama mlivyo.

“Misaada mnayotupa tunaithamini sana lakini tunaomba muendelee kutupatia kwa sababu wale watoto wanatoka katika mazingira magumu kwa hiyo wanahitaji misaada mingi na hata kusoma kwao ni kwa shida na serikali peke yake haitoweza.”

“Tunapowapata wadau kama nyinyi tunapata faraja kubwa kwamba kumbe wale watoto nao wanajiona wanathaminiwa kama binadamu wengine.

“Tumefurahi na tunawashukuru sana na tunawakaribisha kwa mara nyingine,” alisema Mwalimu Mshana.

Rooney aimbwa kila kona

Si vyombo vya habari vya ndani au vile vya nje ya Tanzania pekee ambavyo vilikuwa vinalitaja bila kuchoka jina la mshambuliaji Wayne Rooney ambaye Everton imemsajili hivi karibuni akitokea Manchester United bali pia mchezaji huyo alivuta hisia za kundi kubwa la mashabiki wa soka nchini katika siku zote ambazo Everton walikuwa nchini.

Kila shabiki wa soka alitamani kupata nafasi ya ama kugusana na mshambuliaji huyo au kupiga picha ingawa hilo lilitimia kwa watu wachache kutokana na ulinzi mkali ambao mshambuliaji huyo alikuwa nao.

Kutokana na hamu ambayo mashabiki wengi walikuwa nayo ya kumuona Rooney, haikushangaza kuona mmoja wa mashabiki aliyevaa jezi ya Manchester United akivamia uwanjani na kwenda kumkumbatia mshambuliaji huyo ambaye alifunga bao la kwanza la Everton katika mchezo huo.

JK, Mwinyi waibuliwa na Everton

Mgeni rasmi wa mechi baina ya Everton na Gor Mahia alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan lakini vigogo wengi walijitokeza kuungana naye katika kutazama mechi hiyo.

Baadhi ya viongozi waliojitokeza mbali na Mama Samia ni Rais wa awamu wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya nne, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba sambamba na aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga.

Gor Mahia, Everton wagawana vipindi

Pengine Gor Mahia wangekuwa makini kutumia nafasi walizozipata kwenye kipindi cha kwanza, wangeweza kuandika historia ya kupata ushindi kwenye mchezo huo ambao hata hivyo walikuja kupoteza.

Timu hiyo ya Kenya ilitawala vilivyo kipindi cha kwanza huku wachezaji wake Dan Walusimbi na Karim Nizigiyimana wakionyesha uwezo wa hali ya juu. Hata hivyo kipindi cha pili kilitawaliwa na Everton baada ya kufanya mabadiliko ya kikosi kizima.

Fursa za biashara/Utalii

Kama alivyosema Dk Mwakyembe, ujio umekuwa na faida kwa Tanzania kutangazika nje kwani ambaye haifikirii wala kuizungumza Tanzania ameisoma na kuifuatilia kote duniani ambako Everton inafuatiliwa.

“Ni fursa kwa Tanzania kujitangaza, ujio wa Everton ni neema kubwa, tumefanikiwa na kipindi kijacho, tunataka kuona Everton inacheza mechi na timu za Simba au Yanga au timu nyingine ili Tanzania itangazike pekee,” alisema Dk Mwakyembe katika moja na mazungumzi yake.

Fursa nyingine ni kwa wafanyabiashara wa jezi, skafu, usafirishaji pamoja na hoteli ni miongoni mwa watu walionufaika na ujio wa Everton kutokana na kufanya vizuri kwa biashara zao wakitumia fursa ya ujio wa kundi kubwa la watu kutoka nje na ndani ya nchi.

“Binafsi ningependa hao Everton wakae hapa Tanzania hata kwa wiki nzima kwani biashara ya jezi zao imekuwa ikituendea vizuri kwani mashabiki wamekuwa wakizinunua kwa wingi ili wanapokwenda kutazama mechi waonekane wamevaa sare na wachezaji,” alisema mfanyabiashara Riziki Selemani.

Wasemavyo makocha

Kocha wa Everton Ronald Koeman alisifu mapokezi na uungwaji mkono ambao timu yake ilipata katika kipindi chote ambacho ilikuwa nchini na kukiri kuwa umewapa faida.

“Tulihitaji mahali tulivu ambako tungeweza kufanya baadhi ya programu zetu za kitimu na nashukuru tumefanikiwa katika hilo. Ninawashukuru Watanzania kwa ukarimu na upendo mkubwa ambao wametuonyesha ndani ya hizi siku mbili tulizokuwa hapa.

Mechi yetu dhidi ya Gor Mahia ilikuwa nzuri na tumecheza na wapinzani ambao walijitahidi kuonyesha kiwango bora ingawa Everton tulikuwa bora zaidi yao,” alisema Koeman.

“Nimefurahia kurudi tena Tanzania ambako nimepokelewa vizuri na kupewa heshima kubwa na mashabiki. Ingawa tumepoteza mchezo, nimefurahishwa na jinsi mashabiki wa hapa wanavyopenda soka na ni kitu cha kipekee,” alisema kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr.

-->