Zuma amejiuzulu, sheria inamsubiri

Muktasari:

Utawala wa karibu miaka kumi wa Zuma uligubikwa na tuhuma kali za rushwa, jambo ambalo limekigharimu Chama cha ANC kupoteza sana umaarufu miongoni mwa wananchi. Pia, uchumi wa nchi hiyo umekwenda chini.

Afrika Kusini imepata rais mpya. Jumatano iliyopita aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma alitangaza kupitia televisheni kwamba anajiuzulu papohapo. Kwa hiyo, njia ilikuwa wazi kwa makamu wake, Cyril Ramaphosa aliyechaguliwa mwezi Desemba kuwa mkuu wa chama tawala cha African National Congress (ANC) kuukamata wadhifa huo.

Utawala wa karibu miaka kumi wa Zuma uligubikwa na tuhuma kali za rushwa, jambo ambalo limekigharimu Chama cha ANC kupoteza sana umaarufu miongoni mwa wananchi. Pia, uchumi wa nchi hiyo umekwenda chini.

Kamati Kuu ya ANC Jumanne iliyopita pia ilimpa Zuma kauli ya mwisho: Aachie nafasi yake ili ikamatwe na Ramaphosa, ama sivyo ilimtishia kwamba Alhamisi inayofuata atakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye bungeni. Kinyume na tamko lake la hapo kabla la kuibishia Kamati Kuu ya chama chake na kudai kwamba hajatendewa haki kwa vile hajafanya kosa lolote – na kama liko, basi aarifiwe. Usiku wa Jumatano alibwaga manyanga.

Alifanya hivyo kwa huzuni kubwa. Aliomba abakishwe madarakani hadi Juni mwaka huu ili akabidhi madaraka kwa utaratibu mzuri, lakini hajapewa nafasi hiyo. Wabunge wa ANC walikuwa tayari kuungana na wale wa vyama vya upinzani kumng’oa kutoka kiti cha urais, na hata kumshtaki, ikiwa lazima, kwa kuvunja Katiba.

ANC ilibidi itengane na Zuma kwa vile alikuwa mzigo mkubwa kwa chama hicho. Tuhuma za rushwa pamoja na kashfa nyingine zilimwandama kiongozi huyo, na bila shaka ANC sasa inapumua kwa kuondokewa na mzigo huo.

Chama hicho kimewataka wafuasi wake wamuunge mkono rais mpya na kinatarajia kwamba Ramaphosa atakirejeshea heshima na ataweza kuwashawishi wananchi wakipigie kura kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2019.

Chama cha ANC kimekuwa kikiitawala nchi hiyo ya Ras ya matumaini mema tangu ulipotokomezwa utawala wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

Chama Kikuu cha Upinzani katika Afrika Kusini, Democratic Alliance (DA), kimeitaka ANC iwaandame washirika wa Zuma ambao wanatuhumiwa kuhusika katika vitendo vya rushwa na kuziendesha vibaya taasisi za Serikali. Kiongozi wa DA, Mmusi Maimane, alisema: “Zuma alijenga mfumo wa rushwa uliokwenda ndani kabisa na ambao ulipenya katika kila sehemu ya Serikali na nyendo za kihalifu.”

Afrika Kusini sasa inamuangalia Ramaphosa atachukua hatua gani. Je, atazifumbia macho tuhuma zote na nyingi zinazomkabili Zuma?

Maimane anataka Bunge la nchi hiyo livunjwe kwa haraka na uchaguzi mkuu mpya uitishwe. Anasema: “Hatuna tatizo la Zuma, tuna tatizo la ANC. Huu ni wakati ambapo turejee kwa wananchi wa Afrika Kusini na lazima tuombe kibali chao kipya.”

Chama cha mrengo wa shoto cha Economic Freedom Front (EFF) kilitoa ombi Alhamisi kwamba Bunge lijivunje lenyewe na mwishowe uchaguzi mkuu mpya uitishwe kabla ya wakati wake wa Aprili 2019, lakini bila ya kufanikiwa.

Ilivyokuwa uongozi wa Bunge ulilikataa ombi hilo, wabunge wa EFF walitoka kwenye ukumbi wa Bunge hata kabla ya Ramaphosa kuchaguliwa, ishara iliyoonyesha kwamba kutakuwapo mivutano.

Wakati mambo yote hayo yanatokea, Jumatano hiyohiyo polisi wa Afrika Kusini walipekua nyumba za familia ya Gupta, raia mwenye asili ya Kihindi na ambayo ni washirika wa kibiashara wa Zuma.

Inasemekana kwamba ndugu watatu wa familia ya Gupta walitumia uhusiano wao na Rais wa Afrika Kusini kujipatia ushawishi, na hata kufikia hadi kuwa na uwezo wa kushauri ni mtu gani awe waziri, tena wa wizara gani. Pia, waliweza kujipatia kandarasi nono serikalini wakiutumia urafiki waliokuwa nao na Rais.

Akina Gupta na Rais Zuma wote wamekana kama wamefanya jambo lolote kinyume na sheria. Vyombo vya habari vya Afrika Kusini viliripoti kwamba katika msako huo wa polisi watu kadhaa walikamatwa na pengine huo ndio mwanzo wa hatua za kisheria kuchukuliwa.

Ramaphosa itamlazimu ndani ya muda mfupi ujao achukue msimamo imara ili aweze kuonyesha kwamba amepata mafanikio ya haraka. Afrika Kusini hivi sasa imekabwa na ukosefu mkubwa wa ajira, kunakosekana usawa katika uchumi pamoja na matatizo mengine.

Katika hotuba yake ya mwanzo bungeni kama rais wa nchi, Ramaphosa alisema atafanya kazi sana na vyama vingine vya kisiasa ili kutowavunja moyo wananchi wa Afrika Kusini, tena atafanya kazi hiyo kwa unyenyekevu, ukweli na heshima. Vita dhidi ya rushwa kwake yeye ni kipaumbele. Hotuba yake hiyo fupi ilishangiliwa na kupigiwa vifijo.

Cyril Ramaphosa aliwahi kuwa kiongozi wa wafanyakazi wa migodi na pia kuwa mwandani wa shujaa wa uhuru, Nelson Mandela. Rais wa Afrika Kusini hachaguliwi na wananchi, bali na Bunge, akiwa ni kiongozi wa chama kilichopata wingi wa viti bungeni. Yeye huwa mkuu wa nchi na Serikali.

Lakini, katika kijiji cha Nkandla, katika Jimbo la Kwa Zulu Natal, alikozaliwa Zuma, na ambako huko amejenga jumba la kifahari, watu kadhaa waliandamana kumuunga mkono. ANC katika jimbo hilo ilisema kwamba Zuma amefanyiwa njama na wapinga mapinduzi ili aondoshwe madarakani. Baada ya Zuma kujiuzulu, hata hivyo, sarafu ya Rand ya Afrika Kusini ilipanda thamani yake.

Kabla ya kuwa rais wa nchi, Jacob Zuma aliwahi kuwa gerezani kwa miaka 10 katika Kisiwa cha Robben ambako alizuiliwa na madikteta wa Kizungu wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Katika miaka hiyo alikuwa na wakati wa kutosha, hata akaanzisha klabu ya wacheza dama miongoni mwa wafungwa. Kutoka Kisiwa cha Robben alikuwa akiziangalia nyumba kubwa za wazungu zilizokuweko bara, mwisho wa upeo wa macho yake, nyumba zilizojengwa kwa damu na jasho la Waafrika.

Huo ulikuwa wakati uliomfanya Zuma awe alivyo sasa, mjanja, bingwa wa mizengwe, mchezaji wa siasa kama vile anavyolicheza dama – vyeusi dhidi ya vyeupe au sisi dhidi ya wao.

Zuma na ANC walishinda mchezo, na utawala wa ubaguzi wa rangi ukashindwa. Sahibu wake aliyeishi naye gerezani, Nelson Mandela, alibadilika na akawa mpatanishi wa Waafrika Kusini. Lakini, Zuma yeye alisema: Sasa ni zamu yetu, sasa tutavuna kutokana na mapambano tuliyoyaendesha.

Alijilipa kwa kuipora dola kulia na kushoto, alibadilika na kuwa mtuhumiwa wa ufisadi mkubwa kabisa, mla rushwa wa kutupwa, akikubali kutiwa ndani ya mifuko ya matajiri

Sasa Zuma hayuko kwenye madaraka. Hiyo ni habari nzuri kwa Afrika Kusini. Lakini si habari nzuri moja kwa moja. Tusishangilie mapema mno. Bado hadi dakika hii Chama cha ANC hakijayakana waziwazi, bayana kabisa, matendo ya kihalifu yaliyofanywa na aliyekuwa rais wake na aliyekuwa rais wa nchi, mbali na zile tuhuma alizowahi kukabiliana nazo za kubaka. Hata hivyo, angalau sasa Afrika Kusini imepata nguvu na ujasiri wa kutosha kuondokana na “mchezaji huyu wa sinema.“

Zuma amejiuzulu ili kukwepa kupigwa teke na Bunge, amehepa kushtakiwa na kupata aibu kubwa zaidi. Lakini, Mahakama ya Afrika Kusini inabidi sasa imshtaki na impeleke gerezani ili mwanzo mpya kabisa uweko kwa nchi hiyo.

Nchi hiyo imeweza kufikia mambo makubwa – kuutokomeza ubaguzi wa rangi na kipindi cha enzi ya mpito kimeanza. ANC lazima isafishe meza yake, lazima iseme na ikiri kwamba imemwachia kwa karibu miaka 10 Zuma afanye yale aliyoyafanya.

Ramaphosa inambidi aombe radhi kwa mamilioni ya Waafrika Kusini ambao waliachwa bila ya matatizo yao kushughulikiwa huku rais wa nchi akishughulika kupora mali za dola na kukubali kuhongwa na matajiri.

Swali ni kama Ramaphosa ataweza kufanya hivyo au ataendelea na siasa ya mchezo wa dama ya Zuma, akitaka tu kushinda katika michezo ya “danganya toto”. Tunamtakia Ramaphosa kila la heri. Afrika Kusini haistahili wala haistahiki kudidimia chini zaidi kuliko ilivyofikia wakati wa Zuma.

Kuna mtu aliyeniambia kwamba Ramaphosa ni tajiri mno, anabeba magunia mengi ya mamilioni ya Rand za Afrika Kusini juu ya kichwa chake. Kwa hivyo, hatokuwa na haja au sababu ya kutaka kuhongwa. Suala la rushwa kwake yeye huenda lisizuke.