Matokeo haya dalili njema kwa masomo ya sayansi

Bakari  Kiango 

Muktasari:

  • Nayasema hayo baada ya kuona ufaulu kwa baadhi ya masomo ya sayansi umepanda tofauti na miaka iliyopita, hali inayonipa imani sasa kuwa masomo hayo yanaanza kupendwa na wanafunzi.

        Tanzania ya sayansi inawezekana endapo mkazo utawekwa kuanzia ngazi ya chini kwa kuboresha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia masomo ya sayansi.

Nayasema hayo baada ya kuona ufaulu kwa baadhi ya masomo ya sayansi umepanda tofauti na miaka iliyopita, hali inayonipa imani sasa kuwa masomo hayo yanaanza kupendwa na wanafunzi.

Januari 9, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alitangaza matokeo ya upimaji wa darasa la nne na ule wa kidato cha pili yote iliyofanyika Novemba mwaka jana.

Katika takwimu za jumla alisema wanafunzi wamefanya vyema katika mitihani hiyo hasa katika masomo ya Fizikia, Hesabu na Kemia kwa kidato cha pili na sayansi kwa darasa la nne yote haya ufaulu umepanda ukilinganisha na mwaka 2016.

Hata hivyo, bado nguvu zinahitajika katika somo kama Biolojia ambalo ufaulu wake umeshuka katika matokeo hayo.

Hatua hii ya ufaulu wa masomo ya sayansi kupanda ni dalili njema kwa kuandaa kizazi cha Tanzania ya sayansi, hasa ikikumbukwa kuwa miaka iliyopita masomo haya yalikuwa na changamoto kubwa wanafunzi.

Ufaulu huu unaonyesha dalili nzuri kwa wanafunzi hawa kufanya vizuri katika masomo hayo katika mitihani ya kidato cha nne na ile ya kidato cha sita kabla ya kuingia vyuo vikuu kujiendeleza zaidi.

Ilifika hatua hadi baadhi ya watu walidiriki kuyaita masomo haya kuwa ni ‘Janga la Taifa’, huku wanafunzi wengi wakiyapa kisogo.

Kuna hoja kwamba tatizo la masomo ya sayansi, linasababishwa na uchache wa walimu, vifaa vya kujifunzia na maandalizi duni ya wanafunzi katika ngazi za chini, hivyo kufifisha juhudi za Serikali kutaka wanafunzi wajikite zaidi katika masomo hayo.

Msimamo wa Serikali ni kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo hayo ili hatimaye ndoto ya Tanzania ya viwanda itimie kwa kuwatumia wataalamu wa ndani.

Aliyekuwa mratibu wa masomo ya sayansi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Doroth Mwaluko aliwahi kukaririwa na gazeti hili, akisema watoto wengi hawapendi kusoma masomo hayo.

Lakini sasa hivi naona mambo yanabadilika kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha ufaulu unapanda.

Huku ni kuweka msingi wa kujenga kizazi cha wanasanyasi ambao sio tu wataweza kushindana katika soko la ajira, lakini pia kuwa tayari kuendeleza nchi yetu kiteknolojia.

Naamini ufaulu huu haukuja kirahisi, kuna jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau wengine kuhakikisha wanafunzi wanafaulu.

Ufaulu wa masomo ya sayansi ukiongezeka, ni dhahiri kuwa tunajenga Taifa lenye kizazi cha watu waliobobea katika masomo hayo, hali itakayochangia juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayotaka kutimiza ndoto ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Kwa nyakati tofauti kuanzia katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na baada ya kuchaguliwa Dk John Magufuli amekuwa akisema Serikali yake itakuwa ni ya viwanda.

Ni dhahiri ufaulu huu unaendana na dhamira ya Rais, kwa kuwa tunaandaa wataalamu wa kuja kuanzisha na kusimamia viwanda hivyo.

Nawapongeza wanafunzi wote waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi. Safari imeshaanza wasirudi nyuma, tunahitaji taifa lenye watalamu wengi wa sayansi kama ilivyo katika fani nyingine.

Bakari Kiango ni mwandishi wa Mwananchi