UCHAMBUZI: Matumaini yapo Kili Queens na Serengeti Boys

Dk Mshindo Msolla

Muktasari:

  • Timu hizo zimekuwa na mafanikio katika mashindano ya kufuzu kwenye michuano mikubwa ya CAF na ile ya ubingwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Tanzania katika siku za hivi karibuni imekuwa ikifanya vizuri katika ngazi ya timu za Taifa za vijana na zile za wanawake. Ni dhahiri kwamba timu hizo zimewapa watanzania furaha.

Timu hizo zimekuwa na mafanikio katika mashindano ya kufuzu kwenye michuano mikubwa ya CAF na ile ya ubingwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Nichukue nafasi hii kurejea baadhi ya mafanikio ya timu hizi: Twiga Stars ilifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa bila kuisahau Tanzanite ambayo nayo iliwahi kufanya vizuri na kuwa mabingwa wa Afrika.

Aidha, Kilimanjaro Queens imechukua ubingwa wa CECAFA kwa miaka miwili mfululizo (2017 na 2018 wakiwa nje ya nchi.

Hakuna asiyejua uwezo wa timu ya Serengeti ambao walitufikisha kwenye fainali za Afrika (ambayo sasa ni Ngorongoro) na Serengeti ya sasa ambao wamechukua ubingwa wa CECAFA wakiwa Burundi.

Mafanikio hayo si kidogo na yanaonyesha dalili njema kwa mustakabali wa mchezo huu muhimu. Ni dhahiri mafanikio haya yasingepatikana bila TFF kuwa na mipango madhubuti ya kuuendeleza mchezo huu. Hili limewezekana kwa sababu zifuatazo;

Ligi ya Wanawake

Ligi ilishirikisha klabu nyingi kitaifa, imesaidia kuibua vipaji ambavyo vilikuwepo mikoani na hivyo kuongeza wigo wa wachezaji wapya kuonekana. Tumeona kwamba pamoja na timu hiyo kuwa na wazoefu wachache, wengi wa wachezaji walikuwa vijana. TFF pia ilitumia vizuri michezo ya Umitashumta na Umiseta kupata vipaji vipya.

Michezo ya Umitashumta na Umiseta

Michezo hii imesaidia pia kupata wachezaji wenye vipaji na wengi wao wanakuwa wamepata mafunzo stahiki kutoka kwa walimu wao kwa sababu walimu wengi wamekuwa washiriki wazuri wa kozi za ukocha.

Wachezaji kutoka katika shule wana manufaa kwa sababu elimu waliyonayo inawawezesha wachezaji kuyapokea maelekezo ya walimu na kuwa na ubunifu .

Vituo vya kuendeleza michezo ya vijana

Pamoja na ukweli kwamba vituo vya kukuza vipaji vya wanamichezo ni vichache, vile vilivyopo vimesaidia sana kuwapata wachezaji wenye vipaji. Vituo kama kile cha TFF pale Karume, JK Park, Rolling Stones, Azam, Alliance na Morogoro vimechangia kwa kiasi kikubwa timu zetu za vijana kupata wachezaji mahiri.

Timu za taasisi kuchangia kukuza na kulinda vipaji

Pongezi nyingi ziwaendee JKT kwa kuwa msaada mkubwa hususan kwenye kuchangia wachezaji wengi kwenye timu ya Kilimanjaro queens. Ni dhahiri kwamba wachezaji wengi waliotoka JKT waliweza kupata mafunzo stahiki kwa kuzingatia kwamba timu za jeshi nguzo yake kubwa ni nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Taasisi kama Polisi na Magereza wana nafasi kubwa ya kuwa na timu za wanawake za kandanda ambazo zikiwepo zitaongeza wingi wa wachezaji na kujipatia ajira na kuzidi kuwa na timu za Taifa bora.

Ni vyema TFF kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kwamba mafanikio haya yanaendelezwa.

Soka la vijana likisimamiwa vizuri, linaweza kututoa hapa tulipo badala ya kuwekeza nguvu nyingi kwenye timu ya soka ya wakubwa ambayo imekuwa ikishindwa kufuzu kwenda kwenye fainali za mashindano ya kimataifa.

Niliwahi kuwashauri wafadhili wanaoisaidia Taifa Stars kwamba kwa fedha nyingi wanayoitumia bila mafaninikio ni vyema nguvu hizo wangezielekeza kwenye timu za vijana ambako matokeo yake yangekuwa bora zaidi kuliko timu yetu ya wakubwa.