Matumizi yaliyopitiliza ya intaneti ni chanzo cha magonjwa ya akili

Muktasari:

Utegemezi wa mitandao hiyo unahusishwa na sonona, wasiwasi na mfadhaiko hivyo kuathiri uwezo wa kuwaza na kuamua wa mhusika.


Uraibu wa mitandao ya intaneti unaweza kuwa chanzo cha magonjwa mengine ya akili, ripoti inasema.

Utegemezi wa mitandao hiyo unahusishwa na sonona, wasiwasi na mfadhaiko hivyo kuathiri uwezo wa kuwaza na kuamua wa mhusika.

Maendeleo ya teknolojia yameleta mabadiliko makubwa katika matumizi ya mitandao kutokana na taarifa za kila aina kupatikana kwa urahisi zaidi kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta hivyo kurahisisha maisha ya wengi.

Watu hutumia muda mwingi mitandaoni wakitafuta taarifa, kufanya ununuzi ya bidhaa au huduma, kucheza michezo tofauti iliyopo, kutazama video na picha au kutumiana baruapepe.

Licha ya faida nyingi zilizopo, matmizi ya mitandao hiyo yakizidi huweza kusababisha magonjwa au matatizo ya akili mfano sonona, msongo wa mawazo na wasiwasi.

Katika utafiti uliofanywa na watafiti kutoka nchini Canada umebaini kuwa matumizi ya mitandao yaliyopitiliza yanaweza kuwa kisababishi cha matatizo mbalimbali ya afya ya akili miongoni mwa wanafunzi hasa wa vyuo vikuu.

Katika tafiti huo watafiti walitathmini matumizi ya mtandao kwa wanafunzi 254 kutoka Chuo Kikuu cha McMaster kilichopo Ontario kwa kuzingatia muda ambao mwanafunzi husika ameutumia kwenye intaneti na madhara yanayoweza kujitokeza.

Kwa kutumia kipimo cha kubaini kiasi cha uraibu wa intaneti au Internet Addiction Test (IAT) kama wanavyokiita pamoja na vigezo vingine walivyoviweka walipata matokeo yasiyo na shaka kuwa matumizi yaliyopitiliza ya intaneti ni chanzo cha magonjwa ya akili.

Majibu ya utafiti huyo ambayo yaliwsilishwa kwenye mkutano wa mwaka wa madaktari bingwa wa magonjwa ya akili (ECNP) uliofanyika huko Vienna, Austria yalionyesha wengi wa washiriki hao walikuwa wameathirika.

Majibu yalibainisha wanafunzi 33 walikutwa na viashiria vya kuathirika na matumizi ya mtandao na 107 walikutwa na matatizo yatokanayo na matumizi ya mitandao.

Kiongozi wa jopo hilo, daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka chuo kikuu hicho, Profesa Michael Van Ameringen alisema: “Matumizi ya mtandao yaneobgezeka sana ndani ya miaka 18 iliyopita. Watu wanawasiliana kwa njia ya video, mitandao ya kijamii, kufuatilia habari na mengi mengine. Matumizi yakizi husababisha tatizo.”

Utafiti huo umebaini kuwa wengi wa washiriki walioathirika na matumizi ya intaneti wanashindwa kudhibiti ratiba zao za kila siku huku wakiwa na msongo wa mawazo, wavivu na wasioweza kuzingatia wafanyalo. Walibainika pia kupangilia mambo yao pamoja na kuratibu muda.

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili, Profesa Jan Buitelaar wa Hospitali ya Nijmegen ya Chuo Kikuu cha Radboud huko Uholanzi anasema: “Uraibu wa intaneti ni sehemu ambayo haijafanyiwa utafiti wa kutosha lakini matumizi yaliyopitiliza yanaweza kusababisha uraibu.”

 

Tanzania

Mtaalamu wa afya ya akili, Dk John Chikomo anasema kuwa ni kweli mtu ambaye ana utegemezi mkubwa katika mitandao anaweza kupata matatizo ya akili na kwakuwa mitandao huweza kuiteka akili ya mtu na kumfanya awe tegemezi wa mitandao.

Dk Chikomo anaunga mkono matokeo ya utafiti huo na anatoa mfano wa mtu ambaye amezoea kunywa pombe inapotokea ameikosa kwa muda huanza kujisikia kama anaumwa na mwenye mawazo lakini mara tu anapopata pombe hali yake huimarika na kuwa mwenye amani.

Hali kadhalika katika mitandao endapo mtu amejizoesha kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii kama facebook, twiter, whatsApp na kutazama video hufarijika lakini inapoikosa hali yake kubadilika ndipo mtu anaweza kupata sonona, msongo wa mawazo na wasiwasi.

 

Dalili

Wataalamu wanaeleza kuwa kuna dalili nyingi za mtu aliathirika na matumizi yaliyopitiliza ya mitandao ya intaneti. Kujisikia furaha kila unapotumia kompyuta au simu kama njia pekee ya kumfariji ni moja ya dalili hizo.

Nyingine ni kushindwa kufuata ratiba ipasavyo kiasi cha kuweza kuacha mambo ya msingi na kutumia muda mwingi kuperuzi mitandaoni. Wakati mwingine hamu ya kufanyakazi hupungua.

Inapotokea hupendi kazi yako kama ilivyokuwa hapo awali, wataalamu wanaeleza kuwa ni dalili kuwa intaneti inaaza kukuathiri. Hii inaweza kwenda sambamba na kujisikia uvivu.

Wengine hawathamini muda. Baadhi ya watumiaji wanaoathirika hawawezi kuthamini muda wao kwani huona ni vyema kukaa na kuperuzi mitandaoni kuliko kufanya mambo ya msingi kama kusoma au kazi za ofisini.

Kutokuwa mkweli. Kutokana na kupitiwa mtu huanza kuwa muongo kutokana na kushindwa kutimiza ahadi.

Hali hii inajidhihirisha hasa kwa vijana ambao wanaopenda kuangalia video mitandaoni hasa za ngono kutokana na kutekwa akili.

 

Athari;

Dk Chikomo anaeleza mazoea haya huweza kuibua tabia mpya ambazo mtu hakuwanazo kutoka na taarifa anazokutana nazo mtandaoni. Kwa wanafunzi anasema wengi wanashindwa kufaulu masomo yao kwa kiwango cha juu kutokana na kutegemea intaneti kuwapa majibu ya kila kitu.

“Ukishakua mlevi wa mitandao ni vigumu kuacha. Wagonjwa wanahitaji ushauri nasaha kutoka kwa mtaalamu ili kuwapa njia mbadala,” anasema Dk Chikomo.

Mwalimu sekondari jijini Dar es Salaam, Emmanuel Mhando anasema madhara hayo yanajitokeza kwa wanafunzi wengi sio wa vyuo vikuu pekee.

“Vijana wengi wanaomiliki siku za kisasa wana kumba na tatizo hili. Wanafunzi wengi wanatumia simu zao kutafuta majibu ya maswali na kazi mbalimbali za darasani. Wanazitegemea zaidi simu kuliko akili zao,” anasema.

Anaeleza kuwa wapo baadhi ambao hukamatwa wakizitumia darasani hivyo kulazimika kuwaita wazazi au walezi wao ili kuwashirikisha juu ya umiliki wa vifaa hivyo vya mawasiliano.

“Familia zinapaswa kusaidia hili. Vijana wanatakiwa wasaidiwe ili waweze kufanya shughuli nyingine wanazotakiwa kuzitekeleza,” anasema Emmanuel.

 

Matibabu;

Suala la matibabu kwa mtu ambaye anatatizo la utegemezi wa mitandao ni jambo amabalo limetajwa kuwa ni gumu kwa namna yake kutokana na kwamba mtu anahitaji ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa akili ili kumpa njia mbadala ya kuachana na tabia hizo.

“Ni vigumu kumwambia mtu aachane na matumizi ya mitandao ikiwa yeye mwenyewe anaona ni jambo zuri kwake kinachohoitajika ni ushauri kutoka kwa mtaalamu,” anasema Dk Chikomo.

Dk Elizabeth Wampembe wa Chuo cha Kikuu cha Muhimbili (Muhas), anasema matatizo ya kijamii na kifamilia yanaweza kumfanya mtu kuona hiyo ndiyo njia pekee ya kujifariji na kuepuka matatizo yanayomkabili.

“Mtu akiitegemea intaneti huweza kuathirika kisaikolojia na kubadilika kitabia kwa ujumla hali inayoweza kumfanya ajihusishe na mambo yasiyo ya kawaida,” anasema Dk Eliza.

Anasema kutokana na hali ilivyo sasa watu wenye uwezekano wa matatizo ya akili kutokana na matumizi ya mitandao ni mkubwa kutokana na kutumia muda mwingi wakiperuzi mitandaoni kunakochangiwa na upatikanaji wa intaneti ya uhakika.