Mawasiliano muhimu kwenye bomoabomoa

Muktasari:

  • Bomoabomoa hiyo imekuwa ikifanyika katika maeneo ambayo ni hifadhi ya barabara, reli au mabondeni na maeneo mengine ambayo kisheria hayatakiwi kuwa makazi ya watu.

Katika siku za karibuni kumekuwa na bomoabomoa katika maeneo mbalimbali sababu kubwa ikiwa ni baadhi ya watu kujenga maeneo ambayo hayatakiwi kwa makazi ya binadamu.

Bomoabomoa hiyo imekuwa ikifanyika katika maeneo ambayo ni hifadhi ya barabara, reli au mabondeni na maeneo mengine ambayo kisheria hayatakiwi kuwa makazi ya watu.

Ni jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa nia njema, kwa sababu kuna ambao wanaishi katika maeneo hatarishi yasiyotakiwa kwa makazi ya binadamu hivyo Serikali inafanya wajibu wake wa kulinda maisha ya watu wake. Sababu nyingine ya bomoabomoa hizo ni kutokana na maendeleo ya miundombinu na uwekezaji ambayo kutokana na wakati tulionao hayawezi kuzuilika.

Kunapotokea maendeleo yoyote huwa kuna gharama zake na miongoni ni kama hazo za baadhi ya watu kubomolewa nyumba au hata mashamba kutegemeana na aina ya uwekezaji.

Tumeshuhudia watu kadhaa wakipata maumivu hayo ya kubomolewa nyumba zao kwa sababu hizo tulizoeleza na miongoni mwao ni wakazi wa Jangwani, katika Bonde la Mto Msimbazi, Dar es Salaam.

Katika bomoabomoa iliyofanywa juzi kwenye eneo hilo, vurugu ziliibuka na hata kusababisha basi la abiria na Kituo cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kuvunjwa vioo kwa mawe.

Msemaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Nelly Msuya alisema hatua hiyo imetekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili kuipisha Dawasa kujenga mtambo wa majitaka na kwamba nyumba zilizokuwa eneo hilo zilishavunjwa na kilichokuwapo ni kusafisha mabanda yaliyokuwa yamebaki maeneo hayo.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi eneo hilo wakiungana na wengine, walifanya vurugu wakipambana na askari wa jiji waliokuwa wakisimamia ubomoaji huo.

Hatutaki kuingia kwa undani kuhusu tukio hilo, lakini ambacho kinatusikitisha ni nguvu kubwa ambayo hutumika wakati mwingine bila sababu katika ubomoaji wa nyumba za watu. Inajulikana kwa kila mmoja kuwa nyumba hizo zimejengwa kwa gharama kubwa kutokana na kipato cha kila mtu, hivyo inapofika ubomoaji suala hilo lisiwe ubabe tu.

Elimu ya kuhusu ubomoaji huo, mawasiliano ya mara kwa mara na mikutano kati ya wananchi na mamlaka husika vingeweza kuepusha vurugu hizi.

Inasikitisha kuona kuwa baadhi ya watendaji wakitumia nguvu kubwa bila kuzingatia kuwa wanaobomolewa ni binadamu na wanaumia hivyo kutumia nguvu kupita kiasi ni kuwapa machungu mara mbili.

Hatupingi ubomoaji, tunachosisitiza ni mawasiliano kati ya taasisi za Serikali, watendaji na wananchi ili wote wawe wanazungumza lugha inayofanana.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alizuia bomoabomoa ya zaidi ya nyumba 17,000 katika jiji la Dar es Salaam ambayo ilitakiwa kuanza wakati wowote katika Hifadhi ya Bonde hilo la Mto Msimbazi.

Pia alisitisha ubomoaji wa nyumba zaidi ya 300 za baadhi ya wakazi wa Kata ya Toangoma, Temeke ambao zinazodaiwa kujengwa katika eneo tengefu la Serikali kwa ajili ya kuendeleza ukanda wa kijani maarufu kama “Bonde la Makamba.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akitoa msimamo huo alisema Rais Magufuli ameshangazwa na bomoabomoa hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zitawaumiza wananchi na kwamba hana taarifa zake.

Tunajiuliza kama mkuu wa mkoa hakuwa na taarifa ya kinachofanyika katika mkoa wake itakuwaje kwa wananchi wa kawaida kuhusu kupewa taarifa za ubomoaji huo?