Mfumo ndio unaosumbua mafanikio ya Stars

Muktasari:

  • Katika mchezo huo, pamoja na kufurukuta mwanzoni, wachezaji wa Taifa Stars walishindwa kuhimili vishindo vya Algeria ambayo mara ya mwisho iliichapa mabao 7-0.

Wiki iliyopita, timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ ilichapwa na Algeria mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki mjini Algiers.

Katika mchezo huo, pamoja na kufurukuta mwanzoni, wachezaji wa Taifa Stars walishindwa kuhimili vishindo vya Algeria ambayo mara ya mwisho iliichapa mabao 7-0.

Mchezo huo uliochezwa Alhamisi usiku ni sehemu ya mechi za Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa).

Timu hiyo inatarajiwa kujitupa tena kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na DR Congo, katika mchezo mwingine wa kalenda ya Fifa kesho Jumanne.

Kipigo hicho kimeibua mjadala kila kona kuhusu mustakabali wa soka ya Tanzania katika ushiriki wa mashindano ya kimataifa.

Kwa muda mrefu Watanzania wameshindwa kupata furaha kutokana na kufanya vibaya kwa Taifa Stars katika mashindano mbalimbali.

Zipo sababu lukuki zinazotajwa kuhusu kuboronga kwa Taifa Stars, baadhi wakitoa lawama kwa benchi la ufundi au wachezaji na wengine wakiponda maandalizi ya zimamoto kwa kikosi hicho.

Hata kabla ya mchezo na Congo, Mwananchi lilifanya mahojiano na makocha wa ndani na wale wa kigeni kwa nyakati tofauti walieleza sababu kadhaa.

Mfano, baadhi ya makocha wa Tanzania waliohojiwa walisema kuwa sababu kubwa ni timu hiyo kupatiwa mechi lainilaini za Burundi, Eritrea, Djibouti na wakafika mbali kusema wakati mwingine hata Somalia.

Kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo alisema Algeria haikuwa saizi ya Tanzania na sehemu kubwa walicheza kwa kutojiamini na wakawafunga.

Alitaka timu hiyo kucheza na mataifa kama Ghana, Senegal, Nigeria ili kuwajengea wachezaji kujiamini.

Kwa makocha wa kigeni wanaofundisha timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, wametoa maoni akiwemo Kocha wa Simba, Pierre Lechantre aliyesema tatizo kubwa linaloitafuna soka la Tanzania ni kukosa msingi imara wa wachezaji vijana.

Alisema Tanzania itapata taabu kupata mafanikio kimataifa kwa kuwa haina msingi bora wa vijana na Tanzania inaweza kupata timu bora ya Taifa ikiwa kutakuwa na mfumo bora wa kuibua na kuwatengeneza wachezaji chipukizi.

Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alisema Tanzania ina wigo mpana wa kupata wachezaji hodari wenye uwezo mzuri wa kuipa mafanikio endapo benchi la ufundi litakuwa makini katika uteuzi wa wachezaji.

Naye Kocha wa Mbao, Ettiene Ndayiragije alidai TFF, linatakiwa kuwa na ratiba endelevu ya timu za Taifa hasa ngazi ya vijana.

Kuna mengi ambayo kimsingi yanahitaji usimamizi wa karibu. Tunaweza kusema soka ya Tanzania ni kama mgonjwa anayehitaji uangalizi wa karibu.

Bila kuwa na misingi ya vijana, hatuwezi kupiga hatua, kwa kuwa mchezaji hata akiwa na kipaji kama hakuandaliwa, hatakuwa na utaalamu wa soka.

Wachezaji wengi wanaibuka tu Ligi Kuu na kuteuliwa Taifa Stars na wakati mwingine wanajichezea kwa kuwa mpira unapigwa kwenda mbele.

Algeria wameonyesha soka inavyochezwa, mipira inapita kwenye njia zake na hiyo ni darasani kama anavyosema kocha wa Simba kwa Taifa Stars.

Ukianza kuyapambanua hapa ya soka la Tanzania, madudu ni mengi, cha msingi basi, TFF na wahusika kuyafanyia kazi haya yanayosemwa ili soka ya Tanzania lipige hatua. Watanzania wanataka kufurahi.