Spurs yawapumzisha mastaa wake

Muktasari:

  • Kocha Mauricio Pochettino ametaja kikosi cha wachezaji 25 watakaoshiriki mechi za kirafiki kujiandaa na msimu wa mwaka 2018-19 ‘International Champions Cup’.

London, England. Klabu ya Tottenham Hotspurs, imewapa mapumziko wachezaji wake wote waliocheza fainali za Kombe la Dunia 2018.

Kocha Mauricio Pochettino ametaja kikosi cha wachezaji 25 watakaoshiriki mechi za kirafiki kujiandaa na msimu wa mwaka 2018-19 ‘International Champions Cup’.

Mastaa waliopumzishwa ni pamoja na Harry Kane, Dele Alli, Eric Dier, Kieran Trippier na  Danny Rose (England), Hugo Lloris (Ufaransa), Jan Vertonghen, Mousa Dembele na Toby Alderweireld (Ubelgiji).

Pochettino ameendelea kumpumzisha Harry Winks anayesumbuliwa na kifundo cha mguu ‘ankle’ kwa muda mrefu na msafara wa timu hiyo uliondoka jana Jumapili kuelekea Los Angeles, Marekani.

Kikiwa Marekani kikosi cha Tottenham mbali ya kujifua kitacheza mechi kadhaa na miamba ya soka ya Hispania na Italia, AS Roma, Barcelona na AC Milan.

Kocha huyo ameamua kuwajumuisha kikosini Christian Eriksen, Davinson Sanchez na Son Heung-Min, walioshiriki fainali hizo za Kombe la Dunia lakini timu zao ziling’olewa katika hatua ya makundi.